loader
Picha

Bonde la Olduvai na maajabu ya binadamu wa kwanza duniani

JUMATATU ya wiki hii, wakazi wa Olduvai Gorge wameungana na wanasayansi watafi ti wa kihistoria na watalii kuadhimisha miaka 60 tangu kuvumbuliwa kwa fuvu la binadamu wa kale, maarufu Zinjanthropus.

Maadhimisho hayo yamefanyika katika eneo la Olduvai ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Mashariki mwa Mbuga za Taifa za Serengeti nje kidogo ya mji wa Arusha, ambako inaaminika aliishi mtu wa kwanza duniani.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyeiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kusimamia uboreshaji wa eneo la mnara wa Zinjanthropus ili pavutie zaidi.

Mnara wa Zinjanthropus na Homo habilis umejengwa kwenye Hifadhi ya Ngorongoro karibu na njia panda ya kuelekea Bonde la Olduvai. Fuvu la binadamu wa kale lilivumbuliwa kwenye bonde hili pamoja na visukuku vingi vya wanyama wa kale na masalia mengi ya zana za mawe na watafiti Mary Leakey na mumewe, Luis Leakey baada ya kuchimba mabaki katika eneo hilo la Bonde la Olduvai.

Ugunduzi huo uliofanyika Julai 22, 1959 ulikuwa wa vipande zaidi ya 100 ukasaidia katika kutambua asili ya watu wa awali duniani. Kabla ya ugunduzi huo, wanasayansi na wanahistoria walikuwa wakiamini kuwa, binadamu wa kale walitokea China baada ya ugunduzi wa mafuvu ya kale baina ya 1923 na 1927 nchini humo ya Homo eractus, maarufu kama Peking Man.

Mafuvu hayo ya China yalikuwa na umri wa takribani miaka 750,000. Mafuvu ya Olduvai eneo ambalo kwa sasa lipo Tanzania wakati wa ugunduzi wake, lilikuwa na umri wa takribani miaka milioni 1.75, na hakuna mabaki ya mtu wa kale zaidi ambayo mpaka sasa yamegunduliwa sehemu nyengine yoyote duniani. Tangu utafiti wa mambo ya kale uanze kwenye bonde hili mnamo karne iliyopita, ilithibitika kwamba teknolojia ya mwanzo kabisa duniani ilianzia hapa kutokana na ushahidi wa zana za mawe za muhula wa kwanza.

Ushahidi wa akiolojia na visukuku unaonesha mabadiliko ya viumbe asilia na maendeleo ya utamaduni wa binadamu wa kale katika nyakati tofauti. Lengo la utafiti mkubwa unaoendelea kwenye Bonde la Oldupai ni kuchunguza mabadiliko ya zamadamu na maendeleo ya teknolojia ya zana za mawe kati ya muhula wa mwanzo (Oldowan) na wa pili (Acheulian).

Utafiti huu unafanywa na kikundi cha wanasayansi wa kimataifa kutoka vyuo vikuu mbalimbali duniani. Kikundi hiki kijulikanacho kama Olduvai Geochronology and Archaeology Project (OGAP), kinajumuisha wanasayansi kutoka fani mbalimbali za jiolojia, akiolojia, paleontolojia na mazingira.

Tanzania imebarikiwa sana na uwepo wa vivutio vingi vya kila aina, hata hivyo, licha ya kuwepo maeneo mengi yenye vivutio, Ngorongoro ndiyo huwavutia zaidi watu na kuwafanya kufunga safari kuja Tanzania. Hili ni eneo lenye urefu wa kilometa 20, kina cha mita 600 na ukubwa wa kilometa za mraba 300 na hutembelewa na watu wengi mashuhuri, akiwemo Waziri Mkuu wa zamani wa Israel, Ehud Barak aliyetembelea bonde hili mwaka 2017 sambamba na Mbuga ya Serengeti.

Ngorongoro ni eneo lililo katika orodha ya vivutio vya utalii likiwa na maajabu yaliyolifanya Shirika la Kimataifa linaloshughulikia Elimu, Utamaduni na Sayansi (UNESCO) kulijumlisha kwenye orodha yake ya urithi wa dunia.

Hakika, Bonde la Ngorongoro ni Eden ya sasa (lenye viashiria vyote vya bustani ya Eden kwenye Maandiko Matakatifu) kama watu wengi wanavyopenda kuliita kutokana na maajabu yaliyopo pamoja na historia ya binadamu wa mwanzo kuishi pale. Hili ni eneo ambako wanyamapori na binadamu (Wamaasai) wanaishi pamoja kwa amani bila shida yoyote kwa zaidi ya miaka 200.

Unaweza kukuta kuna wakati ng’ombe wa Wamasai wanachunga pamoja na pundamilia katika Mbuga za Ngorongoro. Kwa jumla Wamasai huishi pamoja na mifugo yao kwa amani na utulivu kabisa bila ya kuwabugudhi wanyamapori (ni kama ilivyokuwa Eden aliyoishi Adam na wanyama bila bughudha).

Hata hivyo, Maandiko Matakatifu yanabainisha kuwa, Eden ilikuwepo eneo ambalo kwa sasa ni nchi ya Iraki, hivyo wengine wanaweza wasipendezwe na eneo la “Laetoli” lililo ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, linaloaminika kuwa binadamu wa kwanza alitembea duniani. Ni eneo lililoitwa kwa Kiingereza ‘Cradle of Mankind’, au kitovu cha binadamu.

Suala la Laetoli linasemekana lilianza kujitokeza wakati binadamu walipoanza kutembea wima, au kwa miguu yao miwili, alama ambazo sasa haziwezi kufutika ardhini katika eneo hili la Ngorongoro, kutokana na milipuko ya volcano au matukio mengine ya aina hiyo ya asili. Hili ni eneo tepetepe lenye mkusanyiko wa alama za wanyama, lipo kilometa 40 kutoka eneo la Olduvai Gorge kunakovuma upepo na ambako inaaminika binadamu wa kwanza aliishi.

Alama hizo za kale za miguu zilizovumbuliwa na Dk Mary Leaky zimehifadhiwa katika majivu ya volkano, wanasayansi wakiamini kwamba majivu hayo yanatokana na mlipuko wa volkano ya sadiman yenye urefu wa kilomita 20. Kwa mujibu wa watafiti, mburuzo huo ni ushahidi usio kifani wa binadamu wa kale kutembea kwa miguu miwili zaidi ya miaka milioni 3.6 iliyopita.

Ngorongoro pia ni hifadhi ambako hupatikana aina mbalimbali za wanyama na itaendelea kushika nafasi yake kama eneo ambalo wanyama wote waliopakiwa katika Safina ya Nuhu, waliteremka baada ya mafuriko, yanayoelezwa katika Biblia. Zipo hadithi kuwa Safina ya Nuhu ilipita eneo hili wakati mvua kubwa ya siku 40i iliponyesha na kusababisha gharika lililoacha athari katika eneo hili, na ishara ya gharika hilo inaonekana katika eneo la Olduvai Gorge.

Kwa mujibu wa wanasayansi ambao wamekuwa wakifanya utafiti kwa takribani miaka sita, mabaki ya Safina ya Nuhu yamepatikana katika mpaka wa Uturuki na Iran kilometa 32 kutoka Mlima Ararat. Kwa mpango huo, eneo la Laetoli linaweza kuwa miongoni mwa maeneo muhimu duniani yenye historia ya kale inayomhusu binadamu.

Mbali na vivutio vilivyotajwa, vingine unavyoweza kuviona ndani ya eneo la Ngorongoro ni Ziwa Ndutu na Masek; maziwa haya muhimu kwa hifadhi hii hayana kina kirefu lakini maji yake yana chumvi hivyo hayafai kwa matumizi ya binadamu.

Kwa ziwa kama Ndutu ambalo hutumiwa zaidi na wanyama kama sehemu ya kunywa maji na kupumzika baada ya wanyama kuhama, na pia ni sehemu nzuri zenye wanyama kama kiboko na mamba, hivyo wageni hutumia nafasi hii kama sehmu ya kuwaona wanyama. Upo pia Mlima Oldonyo Lengai ambao unapatikana nje kidogo ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Ni mlima pekee wenye volkeno hai inaYOonesha kuwa ililipuka kwa mara ya kwanza mwaka 1883, na kwa mara ya mwisho, mlipuko ulitokea kati ya Februari na Machi 2008. Pia, ndani ya Ngorongoro utashuhudia mchanga unaohama, unaosifika kwa kuwa na umbo kama la mwezi.

Inasemekana kuwa, mchanga huo ulitokana na majivu ya Mlima wa Oldonyo Lengai, na umekuwa ukisukumwa taratibu kuelekea upande wa Magharibi wa hifadhi kwa kiwango cha mita 17 hadi 20 kwa mwaka. Mchanga huu una kimo cha mita 9 na mzingo wenye urefu wa mita 100, na unapatikana Kaskazini mwa Bonde la Olduvai.

Ndani ya Ngorongoro kuna Bonde la Olkarien; eneo hili nalo ni muhimu katika hifadhi kwani hutoa hifadhi kwa ndege tai aina ya Ruppell Griffon. Msimu mzuri wa kutembelea eneo hili ni miezi ya Machi mpaka Aprili ambapo tai huzaliana.

Wanyama huja eneo hili pale panapokuwa na malisho ya kutosha. Hata hivyo hutaifaidi Ngorongoro kama hautavizungukia vivutio mbalimbali kama vile Bonde la Olmoti kuelekea nyanda za Embakai, shuka chini kuelekea Bonde la Ufa, pandisha Kaskazini kwenye nyanda za hifadhi ya misitu na kisha eneo la tambarare la Mashariki kuzunguka Miamba ya Nassera, Milima ya Goli na Bonde la Olkarien. Kama alivyosema Waziri Mkuu, tunapaswa kulitunza eneo hili kwani lina historia kubwa s na ni kitovu cha binadamu.

JUHUDI za serikali kupambana na ugonjwa wa homa ya mapafu ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi