loader
Picha

Upinzani makini huangalia maslahi ya taifa, si kupinga tu

NIMEPATA fursa hii kuendeleza zile makala zangu za “Kwa maslahi ya Taifa”, zinazolenga katika kukumbushana na kuelimishina masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kama mchango wangu katika kuisaidia nchi yetu isonge mbele.

Leo imenipendeza kuzungumzia wajibu wa viongozi wa upinzani kwenye masuala yenye maslahi kwa taifa letu pendwa. Ni kweli, kazi mojawapo ya vyama vya upinzani ni kupinga, lakini upinzani makini (responsible opposition) kazi yake sio kupinga tu kila kitu. Kunapotokea jambo kubwa lenye maslahi kwa taifa, Watanzania wote tunapaswa kuungana na kuwa kitu kimoja, wakiwemo wapinzani.

Katika muktadha huo tunapaswa kuwa wakweli, tusipotoshe bali tulisaidie taifa letu kwa michango ya kujenga ili jambo hilo likamilike kama ililivyokusudiwa. Inapotokea serikali iliyoko madarakani inakosea katika jambo muhimu la maslahi kwa taifa, hapo serikali inapaswa ikosolewe kwa njia ya kujenga kwa maana ya kuipa mapendekezo mbadala na sio kwa kubezwa, kutukanwa na kusakamwa.

Rais John Magufuli na serikali yake ya awamu ya tano alipoingia tu madarakani, alitangaza vita nyingi ikiwemo vita ya dhidi ya rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma. Akapambana na vita hiyo kwa njia ya kutumbua tumbua na kuanzisha mahakama ya mafisadi. Tukaanza kuona watu wakiburuzwa mahakamani wakiwemo wale ambao usingewategemea huko miaka nyuma.

Rais alitangaza pia vita dhidi ya ujinga kwa kutoa elimu bure, kuongeza mikopo ya elimu ya juu, kujenga shule zaidi na kuongeza waalimu. Akaanzisha vita dhidi ya maradhi kwa kuongeza bajeti ya afya, kujenga vituo vya afya, zahanati, mahospitali, upatikanaji na usambazaji wa dawa na kuongeza watumishi katika sekta ya afya. Pia alipambana na vita dhidi ya uvivu na uzururaji kwa falsafa yake ya hapa kazi tu ambapo amekuwa akisisitiza kila mtu afanye kazi na uwajibikaji uliotukuka.

Hata tangazo la kupiga marufuku mikutano ya siasa na maandamano, lengo lake ni zuri, kwamba uchaguzi umepita, sasa watu wasikalie tu kupiga siasa na uzururaji wa maandamano, badala yake watu wafanye kazi. Kati ya vita zote ambazo Rais Magufuli na serikali yake ameitangaza, vita ngumu ni vita ya kiuchumi. Hii ndio vita kubwa na ngumu zaidi kuliko vita zote.

Rais Magufuli ameigawanya vita hii katika maeneo tofauti tofauti ikiwemo, kujenga Tanzania ya Viwanda na kujenga miundombinu wezeshi. Ndio maana tunashuhudia ndege za ATCL zikipaa duniani kote, meli zikijengwa, miradi mikubwa ya reli ya kisasa (SGR), mabarabara na madaraja ya juu, umeme wa uhakika kutoka bonde la Stiegler na kadhalika.

Vita hiyo ya uchumi ina kipengele cha kulinda rasilimali za taifa na pengine eneo hilo ndilo gumu zaidi kwa kuwa linajielekeza katika kupambana na ubeberu wa dunia unaojipambanua kupitia mashirika makubwa ya kimataifa. Kimsingi, uwepo na uimara wa ubaberu ni kuhakikisha unaendelea kuzinyonya nchi kama zetu hizi kadri inavyowezekana.

Katika kupigana vita hii kwenye sekta ya madini, Rais John Magufuli alisitisha usafirishaji wa mchanga wa dhahabu (makinikia) wa kampuni ya Acacia ambayo ilikuwa kampuni tanzu ya Barrick ya Canada. Tukatunga sheria mpya ya madini ambayo inaiwezesha Tanzania sasa kumiliki asilimia 16 ya rasilimali zote za ardhini.

Kwa hatua hii, tukapata misukosuko ya kutingishwa na mabeberu au vibaraka wao ili tulegeze msimamo lakini tumeendelea kupambana. Katika kutatua mgogoro wa makinikia, serikali yetu ilifanya mazungumzo na Barrick yaliyodumu kwa zaidi ya miaka miwili ambapo ni wiki iliyopita tu ndipo mgogoro huu umemalizika rasmi kwa Barrick kushika hatamu za Acacia hivyo sasa makubaliano yatasainiwa wakati wowote.

Mazungumzo haya yalikuwa siri na mkataba pia ulikuwa siri lakini kufuatia wenzetu wazungu kuwa wazi zaidi, katika mauziano ya Barrick na Acacia, mkataba huu ukawekwa wazi na kuzua mijadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii ukiwemo mtandao unaoongoza kwa mijadala wa Jamii Forums. Mimi niliandika bandiko kule JamiiForums na kuyasema baadhi ya mazuri ya mkataba huo kuwa ni pamoja na sasa mgogoro wa Acacia na serikali yetu, kumalizika rasmi kwa sababu sasa Acacia haipo tena.

Migodi yote mitatu iliyokuwa chini ya Acacia, sasa itakuwa chini ya Barrick na hivyo yale makubaliano ya serikali yetu sasa yatatekelezwa. Kwa kuanzia tutalipwa dola milioni 300 zilizokuwa ni kishika uchumba, lakini sasa sio kishika uchumba tena bali ni kifuta machozi cha kusamehe lile deni kubwa la kodi la dola bilioni 190. Barrick ataunda kampuni mpya ya ubia na Tanzania kuchukua shughuli za Acacia na kwenye hiyo kampuni mpya, serikali ya Tanzania itakuwa na hisa asilimia 16.

Menejimenti mpya itakuwa na Watanzania na bodi ya kampuni mpya itakuwa na Watanzania pia huku makao makuu yakiwa jijini Mwanza. Tutagawana manufaa ya kiuchumi nusu kwa nusu na kumbuka manufaa ya kiuchumi (economic benefits) ni zaidi ya faida (profit). Watanzania wenye sifa wataajiriwa nafasi za juu, wafanyakazi wa migodi watasomeshwa elimu ya ujuzi kufikia kiwango cha sisi kuwa na wataalamu wa kila kitu kwenye migodi.

Manunuzi makubwa ya bidhaa katika kuendesha migodi hii yatafanyika nchini na siyo nje na hivyo Watanzania kunufaika zaidi na uwepo wa migodi kuliko ilivyokuwa huko nyuma ambapo tunaambiwa hata baadhi ya vyakula vinavyopatikana nchini vilikuwa vinaagizwa kutoka nje. Makinikia yatachenjuliwa hapa nchini pale tutakapoonesha uwezo huku migodi ikitumia zaidi ya dola milioni 70 kila mwaka katika kurudisha faida kwa jamii (CSR).

Huu ndio utakuwa ushindi wa kwanza wa kishindo wa Rais Magufuli katika vita dhidi ya rasilimali za madini na ndio kuanza rasmi kwa utekelezaji wa kwanza wa sheria mpya ya madini. Nichukue fursa hii kumpongeza Rais Magufuli, Profesa Palamagamba Kabudi na pia nitoe hongera kwa Watanzania wote katika ujumla wetu katika kufikia hapa.

Hata hivyo kwenye hili la makinikia, bado kuna mambo hayajakaa vizuri kwa mtazamo wangu ikiwemo kusamehe deni la dola bilioni 190 kwa kulipwa kifuta machozi cha dola milioni 300. Lingine ambalo mimi naona halijakaa sawa labda kama nitapata maelezo ya kutosha ni hili la kuendelea kusafirisha makinikia bila sisi kujua kilichomo. Baadhi ya wanasiasa wa kambi ya upinzani wamekuwa wakiutumia mkataba huo ambao bado haujawa halisi kujipatia umaarufu na kujijenga kisiasa kwa kutumia baadhi ya hoja za kweli wakichanganya na uongo.

Wamefikia hata kupotosha suala zima kwa makusudi kama vile kuwaaminisha watu kuwa huu mkataba tayari umeshasainiwa, kitu ambacho si kweli labda pengine ni kutokana na kushindwa kutafsiri vizuri ‘lugha ya Malikia’. Mmoja wa wanasiasa walioanzisha mjadala huu kule Jamii Forums ni Zitto aliyeibuka na bandiko lenye kichwa cha habari kilichodai: ‘Makubaliano ya Serikali na Barrick Gold changa la macho.’ Zitto alipoona ile Draft Agreement (muswada wa mkataba wa awali wa makubaliano) ikielezwa kuwa imekuwa initialed, akaibuka na upotoshaji kuwa huo mkataba tayari umesainiwa! Kwake neno draft agreement amelitafsiri kuwa ndio mkataba halisi, na neno kuwa initialed kwake ametafsiri kuwa huku ndiko kusainiwa kwenyewe! Hizi lugha za watu jamani, zisitufanye kuonekana waongo na wapotoshaji, tuwe makini.

Zitto akaandika: “Kiambatanisho namba nne kimeweka muhtasari wa kinachoitwa ‘Material Terms’ katika Makubaliano ya awali kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick Gold ambayo yamesainiwa (Initialed) mwezi Mei mwaka huu.

Kimsingi Barrick imelazimishwa na kanuni za masoko ya mitaji kuweka wazi makubaliano hayo. Ni masikitiko makubwa kuwa Serikali yetu haijathubutu hata kuliambia Bunge kuwa kuna makubaliano ya namna hiyo wakati wa Bunge la Bajeti, imesaini kwa siri kama ulivyosainiwa mkataba wa Buzwagi. Ikumbukwe kuwa makubaliano hayo yamesainiwa wakati Bunge likiwa linaendelea na mkutano wake jijini Dodoma. Sisi kama wawakilishi wa wananchi imebidi kusubiri masoko ya mitaji ya ‘mabeberu’ wa London yaweke wazi masuala yanayohusu nchi yetu.” Mwisho wa kumnukuu.

Nami nilimjibu hivi: “Mkuu, Mhe. Zitto, kwanza asante kwa bandiko hili na uzalendo wako kwa nchi yako. Kwa heshima na taadhima, naomba nitofautiane na wewe kwa kukuomba uwe mkweli na usifanye upotoshaji, just tell the truth and the truth will set you free. Siyo kweli kuwa mkataba huu umeisha sainiwa! Hilo neno ‘Initialed’ sio kuonyesha kuwa umesainiwa, bali katika mikataba, kunatakiwa signatories watie initials zao kwenye kila ukurasa waa draft kuonesha wameelewa, lakini draft ni draft (muswada) na mkataba ni mkataba! Ku-initial sio kusaini.”

Nihitimishe kwa kusema kwamba kazi rasmi ya upinzani ni kupinga kwa kuonesha makosa na kwa hoja mbadala za ukweli na sio kwa hoja za uongo na upotoshaji. Lakini kwenye jambo lenye maslahi kwa taifa kama hili la rasilimali madini, wapinzani, CCM, Serikali na Watanzania wote tusimame pamoja, tuongee lugha moja na kwa sauti moja.

Nitoe wito kwa wapinzani kwamba tujenge upinzani makini, sio upinzani wa kupinga tu kila kitu hata mambo muhimu na yenye maslahi ya Taifa ambayo tunatakiwa kuwa kitu kimoja kwa kuyaunga mkono. Pia nitoe mwito wangu kwa Serikali yangu tukufu kwa kukubali kusikiliza hoja mbadala hata kama zinatoka kwa wapinzani tukiwemo sisi tuso na vyama alimradi ziwe na maslahi kwa taifa na kuzifanyia kazi.

BAADA ya kupiga kambi kwa siku tofauti 15 katika vituo ...

foto
Mwandishi: Pascal Mayalla

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi