loader
Picha

Mlemavu afungiwa miaka 18

KIJANA mwenye umri wa miaka 18, Chiba Malongo, mkazi wa kijiji cha Mahama, Kata ya Chilonwa, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma anahitaji msaada kutoka kwa wasamaria wema.

Kijana huyo anaishi kwa kufungiwa ndani ya banda lililojengwa kwa miti kutokana na ulemavu wake.

Licha ya ulemavu alionao kumfanya asiweze kula mwenyewe, kuzungumza, kujisaidia, kijana huyo amekuwa akichana na kuvua nguo anazovalishwa na anatoa sauti ya mungurumo mithili ya mnyama.

Baba yake mzazi, Daud Malongo amesema mjini hapa kuwa huyo ni mtoto wake wa kwanza na kuwa alizaliwa mwaka 2001 katika zahanati ya kijiji cha Nzali iliyopo kata ya Chilonwa mkoani Dodoma.

“Serikali inisaidie nimehangaika na mtoto huyu tangu kuzaliwa kwake hospitali nimeenda hadi Mirembe nimefika, kwa waganga wa kienyeji nimeenda, makanisani kwenye maombi, kwa Mungu nimeenda hata Loliondo kwenye kikombe cha babu nimefika lakini sikuweza kupata namna ya kumsaidia kumtoa katika hali aliyonayo,” amesema baba huyo na kuongeza kijana huyo hushinda bandani jioni wanamwingiza ndani.

Akiwa ndani ya banda hilo kijana huyo amekuwa akitumia muda mwingi kula upindo wa kanga aliyofungwa lubega .

“Alizaliwa kwa tabu mama yake aliumwa uchungu kuanzia saa 11 alfajiri mpaka alipojifungua saa tatu usiku na mtoto hakulia, alikuwa hali wala hanyonyi.

Alikuwa akipewa maji yenye sukari na maziwa ya ng’ombe baada ya siku nne ndipo alipoanza kulia,” alisema na kuongeza mtoto huyo alizaliwa akiwa na uzito wa kilo tano na kadri alivyoendelea kukua alianza kuonesha tabia tofauti, alikuwa akilia bila kunyamaza na kukaa chini mpaka aamue na alipoanza kutembea mwendo wake ulikuwa wa kasi sana.

Alisema kutokana na dhiki ya kumlea mtoto wake na kuhitaji usalama wake na matunzo yenye uhakika mwaka 2010 alienda kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu cha Miuji Dodoma na kuambiwa sifa za watoto wanaochukuliwa kituoni hapo lazima atambue anakoenda, aweze kula mwenyewe na kujisaidia.

Alisema aliwaeleza sifa hizo mtoto wake hana wakasema aende kuishi na mwanae hivyo amebaki naye.

Malongo alisema pia alivyoona hali ya mtoto wake alifikiri atapata msaada hospitalini kwani alionesha dalili za kuwa na ulemavu wa akili, hivyo mwaka 2012 alimpeleka hospitali ya Mirembe kupata tiba.

Mzazi huyo alisema aliwaona madaktari wa hapo na walimpatia dawa za kutumia lakini hali yake ilibaki vile vile hata alipotumia dawa hivyo hakurejea hospitali kwani akitumia dawa hali ilikuwa mbaya zaidi.

Alisema mwaka 2014 kuna mwalimu mmoja wa shule ya sekondari kutoka mkoani Kagera aliahidi kumpa msaada, akapiga picha kumpelekea mfadhili, akapigiwa simu na kuulizwa maswali kadhaa lakini alisema kutokana na hali ya ulemavu aliyonayo mtoto wake wakasema itawawia vigumu kumsaidia kwa chochote.

Tabia zake

Malongo alisema mtoto huyo anapenda kula vyakula vizuri tu, kama ugali na samaki, nyama, maziwa, maharage, wali lakini kama wakimpa mrenda au kande anakataa kula akiachwa bila ulinzi hutoroka.

“Hapendi mzungumze wakati mnakula, mkizungumza anapata hasira anamwaga chakula, hawezi kula mwenyewe mpaka alishwe, nguo anavua hataki kuvaa, ana hasira sio za kawaida , anaweza kumaliza mwezi hataki maji ya kunywa, napata tabu kwenye malezi ya huyu mtoto, kusafiri kwangu tabu,” alisema.

Alisema kutokana na kuvua nguo na kuzichana, inabidi wamvalishe lubega ingawa hutafuna upindo wake na pia anatafuna sana vidole na nguo na kila siku saa 12 asubuhi huwa anaogeshwa na kuvalishwa nguo. Malongo aliiomba serikali iangalie njia ya kumsaidia kwani anasumbuka juu ya malezi ya mtoto huyo.

Mama mzazi wa mtoto huyo, Rose Mwaluko alisema mtoto huyo tangu akiwa mdogo alikuwa hawezi kushika chochote kupeleka mdomoni na hali hiyo iliendelea hadi alipoanza kutembea, hata akimsogezea chakula mpaka amlishe na hakubali kukaa na mtu mwingine zaidi ya baba, mama na bibi yake.

Ofisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Sophia Swai alisema wanaangalia namna watakavyoweza kumsaidia mtoto huyo kwani licha ya ulemavu alionao ana haki zake za msingi.

TATIZO sugu la mimba za utotoni kwa wanafunzi wa shule ...

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi, Chamwino

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi