loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Madiwani na umuhimu wa usimamizi shirikishi wa misitu

WAHENGA husema asifi ye mvua imemnyea na pia wanasema adhabu ya kaburi aijuaye maiti. Methali hizo zinasadifu kile ambacho madiwani wa Halmashauri za wilaya za Morogoro, Mvomero na Kilosa mkoani Morogoro walichosisitiza hivi karibuni baada ya kuambiwa kwamba ufadhili wa mradi Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa (TTCS) unakoma rasmi mwezi Novemba katika maeneo yao.

Madiwani hao wanakumbuka namna misitu ya asili katika maeneo yao ilivyokuwa inateketea kutokana na kugeuzwa mashamba sambamba na ukataji holela wa mkaa hasa kwa kuzingatia kwamba mkoa huo uko jirani na Dar es Salaam, jiji ambalo inaaminika hutumia zaidi ya nusu ya mkaa wote unaozalishwa nchini! Lakini mradi wa TTCS maarufu kama ‘Mkaa Endelevu’ umeonesha uwezo mkubwa wa kuokoa misitu ya vijiji vyao, mbali na kuviingizia mapato huku halmashauri zao pia zikinufaika na mapato yatokanayo na rasilimali hizo za misitu.

Katika warsha zilizofanyika Kilosa na Morogoro wiki iliyopita, madiwani walikiri kwamba Usimamizi Shirikishi wa Misitu (USM) unaosisitizwa na mradi wa TTCS ndio suluhisho katika ulinzi wa misitu inayozunguka vijiji. Kwamba wananchi wasipoona faida ya misitu yao, siyo tu kwamba hawashiriki katika kuilinda bali pia huhusika katika kuivuna kwa njia holela.

Madhumuni ya warsha hizo kwa madiwani wa kila halmashauri hizo tatu, yalikuwa ni kutoa mrejesho wa shughuli za mradi wa TTCS toka umeanza, takribani miaka saba iliyopita kwa upande wa Kilosa na miaka miwili na nusu kwa Halmashauri za Morogoro na Mvomero. Madiwani pia walijadili namana ya kupata ufumbuzi wa kuendeleza fursa zinazoletwa na mradi huo na hivyo kutatua changamoto na hatari zinazoweza kujitokeza katika kuendeleza Usimamizi Shirikishi wa Misitu (USN) ndani ya wilaya zao baada ya ufadhili wa sasa kukoma.

Mradi wa TTCS unafadhili na Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswisi na kuendeshwa katika vijiji 20 wilayani Kilosa, vijiji 11 katika wilaya ya Mvomero na vijiji vitano katika wilaya ya Morogoro. Wanaosimamia mradi huo ni Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) kwa kushirikiana na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (Mjumita) pamoja na Shirika la Kuendeleza Nishati Asilia (TaTEDO).

NINI KIMEFANYWA NA TTCS?

Meneja wa mradi huo kutoka TFCG, Charles Leonard, aliwaambia madiwani kwamba mradi wa TTCS umesaidia sana kulinda misitu ya vijiji vinavyoutekeleza kulinganisha na vile ambavyo havina mradi huo. Akizungumza kwa kuonesha takwimu alisema hali hiyo imetokana na wanakijiji kuona faida ya raslimali zao na hivyo kugeuka kuwa walinzi namba moja wa misitu yao.

Alisema kupitia mradi huo wananchi pia hujifunza namna ya kuendesha kilimo hifadhi ambacho kinatumia eneo dogo kwa kuzalisha mazao mengi na hivyo kuondokana na kilimo cha kuhamahama kinachochangia sana kumaliza misitu. Alisema mapato ambayo vijiji vimekuwa vikipata kupitia uvunaji mkaa kwa njia endelevu yametumika kwa kujenga madarasa, kununua madawati, kugharimia bima za afya kwa wanakijiji, kuchimba visima na kadhalika. “Kiasi kingine cha fedha kinatumika katika ulinzi na uendelezaji wa misitu,” alisema.

MFUMO WA MRADI

Leonard alisema mradi huo unaanza kwa kuviwezesha vijijini kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi katika kijiji na hivyo eneo la msitu pia kujulikana na kutengwa. Hatua nyingine alisema ni vijiji kutenga eneo la msitu la asilimia 10 pekee kwa ajili ya kuzalisha mkaa kwa njia endelevu na kwa miaka yote. Katika eneo hilo la asilimua 10. Kijiji hutakuwa kutenga vitalu vya mita 50 kwa 50 ili kuwezesha kuzalisha mkaa ambapo kitalu kimoja kikivunwa, kingine kinarukwa na kwamba siyo kila mti unavunwa. Hatua nyingine alisema ni kuandaa matanuri yaliyoboreshwa yanayotoa mkaa bora pia. Alisema kupitia njia hiyo, eneo lililovunwa uoto wake wa asili hurudi kwa njia ya visiki vilivyoachwa kuchipua.

Kuhusu mapato, Leonard alisema, katika vijiji vinne tu vinavyotekeleza mradi huo katika halmashauri ya Morogoro, kwa mfano, jumla ya Sh milioni 419 zimekusanywa katika kipindi cha miaka miwili na nusu kuanzia mwaka 2017. Akasema, halmashauri ya wilaya hiyo pia iliweza kujipatia jumla ya Sh milioni 101 kutoka kwenye vijiji hivyo vya mradi kama sehemu ya makusanyo ya mapato.

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, mradi huo alisema umeviwezesha vijiji 20 kuingiza zaidi ya shilingi bilioni moja huku halmashauri hiyo pia ikikusanya zaidi ya Sh milioni 260 kuanzia Mei mwaka 2013 hadi Mei mwaka huu.

MAAZIMIO YA MADIWANI

Ingawa kila halmashauri ilifanya warsha kivyake, lakini maazimio ya madiwani, hususani yake muhimu yalielekea kufanana. Wote walikubaliana umuhimu wa vijiji vyote kupima, kutambua na kuanisha maeneo yao ya misitu ili vifanyiwe mpango wa usimamizi bora. Walikubaliana pia kuwa halmashauri zao zihakikishe zinatenga fedha na kuzitoa kwa ajili ya kuendeleza USM katika vijiji vya mradi. Wakaona kwamba ni muhimu sehemu ya asilimia inanayokusanywa kutoka vijiji vya mradi itolewe kwa ajili ya kutumika kuanzisha miradi kama hiyo ya USM katika vijiji vingine kila mwaka.

Kuna halmashauri zilizopendekeza vijiji viwili na zingine vijiji vitano. Katika halmashauri ya Kilosa, madiwani walichachamaa baada ya kuona uongozi wa halmashauri yao unasuasua kutenga fedha kwa ajili hiyo licha ya agizo ambalo liliwahi kutolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Adam Mgoyi mwezi Machi mwaka jana.

Akizungumza baada ya kutembelea mradi wa TTCS katika kijiji cha Kitunduweta, Tarafa ya Uyala, Kilosa, Mgoyi alisema anataka kuona mradi kama huo ukifanywa na halmashauri ya Kilosa katika mwaka wa fedha 2018/19. Aliiagiza halmashauri hiyo ijielekeze katika maeneo ambayo ni hatari katika kuharibu misitu hususani maeneo ya kaskazini mwa wilaya ya Kilosa, kuanzia eneo la Mbaku hadi kijiji cha Kwambe. “Mwaka ujao, halmashauri itatakiwa kuwa na kijiji ambacho na wao watakifanya kama kijiji cha mfano wakishirikiana na wanaoendesha mradi huu,” alisema.

Alihimiza madiwani na halmashauri kwa ujumla kufanyia tathmini miradi inayoletwa na wahisani katika wilaya hiyo na kuianzisha mahala pengine pale inapoonekana ina manufaa na hivyo akaagiza kutengwa kwa fedha ili halmashauri ianze kutekeleza mradi wa mkaa endelevu. Madiwani katika halmashauri zote tatu, kwa nyakati tofauti waliazimia pia kwamba taarifa kuhusu kuendeleza USM zifike kwenye vikao vya robo mwaka vya halmashauri zao, hususani taarifa zinazohusu uendelevu wa matumizi ya maliasili kwenye vijiji vya mradi na vijiji vingine.

Kwa vile ilipendekezwa kwamba baada ya ufadhili kukoma vijiji vyenye miradi vichangia asilimia saba ya mapato kwa ajili ya kulipia huduma ya ushauri wa kitaalamu kutoka Mjumita ili mradi ubaki kuwa endelevu, walikubaliana kukaa pamoja ili kupitia rasimu ya mkataba huo wa ushirikiano. Hilo wakasema liende sambamba na kupita kwenye vijiji husika ili kupate maoni yao na taarifa husika ziwasilishwe katika vikao vya robo mwaka ya halmashauri.

Kimsingi, madiwani walidhihirisha kwamba wameona manufaa makubwa ya USM na kushauri serikali kuona umuhimu wa kuhamishia dhana nzima ya USM kupitia mradi wa mkaa endelevu katika halmashauri zingine zenye misitu. Ama kwa hakika asifuye mvua imemnyea

KATIKA makala mbili zilizopita tumeangalia manufaa ambayo wanavijiji wamepata kutokana ...

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi