loader
Picha

Ujenzi barabara ya Kabingo - Kasulu - Manyovu kwa kiwango cha lami wanukia

Serikali ipo katika hatua za mwisho kuanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Kabingo - Kasulu hadi Manyovu yenye urefu wa kilomita 260 Kwa kiwango cha lami ikiwa ni hatua ya kuendelea kuufungua mkoa huo katika miundombinu ya barabara mkoani Kigoma.

Utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara hiyo unatarajiwa kuwa wa muda mfupi kutokana na kugawanywa katika sehemu nne ambazo ni Manyovu - Kasulu (km 68.25), Kanyani - Mvugwe (km 70.5), Mvugwe - Nduta (km 59.35) na Nduta - Kabingo (km 62.50).

Akizungumza katika hafla ya kuutambulisha mradi huo mkoani humo kwa viongozi wa Serikali ngazi ya mkoa, wadau wa Sekta ya Ujenzi na Wabunge, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Patrick Mfugale, amesema tayari Serikali imepata fedha za mkopo wa nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo na kwamba kazi inayoendelea hivi sasa ni kukamilisha taratibu za kumpata mzabuni.

"Mpaka sasa zabuni ya mradi wa barabara hii imeshatangazwa na ujenzi utaanza hivi karibuni mara baada ya taratibu nyingine kukamilika", amesisitiza Mfugale.

Amebainisha kuwa mradi huu ni wa mfano kwani utahusisha miradi mingine ya kijamii inayogusa moja kwa moja wananchi katika Sekta ya Elimu, Maji na Afya.

Ametaja miradi hiyo kuwa ni Ukarabati wa masoko ya Makere na Manyovu, Ujenzi wa Sekondari ya Buhigwe na Shule ya Msingi Busunzu, Ujenzi wa vituo vya mabasi vya Manyovu na Kabingo, Kusambaza maji katika maeneo ya Busunzu, Kasulu, Buhigwe na Manyovu, Uboreshaji wa kituo cha Afya cha Makere, Ununuzi wa magari manne ya Wagonjwa (Ambulance) na Ukarabati wa Hospitali ya Kasulu na Kibondo.

Akifungua warsha hiyo kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, amesema kuwa mradi huo ni moja ya miradi mikubwa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaosaidia kuinua uchumi wa nchi sambamba na kuunganisha mkoa wa Kigoma na mikoa mingine pamoja na nchi jirani.

"Mradi huu utaandika historia mpya katika nchi ya Tanzania kwani ni moja ya barabara pekee inayounganisha nchi yetu na nchi jirani iliyokuwa imebaki katika kiwango cha changarawe", amesema Prof. Ndalichako.

Ameongeza kuwa utaratibu wa kuwafahamisha wadau na wananchi kuhusu ujio wa miradi utasaidia kutatua changamoto zitakazojitokeza na kupata ushirikiano wa karibu wa maoni ambayo yatawezesha kufanikisha utekelezaji wa mradi huo ndani ya muda, gharama na ubora unaotakiwa.

Naye Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Alex Mubiru, ameeleza kuwa Benki hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali na kuhakisha kuwa miradi hiyo inakuwa chachu ya kukua kwa uchumi na kupunguza umaskini.

Ameongeza kuwa Benki imeweza kuandaa fedha za utekelezaji wa miradi mikubwa mitatu (3) ambayo ni ujenzi wa barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu (km 260), Dodoma Outer Ring (km 110.2) na ujenzi wa barabara Tanga - Pangani - Bagamoyo (km 121) ikiwa ni lengo la kufungua fursa mbalimali za maendeleo nchini Tanzania.

Warsha hiyo ya siku mbili yenye lengo la kuwafahamisha wadau mbalimbali kuhusu mradi huo imehusisha Mawaziri na Wabunge wanaotoka eneo la mradi, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi wa Wilaya zilizopo mkoani humo, Maafisa Watendaji wa Misitu, Madini, Ardhi, Shirika la Umeme (TANESCO), Maji na Shirika la Mawasiliano (TTCL).

RAIS John Magufuli amesema Waziri wa Mambo ya ...

foto
Mwandishi: Isdory Kitunda

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi