loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Sifa za mwalimu bora wa Lugha ya Kiswahili

KABLA makala haya hayajaanza kuchambua sifa za mwalimu bora wa Lugha ya Kiswahili, kwanza tujikumbushe kuhusu lugha. Lugha ni mfumo wa sauti za nasibu ambazo hutumiwa na jamaii kwa ajili ya mawasiliano.

Lugha hutawala maisha ya wanadamu. Lugha hutumika kueleza fikra za watu, kuendeleza uhusiano wa watu na hata kuhifadhi na kupitisha utamaduni wa watu. Bila lugha, historia ya mwanadamu haingekuwa jinsi ilivyo.

Lugha hutumika tu na binadamu. Kati ya viumbe wote duniani, binadamu ndiye aliyejaliwa kipawa cha kujifunza lugha. Lugha ya mwanadamu inatofautiana sana na mawasiliano ya wanyama na viumbe wengine kama vile ndege, samaki, wadudu n.k. Lugha ya wanadamu ni bunifu na hivyo humwezesha binadamu kuelezea hali mbalimbali.

Aidha, anaweza kutumia lugha kuzungumzia mambo yaliyopo, yajayo na yaliyopita na hata mambo ya kidhahania. Hivyo basi, ili lugha iendelee kukua kwa vizazi na vizazi, lazima kuwe na vitu au watu wa kusimamia na kutoa miongozo ya namna bora ya kuitumia lugha hiyo.

Hawa ni walimu wa lugha. Watu wanadhani mwalimu wa lugha ni yule tu anayefundisha darasani, si kweli, walimu wa lugha wako wengi mfano: wazazi/mzazi mama, mwalimu darasani, vyombo vya habari kama magazeti, wazungumzaji wa Kiswahili, vitabu, mitandao, wataalamu, na wadau wa lugha.

Mwalimu wa Lugha ya Kiswahili ni mtu anayesaidia wengine kupata ujuzi, maarifa na tunu. Kazi hiyo, inaweza kufanywa na yeyote katika nafasi maalumu. Kwa mfano, mzazi au ndugu akimfundisha mtoto nyumbani, lakini kwa wengine ndiyo njia ya kupata riziki inayomdai karibu kila siku, kwa miaka mingi, kuifanya: kwa mfano shuleni. Huko mwalimu anatakiwa kuwa na astashahada, stashahada au shahada, kadiri ya sheria za nchi na ya ngazi ya elimu inayotolewa.

Kazi ya mwalimu wa Lugha ya Kiswahili inafanana na ya dereva wa gari ambayo ni kuongoza chombo hadi kifike mwisho wa safari salama. Hivyo, mwalimu wa Kiswahili kama alivyo dereva wa gari, anapaswa kuwaongoza wanafunzi kwa uangalifu, nidhamu na utaalamu wa hali ya juu. Katika makala haya, tutamuangazia mwalimu wa darasani wa Lugha ya Kiswahili. Hebu tujikumbushe baadhi ya sifa za mwalimu bora wa Lugha ya Kiswahili. Kwanza kabisa, mwalimu anatakiwa kuijua vyema Lugha ya Kiswahili.

Katika hali ya kawaida, kama mtu hajui jambo fulani, hawezi kulielezea sawasawa. Mwalimu anapaswa kuwa na ufahamu unaozidi wanafunzi wake. Ikitokea katika darasa mwanafunzi anajua zaidi ya mwalimu wake, mwalimu anapaswa kwenda mbali zaidi ili asije kudharauliwa naye. Sarufi ya lugha ya Kiswahili lazima aifahamu, ili aweze kufundisha kwa usahihi bila kupotosha.

Pia, ikiwa ana matatizo ya matamshi ya baadhi ya sauti za lugha ya Kiswahili kama vile ‘r’ badala ya ‘l’; ‘th’ badala ya ‘s’; ‘dh’ badala ‘z’ nk. anapaswa kujirekebisha kwani athari yake ni kubwa kwa anaowafundisha. Ni wazi kuwa, wazungumzaji wa Kiswahili siyo wazawa asilia wa jamii ya Waswahili, kwa hali hii mwalimu anaweza kujikuta ameathiriwa na lugha mama. Mwalimu imara anapaswa kujiendeleza kitaaluma na kukubali kujifunza kila siku mabadiliko ya Lugha ya Kiswahili ili kujua na kufanya somo lake lieleweke vizuri.

Pili, mwalimu anapaswa kuwa mnyumbufu na mbunifu katika uwasilishaji wa Somo la Kiswahili. Lugha ya Kiswahili ni tamu sana na rahisi kujifunza. Watu wengi hasa wageni wanatamani kujifunza kwa sababu ya urahisi wake, lakini cha kustaajabisha, baadhi ya wanafunzi wa Kitanzania wanasema Somo la Kiswahili ni gumu sana. Katika hali ya kawaida, haikutarajiwa kwa Mtanzania yeyote kuona ugumu wa lugha hii ambayo wengine wanaiona ni lulu kuijua.

Mtazamo huu hasi unapaswa kuondolewa na mwalimu kulingana na ubunifu na unyumbufu wake katika kuliwasilisha somo hili. Ubuninifu wa mwalimu unaweza kuwa katika maandalizi ya somo na nyenzo za kufundishia. Maandalizi ya somo yanapaswa kufanyika kwa muda mrefu kwa kuzingatia mtaala na kudurufu maandiko mbalimbali yanayoendana na somo. Aidha, matumizi ya nyenzo halisi katika uwasilishaji wa somo.

Ili wanafunzi waweze kuwa na uelewa kabambe, kila somo linahitajika kuwa na vifaa vyake. Mfano, mwalimu anafundisha fasihi simulizi inayohusiana na ngoma ya Wagogo, vifaa halisi vitakuwa vyombo kama njunga, ngoma, mashuka meusi n.k. Kama vifaa halisi havitapatikana, basi michoro yake inaweza kutumika. Inashauriwa kuwa matumizi ya vitu halisi ni bora zaidi kwa ufundishia kuliko kifaa cha aina nyingine ile.

Kwa kutumia vitu halisi, mwanafunzi anajifunza kwa udadisi, kuchunguza, na kugundua. Pia, vitu halisi vinampa mwanafunzi nafasi kubwa ya kujifunza kwa vitendo na kutumia milango mingi ya fahamu kwawakati mmoja.

Tatu, mwalimu wa Kiswahili anapaswa kuwa mcheshi, mchangamfu na bidii katika kuwasilisha somo lake. Taaluma ya ualimu ni tofauti na taaluma nyingine, hususani uaskari. Mwalimuatakayeingia darasani akiwa amevaa sura ya askari, huwa anatishia na kuwaogofya wanafunzi kiasi kwamba, usikilizaji na uelewa hufifishwa na hali ya mwalimu wao.

Hivyo ni vyema mwalimu anapoingia darasani, anashauriwa kuwa mchangamfu na mcheshi ili kuwafanya wanafunzi wake kuchangamka na kupokea anayofundisha bila kuogopa. Sauti yake iwe ya wastani yenye mvuto kwa wanafunzi kumakinika na kusikiliza. Halikadhalika, bidii ya mwalimu katika kuhudhuria vipindi vyake, kutoa mazoezi ya kutosha, kutoa mrejesho na masahihisho bila shaka wanafunzi wataiga na kumakinika na yale wanayofundishwa na mwalimu wao.

Itoshe tu kusema kwamba, wataalamu wa sayansi ya elimu wanazidi kukubaliana kwamba, mwalimu yeyote anahitaji mambo matatu: ujuzi (kufahamu mada na namna ya kuifundisha, mtaala, sayansi ya elimu, saikolojia, tathmini n.k.) vipaji (kupanga kipindi, kutumia vifaa, kuongoza wanafunzi, kuendesha makundi, kutathmini maendeleo) na misimamo (tunu, tabia, imani na uwajibikaji). Hivyo mwalimu wa Kiswahili ana nafasi kubwa sana kuwafanya wanafunzi wa Kitanzania hata wa kigeni kulipenda Somo la Kiswahili ambalo ni lulu ya dunia kwa sasa.

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England 2020/2021 umeanza na ...

foto
Mwandishi: Arnold Mayange Msofe

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi