loader
Picha

ANZILAN MAYANI Mtoto mwenye ulemavu anayechora kwa kutumia miguu

“NIMEKWENDA kumtafutia nafasi katika shule za walemavu Iyunga na Katumba zilizopo Tukuyu mkoani mkoani Mbeya, lakini kote nikaambiwa hawawezi kukaa na mtoto ambaye hawezi kujitegemea kwa mambo kama kula mwenyewe, kutandika kitanda; asiyeweza kwenda chooni mwenyewe na asiyeweza kuoga mwenyewe eti mpaka aogeshwe maana kumpata mtu wa kumsaidia yeye pekee.”

Ndivyo anavyosema mama mzazi wa mtoto Anzilani Mayani (14), mkazi wa Ilolo wilayani Mbozi anapozungumzia hali ya ulemavu wa mtoto huyo na pia, kukosekana kwa nafasi ya masomo kwa mtoto huyo.

Anzilani ni mtoto mwenye ulemavu wa viungo ambaye licha ya kufikisha umri wa miaka 14 sasa, hakuwahi kukanyaga shuleni kwa sababu ya vikwazo anavyopata kutokana na hali yake, lakini hata hivyo, licha ya kutotembea, kuongea wala mikono kufanya kazi, amekuwa akiwasahangaza watu wengi kutokana na kipaji chake cha uchoraji kwa Kwa mujibu wa mama huyo, mtoto wake ana ulemavu wa viungo vyote kwani hawezi kuongea, hawezi kushika kitu wala hawezi kusimama wala kutembea, hivyo anapata mahitaji yake ikiwa ni pamoja na kulishwa chakula kwa kusaidiwa na mama pamoja na ndugu “Pamoja na mtoto huyu (Anzilani) kutobahatika kwenda shule wala kufundishwa na mtu yeyote akiwa na miaka 14 sasa, hakuwahi kufundishwa na mtu kuhusu uchoraji…”

Mama huyo anasema hata alipohamia mkoani Songwe kutoka Mbeya alipozaliwa Anzilani, aliambiwa Shule ya Msingi Mwenge iliyopo wilayani Mbozi, inatoa huduma kwa watoto wenye ulemavu. Eda anasema: “… Kwa kweli ukosefu wa mabweni na miundombinu mingine isiyo rafiki kwake, ni mambo yanayoendelea kumkosesha haki ya kupata elimu mtoto wangu huku akionekana kuwa ana kipaji kikubwa cha kuchora pasipo hata kwenda shuleni.”

Mwandishi wa makala haya alipotembelea nyumbani kwa mtoto huyo, alishuhudia namna anavyoonesha kipaji chake kwa kuchora picha kwa kuangalia picha zilizopo kwenye magazeti, au kwa kumwangalia mtu kisha kuanza kuchora. Mama wa mtoto huyu (Eda) anasema mtoto huyo ni wa mwisho kati ya watoto wake wanne. Alizaliwa vizuri kama walivyo wengine, lakini baada ya kuzaliwa, hakutoa sauti yoyote, hali ambayo kitaalamu ni moja ya ishara za kuwapo tatizo.

“Mwanangu niligundua kuwa ana ulemavu baada ya kuambiwa na madaktari, lakini ikiwa ni wiki ya pili tangu azaliwe kutokana na kukaa muda mrefu bila kutoa sauti baada ya kuzaliwa. Hali hiyo ilinifanya nihudhurie hospitali mara kwa mara ili kupata ufumbuzi,” anasema. Alipoulizwa wakati wa kujifungua mtoto wake alikumbwa na shida gani, mama wa mtoto huyo anasema: “Wakati wa kumzaa sikupata shida yoyote, lakini niliona tofauti kwamba, alipokuwa analia, alikuwa hatoi sauti, badala yake, tunaona machozi yanamtoka ndipo tukaingiwa na wasiwasi na kuanza kufuatilia hospitali.”

Daktari Bingwa Magonjwa ya Wanawake na Afya ya Uzazi Hospitali ya Mkoa wa Songwe, Dk Lukombodzo Lulandala anasema wakati mwingine changamoto kama hiyo, hutokana na hitilafu za uumbaji. Anasema zipo pia MAKALA Inatoka Uk. 9 sababu zinazoweza kusababisha tatizo hilo ikiwa ni pamoja na utumiaji wa dawa wakati wa ujauzito hasa chini ya miezi mitatu ya mwanzo. Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Akinamama na Uzazi katika Chuo Kikuu cha Sayansi za Tiba cha Muhimbili (Muhas), Dk Peter Wangwe, anasema mara nyingi watoto wanaochelewa kulia baada ya kuzaliwa huchelewa kukua, kuongea; ni wazito kufikiri na huwa na ugumu katika kujitegemea.

Kipaji cha kuchora kilivyoonekana Eda anasema licha ya mtoto wake kutokwenda shule kabisa, alianza kuonesha kuwa na kipaji hicho pale alipowaona watoto wenzake wameshika madaftari na wanasoma, ndipo na yeye akaanza kuchora kwa kutumia mguu wake wa kulia akishikilia penseli kwa kutumia vidole vya mguuni. “Mara nyingi huchora picha baada ya kuangalia zilizo kwenye magazeti na muda mwingine, humchora mtu atakayemwona, na huchora kwa kutumia vidole vya mguuni kwa kuwa mikono na viungo vingine havifanyi kazi kabisa,” anasema.

Mtoto alivyokosa haki yake ya elimu Anasema alitamani na mpaka sasa anatamani mwanawe apate shule kama walivyo watoto wengine, lakini juhudi zake ziligonga mwamba kutokana na kukataliwa katika shule za wanafunzi wenye ulemavu alizojaribu kuomba nafasi eti kwa madai kuwa, itakuwa vigumu kumhudumia kwa kuwa ana ulemavu wa viungo, hasa kushindwa kutembea.

Mama huyo wa mtoto Anzilani Mayani anasema hali hiyo ilimfanya akose nafasi ya shule kwa mtoto wake katika shule maalumu za wanafunzi wenye mahitaji maalumu za Iyunga na Katumba mkoani Mbeya. Alisema ilionekana kuwa, hali hiyo itaongeza gharama kubwa kutokana na kuhitaji kumpata mtu wa kumsaidia mtoto huyo kwa mahitaji yake ya kipekee. “…Ukosefu wa mabweni na miundombinu mingine isiyo rafiki kwake ndio umeendelea kumkosesha mwanangu haki ya kupata elimu ingawa ana kipaji cha hali ya juu kiasi cha kuchora kwa kutumia vidole vya miguu kushika penseli na bila hata kuwa amekwenda shule,” anasema Eda. Majirani wanena Martha Mwakabendi ni mmoja wa majirani wanaomfahamu vizuri mtoto Anzilani.

Anasema wanashangaa kipaji cha mtoto huyo huku akiwaomba watu na serikali kuanzisha shule za watoto wa aina hiyo ili waweze kuonesha vipaji vyao. “Tunashangaa kipaji cha huyu mtoto; yaani licha ya kutokwenda kabisa shuleni, lakini bado anajitahidi kutushinda hata sisi tunaotumia mikono na pia tulio kwenda darasani,” anasema Martha na kuongeza: “Huyu mtoto akisomeshwa, kipaji chake kitakua zaidi.” Jirani mwingine Bupe Godfrey anasema wanafarijika kuona kipaji alicho nacho mtoto huyo cha kuchora bila ya hata kufundishwa na mtu yeyote.

Anaiomba jamii, taasisi za dini na serikali, kuungana kumsaidia mtoto huyo ilia pate masomo na kukitumia ipasavyo kipaji chake kwa manufaa yake, gfamilia, jamii na taifa kwa jumla. “Mtoto huyu akisaidiwa kupata masomo na akapelekwa katika shule maalumu kukuza kipaji hicho ambacho watu wengi hawana, atafika mbali kimaendeleo,” anasema.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Nicodemas Mwangela anasema katika Mkoa wa Songwe, kuna ukosefu wa shule za walemavu, hali inayosababisha watoto wengi kukosa haki ya kupata elimu. Anasema serikali mkoani Songwe inajipanga kujenga shule maalumu kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu ili wapate elimu na kuonesha vipaji vyao muhimu. Hivi ndivyo mtoto Anzilani hushika penseli na kuchora kwa kutumia vidole vya mguu (Picha na Baraka Messa). Anzilani akionesha kipaji chake cha kuchora kwa kutumia mguu wake wa kulia (Picha na Baraka Messa).

MSEMO wa wahenga ‘Majuto ni mjukuu, huja baada ya kitendo’ ...

foto
Mwandishi: Baraka Messa

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi