loader
Picha

Majaliwa aonya NEC, asasi Daftari la Wapigakura

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametaka watendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa weledi katika uboreshaji wa uandikishaji wa wapigakura bila kuingiza itikadi za kisiasa.

Aidha waziri mkuu ametaka asasi za kiraia kutoa elimu ya umuhimu wa uandikishaji wapigakura bila kuvisemea vyama vya kisiasa kwa namna yoyote. Waziri mkuu alisema hayo wakati akizindua uboreshaji wa daftari hilo katika viwanja vya shule ya msingi Mandela Manispaa ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro.

“Waandikishaji wa daftari la wapigakura, tumieni lugha nzuri, fanyeni kazi hii kwa weledi, msiulize anatoka chama gani cha siasa zingatieni kama ametimiza vigezo na ni mtanzania, hayo mengine msiyaingize huko,” alisema.

Alisema serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa baadhi ya wananchi ambao kwa makusudi watataka kujiandikisha mara mbili ingawa mfumo wa kielektroniki uliopo utawabaini mara moja.

Alitaka pia vyama vya siasa kufuata utaratibu uliowekwa na tume katika kuwasilisha malalamiko na kasoro zinazojitokeza wakati wa uboreshaji wa daftari hilo badala ya kwenda katika vyombo vya habari. “Naipongeza NEC kwa jitihada iliyofanya katika majaribio na sasa wakati wa uzinduzi wa daftari hili. Niwahakikishie kwamba hakuna mwananchi atakayeachwa wakati wa uandikishaji lakini pia niwatahadharishe kwamba hakuna mtu atakayepiga kura bila kujiandikisha, nenda katimize haki yako,” alisema.

Majaliwa alitaka wakati wa kujiandikisha watendaji wa tume kutoa kipaumbele kwa makundi maalumu, yakiwamo ya wazee. walemavu, wajawazito na wale wenye watoto wachanga waweze kuandikishwa mapema ili wasipoteze haki yao kikatiba.

Alisema NEC imetoa elimu kwa jamii nzima kuhusu umuhimu wa kujiandikisha na kutaka vijana ambao ndio mara yao ya kwanza kujitokeza kujiandikisha ili waweze kupiga kura hapo mwakani.

“Tume imetenga mashine za BVR 3000 nchini kwa ajili ya kujiandikisha kuanzia leo hadi Julai 24 mwaka huu, nchi nzima, naelezwa kuwa vituo navyo vimeongezwa kutoka 36,549 vilivyokuwepo mwaka 2015 hadi vituo 37,407 vilivyopo mwaka huu, tuvitumie kikamilifu,” alisema.

Mapema Waziri wa Nchi Ofisi ya Wazisi Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema wamezingatia matakwa ya kisheria katika maboresho ya daftari. Alisema kwa kushikisha wadau wote wa uchaguzi vikiwamo vyama vya siasa, makundi maalum, dini, asasi za kiraia na waandishi wa habari ili kushughulikia changamoto kwa wakati ili kuhakikisha kila mtu anapata haki yake.

“Uboreshaji unaofanyika sasa utalifanya daftari la kudumu la wapigakura kuwa hai kwa kuwaondoa wale waliopoteza sifa kwa kufariki na sasa kuweza kutumika katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, kulingana na mahitaji ya kisheria yaliyopo,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage alisema kifungu cha 15 (5) cha sheria za taifa ya uchaguzi, sura ya 343 kikisomwa pamoja na kifungu cha 21 (5) cha sheria ya uchaguzi ya serikali za mitaa kinaipa tume mamlaka ya kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura.

mMwenyekiti alisema pia tume iliendesha zoezi la uhakiki wa vituo vya kuandikisha wapigakura nchini ambapo vimeongeza vituo vya kujiandikisha kutoka vituo 36,549 hadi 37,407 nchini kote. Alisema vituo vitafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12 jioni na kwamba hakuna mwenye sifa ya kuandikishwa atakayeachwa.

RAIS John Magufuli amesema Waziri wa Mambo ya ...

foto
Mwandishi: Nakajumo James, Moshi

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi