loader
Picha

Kadi yako ndiyo kura yako jitokeze kujiandikisha mapema

“MAMBO mazuri hayataki haraka” lakini pia kuna msemo wa Kiswahili usemao: “Kawia ufike’’ unaomaanisha kuwa, haijalishi utatumia muda gani kufika pale unapokusudia kufika, hata uwe muda mrefu kiasi gani muhimu ni uweze kufika ulipokusudia.

Hatimaye, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imetimiza moja ya jukumu lake la kikatiba kwa kuanza uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura ikiwa ni hatua muhimu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.

Uzinduzi wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura uliofanyika mkoani Kilimanjaro na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa umeanza katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha na vivyo hivyo, utaendelea katika mikoa yote kwa mujibu wa ratiba itakayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kumekuwa na kilio cha muda mrefu cha wadau wa uchaguzi nchini wakitaka kufanyika kwa maboresho katika Daftari la Kudumu la Wapigakura ili kuwawezesha Watanzania wenye sifa za kuandikishwa katika daftari hilo, waandikishwe.

Wadau hao wa uchaguzi vikiwemo vyama vya siasa wamekuwa wakitoa kilio hicho kutokana na kile wanachokiona kuwa, ni kupungua kwa wanachama wao ambao wangeweza kuwa na mchango katika chaguzi kwani kigezo kikubwa zaidi cha mtu kupiga kura, ni kuwe ameandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapigakura.

Daftari la Kudumu la Wapigakura lilianzishwa chini ya Ibara ya 5(3)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977. Tume ya Taifa ya Uchaguzi imekuwa ikitekeleza uandikishaji wa wapiga kura kwenye daftari hilo kwa kuzingatia Ibara ya 74(6)(a) na (e) ya Katiba hiyo.

ANAYESTAHILI KUANDIKISHWA KUWA MPIGAKURA

Kifungu cha 10 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 pamoja na Kifungu cha 15(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, kinataja sifa za mtu atakayeandikishwa kuwa mpigakura. Sifa hizo ni pamoja na mtu kuwa raia wa Tanzania; ametimiza umri wa miaka 18 au zaidi; na hajapoteza sifa kwa mujibu wa Sheria za Uchaguzi au sheria nyingine yoyote iliyotungwa na Bunge.

Aidha, Kifungu cha 11 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 pamoja na Kifungu cha 16 cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, vinataja sifa za mtu kutoandikishwa Sifa hizo ni pamoja na mtu kuwa raia wa nchi nyingine; kuwa amethibitishwa kuwa hana akili timamu; amehukumiwa adhabu ya kifo au anatumikia adhabu ya kifungo kinachozidi miezi sita na amepoteza sifa za kuwa kuwa mpigakura kwa mujibu wa sheria za uchaguzi au sheria nyingine yoyote iliyotungwa na Bunge.

Itakumbukwa kuwa, hoja kuhusu Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura imekuwa ikiibuka mara kwa mara hata katika vikao maalum vya wadau mbalimbali likiwemo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Itakumbukwa wakati akitoa kauli ya serikali, kuhusu uboreshaji wa daftari la Kudumu la Wapigakura katika kikao cha hivi karibuni cha Bunge jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde alisema Nec ilikuwa katika hatua za mwisho za kuanza uboreshaji wa majaribio.

Muda mfupi baada ya kauli ya Mavunde, Tume hiyo (Nec) ilitangaza kuanza kwa mchakato wa uboreshaji wa daftari wa majaribio katika Kata za Kibuta katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo na Kata ya Kihonda katika Manispaa ya Morogoro. Katika kutimiza mojawapo ya maadili yake ya msingi ya kuwa chombo kinachotekeleza majukumu yake kwa uwazi na katika hali shirikishi.

Tume iliitisha mkutano na wadau wake wakuu yaani vyama vya siasa. Kupitia mkutano na vyama vya siasa, Tume ilibainisha baadhi ya mambo yaliyokuwa yakiendelea katika kuelekea uboreshaji. Mambo hayo kama yalivyobainishwa na Mwenyekiti wa Tume Jaji (Rufaa), Semistocles Kaijage ni pamoja na kuzifanyia marekebisho kanuni zinazosimamia uboreshaji pamoja na kuhakiki vituo vya uandikishaji.

Maandalizi mengine yalikuwa kuwashirikisha wadau wakuu wa uchaguzi yaani vyama vya siasa ambapo pia Tume ilipokea maoni, ushauri na Mapendekezo mbalimbali ambayo iliahidi kuyafanyia kazi ili kufanikisha utekelezaji shirikishi wa zoezi hili lililoanza la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura. Watanzania wengi wanaamini maandalizi yaliyokuwa yakifanywa na Tume yalilenga kuhakikisha zoezi hili linafanyika kwa umakini, linashirikisha wadau wote bila kumwacha mwananchi yeyote mwenye sifa anayestahili kuandikishwa au mwenye haja ya kuboresha taarifa zake.

Aidha, katika kuhakikisha taarifa kuhusu zoezi hili zinamfikia kila raia, Tume ilikutana na viongozi na wawakilishi wa wadau wa uchaguzi kutoka vyama vya siasa, viongozi wa dini, wahariri wa vyombo vya habari, asasi za kiraia na makundi maalumu ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Kimsingi, utaratibu wa uandikishaji wapigakura unatofautiana baina ya nchi na nchi. Katika baadhi ya nchi, mwananchi huingizwa moja kwa moja kwenye Daftari la Wapigakura pale anapotimiza umri wa kupiga kura.

Lakini nchi nyingine ikiwemo Tanzania, uandikishwaji kuwa mpigakura ni suala la hiari. Pamoja na kwamba uandikishaji na upigaji kura kwa Tanzania ni suala la hiari, bado ni muhimu kukumbushana umuhimu wa kila raia aliyetimiza umri wa miaka 18 au zaidi kujitokeza kwa ajili ya ama kuandikishwa kwa yule ambaye hakuwahi kuandikishwa, mwaka 2015 au kurekebisha taarifa zake kwa wale ambao wamehama Jimbo au Kata au wamepoteza au kuharibu kadi zao za kupigia kura.

Uandikishaji wa Wapigakura uliofanywa na Tume mwaka 2015 ulihusisha uandikishaji wa wapigakura wote kutokana na mabadiliko ya teknolojia ya uandikishaji iliyotumika yaani kutoka ile ya Optical Mark Recognition (OMR) na kwenda kwenye ile ya Biometric Voter Registration (BVR).

Ni dhahiri kwamba ile kiu waliyokuwa nayo wananchi ya kuboreshwa kwa Daftari la Kudumu la Wapigakura itakwenda kukatwa kutokana na kuanza kwa uboreshaji huo na hasa kama wananchi watatumia kikamilifu fursa hiyo katika mikoa yao kulingana na ratiba itakavyokuwa. Ikumbukwe kuwa, kazi hii ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura ni maandalizi, lakini pia ni hatua za mwisho hasa kwa wakati huu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano na Madiwani wa Tanzania Bara wa Mwaka 2020.

Mwenyekiti wa Tume Jaji, Semistocles Kaijage na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Dk Athumani Kihamia kwa mara kadhaa wamesikika wakitoa rai kwa wananchi kujitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao pamoja na kutoa ushirikiano kwa watendaji wa Tume wakati wakitekeleza kazi hiyo. Aidha, Tume kupitia kwa watendaji hao imetoa maelekezo kwa watendaji wa uchaguzi vituoni kutoa kipaumbele kwa wazee, wagonjwa, watu wenye ulemavu, wajawazito na wenye watoto wachanga ili waweze kupiga kura bila kulazimika kupanga foleni.

Ni dhahiri kwamba, ile kiu waliyo nayo wananchi ya kuboreshwa kwa Daftari la Kudumu la Wapigakura inakwenda kukatwa kufuatia kuanza kwa kazi hii ya kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura siyo tu kwa matumaini ya kupata kadi ya mpigakura, bali kuwawezesha kushiriki uchaguzi ujao sambamba na uchaguzi mdogo utakaojitokeza.

k‘’KAJIANDIKISHE, KADI YAKO KURA YAKO’’

AWAMU ya Kwanza ya Serikali ya Tanzania iliyoongozwa na Mwalimu ...

foto
Mwandishi: Margareth Chambiri

1 Comments

  • avatar
    Edna mbugani
    08/10/2019

    Naomba kujua Kwa hapa dar es salaam zoezi linaendelea mpaka lini?

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi