loader
Picha

Azam, KCCA mechi ya kisasi leo

KOCHA wa Azam FC Ettiene Ndayiragije amesema mchezo wa leo wa fainali Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati Kombe la Kagame ni wa kisasi.

Akizungumzia mchezo huo jana kupitia sauti iliyotumwa na Msemaji wa klabu hiyo Jaffar Maganga, Ndayiragije alisema kwa kuwa mchezo wa kwanza wa makundi walipoteza 1-0 dhidi ya KCCA, hawatakubali tena iwe hivyo.

“KCCA ni timu nzuri tulikutana nao hatua ya makundi tulikuwa bado hatujaunganika vizuri, tunawafahamu nina imani mechi itakuwa bora zaidi na sisi tunahitaji kulipiza kisasi,”alisema.

Ndayiragije alikiri kuwa mchezo hautakuwa rahisi kwa kila mmoja kutokana na umuhimu wake, wakitaka kuweka historia ya kulichukua mara tatu mfululizo na KCCA wanataka kuweka historia ya kulitwaa baada ya kulikosa kwa miaka mingi. Mabingwa hao watetezi walifanikiwa kufika hatua hiyo baada ya kuitoa AS Maniema ya DR Congo kwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya kucheza dakika 120 bila kufungana.

Aidha, wapinzani wao KCCA walitinga hatua hiyo baada ya kuwaondosha Green Eagles ya Zambia kwa mikwaju ya penalti 4-3 kufuatia kupata sare ya mabao 2-2 ndani ya muda wa nyongeza.

Azam FC ambayo ndio bingwa mtetezi wa michuano hiyo inayoandaliwa na Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), inahitaji kutetea taji hilo ililotwaa msimu uliopita baada ya kuifunga Simba mabao 2-1 katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Iwapo watafanikiwa kulitwaa tena itakuwa ni mara ya tatu.

Mara ya kwanza walilitwaa mwaka 2015 kwa kuichapa Gor Mahia ya Kenya mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

KCCA wanaingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kulikosa taji hilo mwaka 1979 walipocheza fainali dhidi ya Abaluya FC kwa sasa inajulikana kama AFC Leopards ya Kenya baada ya kupoteza kwa bao 1-0.

Ushindi dhidi ya Azam FC leo utawafanya kuweka historia nyingine mpya kwao kuchukua taji hilo kwa mara ya pili baada ya kulichukua kwa mara ya kwanza mwaka 1978.

BAADHI ya makocha na wachambuzi wa soka nchini ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi