loader
Picha

Siko tayari kuongoza nchi ya machozi -JPM

BAADA ya kushuhudia wafungwa na mahabusu wengi katika Gereza Kuu la Butimba jijini Mwanza wakimlalamikia kwa kubambikiwa kesi na polisi, Rais John Magufuli amesema hayuko tayari kuongoza nchi ya machozi.

Alitoa kauli hiyo alipozungumza na wananchi wa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma jana kwenye mkutano wa hadhara. Magufuli alisema ameshatoa maelekezo kwa Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vinavyohusika na mahakama kuhakikisha wanapita kwenye magereza yote nchini na kuzungumza na mahabusu ili wale wasio na hatia waachiwe huru.

Alisema hali aliyoiona katika gereza hilo ilimpa picha kamili ya hali ya magereza yote ilivyo nchini kutokana na msongamano wa wafungwa na mahabusu ambao wengine wamefungwa au kuwekwa mahabusu kwa uonevu kwa kubambikiwa kesi.

Katika Gereza la Butimba alishuhudia idadi kubwa ya mahabusu wanaofikia 925 na wafungwa 1,000 huku wengine wakiwekwa mahabusu kwa uonevu kwa zaidi ya miaka minane kwa kisingizio kwamba upelelezi haujakamilika. “Watu wanahangaika, katika magereza ni shida, siwezi kuongoza nchi ya machozi, machozi haya yataniumiza, wala siwezi kutawala nchi ya watu wanaosikitika ambao wako kwenye unyonge na unyonge wao unatokana na kuonewa,”alisema Rais Magufuli.

Magufuli alisema ni hatua sahihi iliyochukuliwa juzi na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Augustine Mahiga na DPP Mganga ya kuwaachia huru watu 75 katika Gereza la Butimba, watu 100 Bariadi, watu 52 Mugumu Serengeti, watu 6 Tarime, watu 24 Bunda na watu 43 Kahama. Alisema iliwachukua Waziri na DPP muda wa zaidi ya saa saba kuzungumza na watuhumiwa katika gereza hilo na kubaini watu wengine hawakuwa na makosa na wengine walikuwa na makosa ya kawaida kama vile wizi wa kuku na wengine wangestahili vifungo vya muda mfupi wa miezi sita lakini cha kusikitisha wamekaa mahabusu kwa zaidi ya miaka minane.

Kwa mujibu wa Rais, jana viongozi hao walikwenda katika Gereza la Kasungamile na Gereza la Geita. Alisema amewaagiza wakitoka huko waende kwenye mikoa yote nchini ili maelfu ya watuhumiwa ambao wanashikiliwa isivyo halali waweze kuachiwa huru.

“Hata wale polisi waliohusika na wizi wa dhahabu kule Mwanza wameachiwa huru kwa sababu hata kwa kuwaona tu, unaweza ukajua kupitia macho yao, nao nimewarudisha kazini kwa sababu walikuwa wameshafukuzwa kazi, ila iwe fundisho kwa askari wanaopenda rushwa, lakini pia polisi msiwaonee raia wanyonge kwa kuwabambikia kesi, siyo kitu kizuri, tumwogope Mungu,” alieleza Magufuli.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliendesha harambee ya kuchangia Shule ya Msingi Sagara iliyopo Kongwa baada ya vyumba vinane vya madarasa kuezuliwa kwa upepo hivi karibuni. Shule hiyo imeelezwa kuwa na jumla ya wanafunzi 1,200.

Katika harambee hiyo jumla ya Sh milioni 6.5 zilipatikana pamoja na mifuko 328 ya saruji huku yeye mwenyewe akichangia Sh milioni 5. Aliwataka watu wote waliotoa ahadi kuhakikisha wanakamilisha michango yao ndani ya mwezi huu.

Awali, Mbunge wa Kongwa ambaye pia ni Spika wa Bunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, aliishukuru serikali ya Magufuli kwa kuwapatia Sh bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Sh milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya na Sh milioni 400 nyingine kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Ugogoni na fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara.

Ndugai pia alimwomba Rais Magufuli kuienzi Kongwa kwa kurejesha kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kuwa eneo hilo ndiyo lilikuwa kitovu cha ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika. Magereza Kwa upande wake Msemaji wa Jeshi la Magereza nchini, Amina Kavirondo, alisema kuwa Jeshi hilo linazidi kujizatiti kukabiliana na wafungwa na mahabusu wanaoingia na vitu visivyoruhusiwa gerezani kama vile simu na vitu vingine.

Alisema mfungwa ni binadamu kama wengine na ana mbinu za kiuhalifu, hivyo anapokuwa gerezani anajitahidi kutafuta mbinu ya kuishi kwa urahisi, ikiwemo kuingiza vitu vilivyokatazwa, lakini wajibu wa jeshi ni kuzuia jambo hilo kwa usalama wa wafungwa wengine, taasisi na watendaji wa Magereza.

Afande Kavirondo alisema wanatumia njia ya kuwakagua kwa kuwapekua na kuongeza kuwa mbinu za kihalifu duniani zinabadilika kutokana na kukua kwa matumizi ya teknolojia, hivyo hata teknolojia ya kuwabaini watu wanaobeba dawa za kulevya nayo imebadilika. Alisema wao kama Jeshi kulingana na uwezo wao wa kibajeti watajitahidi kupata vifaa vya kisasa kwa ukaguzi japo vifaa hivyo ni gharama na watafanya kadri bajeti itakavyokidhi na wataanza na magereza machache.

RAIS John Magufuli amesema Waziri wa Mambo ya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi