loader
Picha

‘Dhibitini kampuni za bima danganyifu’

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) Kanda ya Kati, kuhakikisha inadhibiti kampuni zinazofanya udanganyifu katika sekta ya bima mkoani humo.

Akifungua Maadhimisho ya Siku ya Bima kwa Kanda ya Kati iliyofanyika mkoani hapa kwenye Viwanja vya Nyerere Square, Dk Mahenge alisema udanganyifu na ucheleweshaji wa kulipa fidia umekuwa ukikatisha tamaa wananchi hususani wawekezaji kujiunga na huduma za bima.

Alisema ili sekta ya Bima iweze kuwa na manufaa ni vyema vitendo vya udanganyifu, ikiwa ni pamoja na kutoa bima feki, kulipa fidia kwa wakati kufanyika kwa umakini mkubwa. Aidha, Dk Mahenge alisema mbali na sifa za kuondokana na idadi ya wanaoghushi, lakini bado kunahitajika elimu ya kutosha kwa Watanzania, kwani wengi hawajawa na uelewa kuhusu bima na faida yake.

Aliwataka wenye kampuni kujali sheria wakati wa kulipa bima ili watu wafaidi matunda yao kwani haina maana watu kupata majanga lakini inachukua muda mrefu kuwalipa haki yao licha ya kukamilisha taratibu zote. Naye, Meneja wa TIRA, Kanda ya Kati, Stella Rutaguza alisema kutokana na operesheni walizokuwa wakifanya kila mara imesaidia kupunguza uhalifu na malalamiko kwenye sekta ya bima.

Alisema katika operesheni ya mwaka 2017, walikamata magari 42 na pikipiki 19 zikiwa na bima feki na watu wanne walikamatwa kutokana na kufanya uhalifu. “Lakini katika operesheni kubwa tuliyoendesha hivi karibuni, hawakupata bima feki kama ikivyokuwa kipindi cha nyuma. Kwa upande wa malalamiko pia yamepungua kwani mwaka 2017 kulikuwa na malalamiko 17 mwaka 2018, malalamiko 13 na mwaka 2019 tumepokea malalamiko matatu,” alisema.

Rutaguza alisema kwa sasa kuna watoa huduma za bima wamefikia 27 kutoka 10 waliokuwepo mwaka 2015. Aidha, maadhimisho hayo yamekwenda sambamba kwa mamlaka, mawakala, madalali na kampuni za bima zimetoa msaada wa vifaa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma vyenye thamani ya Sh milioni 5.4.

Akikabidhi vifaa hivyo, Rutaguza alisema wametoa kitanda kimoja cha kujifungulia, mashuka, blanketi na vyombo vya taka, lengo likiwa ni kuchangia huduma ya afya. Naye, Muuguzi Mfawidhi wa hospitali hiyo, Stanley Mahundo alishukuru msaada huo na kuahidi kuitumia kama ilivyokusudiwa. Alisema kwa sasa serikali imekuwa ikiimarisha utoaji wa huduma katika hospitali za umma na kuwa kwa sasa hospitali hiyo ambayo inahuduma zote za kibingwa dawa zinapatikana kwa asilimia 98.7.

RAIS John Magufuli amesema Waziri wa Mambo ya ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi