loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mila za Kisukuma zinavyohimiza watoto pacha kufanyiwa tambiko

WASUKUMA linatajwa kuwa kabila kubwa pengine kuliko yote Tanzania likipatikana katika mikoa minne ya Tanzania. Mikoa hiyo ni Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Geita, ingawa kuna Wasukuma wengi pia katika baadhi ya wilaya za mkoa wa Mara na Tabora.

Licha ya mwingiliano wa makabila na athari za utandawazi, bado baadhi ya Wasukuma wanaendelea kuenzi mila na desturi zilizokuwepo tangu enzi na enzi kwa kuzidumisha.

Moja ya desturi hizo ni namna wanavyohudumia watoto pacha walioaminika kuandamwa na mikosi. Sonda Kabeshi, mzaliwa wa mkoa wa Shinyanga ambaye kwa sasa anaishi katika kata ya Ndembezi katika Manispaa ya Shinyanga anajitambulisha kama mhifadhi wa mila na desturi za kabila la Wasukuma.

Kuhusu namna watoto pacha wanavyopaswa kuhudumiwa kwa mila za Kisukuma, Kabeshi anasema mama anapozaa watoto pacha, kwa mujibu wa mila na desturi zao hawapaswi kunyolewa nywele mara moja isipokuwa kwa masharti.

Anasema kama familia ina tabia ya kupikia ndani basi majivu yanatakiwa yasiondolewe na kwamba hata wanapofagia uchafu wasitupe nje bali wauweke pembeni mwa mlango.

“Ndani ya nyumba kukiwa na watoto pacha hawapaswi kunyolewa nywele na hadi wanapofikisha umri wa mwaka mmoja au zaidi. Halikadhalika uchafu hautolewi ndani mpaka aje nyakanga kuwafanyia sherehe,” anasema.

Anasema ili kuwaweka sawa watoto pacha waendelee kuishi kama watu wengine wasio pacha, wataletwa wazazi wengine waliozaa pacha wanaotambulika kwa Kisukuma kama ‘Bagangi’ na kuwabeba wakati wa hafla hiyo maalumu ya kutoa pacha nje.

“Siku ya sherehe inategemea familia iliyopata pacha ina uwezo gani wa kufanya maandalizi ya kuwatoa nje kwa huchinja ng’ombe ili watu wale na hapo ndipo nywele zao hunyolewa rasmi, nyumba kufagiliwa uchafu kutolewa nje,” anasema Kabeshi.

Kabeshi anasisitiza kwamba kwa mila na desturi za Wasukuma watoto wakinyolewa nywele na nyumba ikifagiliwa kabla ya kufanyiwa sherehe za kimila za kuwatoa nje rasmi ni kuvunja miiko na kwamba pacha hao wanaweza wasiishi maisha ya kawaida kama wenzao waliozaliwa bila kuwa na pacha wao.

Anasema malezi na makuzi ya watoto pacha yanatakiwa muda mwingi wawe wakivaa nguo sare na asiyefanya hivyo anapingana pia na mila na kwamba kwa imani za Wasukuma, hali hiyo itawafanya mapacha kutengana haraka na kwamba mmoja akichukia anaweza kuugua au hata kufariki kabisa.

“Hii ya kuwavalisha sare ni kuonesha kwamba wapo mwili mmoja. Ukiwatofautisha utakuwa umevunja miiko, na pia wakililia chakula fulani lazima uwape au ng’ombe achinjwe kwa ajili yao. Usipofanya hivyo, kama una ng’ombe utashitukia hata zizi zima ng’ombe wamekufa. Ndio maana huko nyuma mapacha kwa Wasukuma waliitwa watoto wenye mikosi,” anasema Kabeshi.

Anasema uwepo wa wazazi waliokwisha zaa pacha, yaani ‘abagangi’ hulazimika kwenda kwenye familia yenye watoto pacha ili kuwaondolea mikosi na kwamba mpaka leo bado baadhi ya watu wanafanya matambiko hayo. Kabeshi anasema sababu ya kufanya matambiko ilitokana na imani kwamba watoto hao huweza kuwa chanzo cha kuleta balaa au mikosi katika jamii kama vile mvua kutonyesha au kunyesha mvua ya mawe na upepo ikiambatana na radi na balaa la njaa kwenye kijiji husika.

Anasema enzi hizo, familia ikishindwa kuwafanyia matambiko watoto wao pacha inaweza kutengwa na jamii kwa sababu itaonekana imefuga watoto wenye kuleta mikosi ndani ya kijiji. Aidha Kabeshi anasema mtoto mmoja akitokea kafariki dunia basi wazazi watalazimika kutengeneza kibuyu ambacho kitakuwa mbadala wa yule aliyefariki dunia na kukiweka nje ya nyumba na kwamba akitokea mtu akaja kusalimia ataanzia nje kwenye kibuyu kutupia kiasi chochote cha fedha alichonacho na kwamba hiyo inakuwa ni ishara ya salamu. Akielezea sababu za kufanya matambiko hayo, Kabeshi anasema zipo simulizi zinazoonesha kwamba alipokuwa akifariki mtoto pacha, baada ya siku kadhaa za maziko yake mvua kubwa iliyoambatana na radi ilikuwa ikinyesha na kaburi kufukuliwa na radi na kwamba ndio ikawa chanzo cha kufanya matambiko. Kabeshi anasema mtoto anayezaliwa kwa kutanguliza makalio huitwa Kashindye na kwamba na yeye hufanyiwa tambiko na ikitokea akafariki dunia wanaoshughulikia mazishi yake ni wale walioandaliwa maalumu. Mkazi wa kijiji cha Idukilo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, Damian Mussa anasema watoto pacha na Kashindye hawawezi kunyolewa nywele tangu kuzaliwa kwao mpaka waonane na nyakanga wa ‘ukango’ ambaye pia huwa na kibarua cha kuwafunda wazazi husika wasije wakaharibu mila. Anasema kama nyakanga hajatokea ili kuwatoa nje, watoto hao hubaki ndani hata kwa miaka mitano na kwamba wakitolewa nje ndipo hunyolewa ili kuwaondolea mikosi na kupewa majina na nyakanga hao. Jesca Sunubi, mkazi wa kata ya Ndala katika Manispaa ya Shinyanga ambaye amezaa watoto pacha anasema alipozaa wanawe hao baadhi ya majirani zake walikuwa wakimweleza awafanyie matambiko kwani watamhangaisha katika kuwalea na kwamba endapo ataugua mmoja kama hawatofanyiwa matambiko basi ajue mwingine pia atafuatia. Sunubu anasema kutokana na maoni hayo ya ‘wakubwa’ alilazimika kufuata mila na desturi za kuhakisha wananyolewa na nyakanga katika hafla maalumu na pia kuwavalisha sare. Anasema hata mvua ilipokuwa ikinyesha majirani walikuwa wakimwambia aweke jembe nyuma ya mlango kuzuia radi isiwapige. “Lakini baadaye nilishauriwa na baba yangu mzazi kwenda kanisani na kuachana na mila hizi kwa sababu ni gharama pia kama vile kuchinja ng’ombe na kadhalika. Nimeanza kufuata ushauri wa baba,” anasema Sunubu.

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England 2020/2021 umeanza na ...

foto
Mwandishi: Kareny Masasy

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi