loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wiki ya Kagera kuibua fursa biashara, uwekezaji

KATIKA kuunga mkono jitihada za Rais John Magufuli za kuijenga Tanzania ya viwanda mkoa wa Kagera umeandaa Wiki ya Kagera, yenye lengo la kuibua fursa za kibiashara na uwekezaji mkoani humo.

Katika wiki hiyo ambayo kilele chake kinatarajiwa kufanyika Agosti 14, mwaka huu na kufunguliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, mkoa huo umejipanga kutumia fursa iliyonayo ya kijiografia ya kuwa mkoa uliopakana na nchi takribani sita, kuufanya kuwa kitovu cha uchumi na uwekezaji.

Wiki hiyo inatarajiwa kukutanisha wadau wa biashara na uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi zaidi ya 300. Mpaka sasa wadau 250 wa ndani, sawa na asilimia 75 ya lengo na wafanyabiashara kutoka nje 60, wamethibitisha kuhudhuria.

Akizungumza na waandishi wa habari kutoka Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti amesema uamuzi wa kuandaa wiki hiyo, umetokana na ukweli kuwa Kagera ina fursa lukuki za uwekezaji na biashara, lakini hazijatendewa haki.

“Tunataka Tanzania na dunia ijue umuhimu wa uchumi wa Kagera. Tanzania inapakana na nchi nane, kati ya hizo tatu zinapakana kabisa na Kagera lakini pia kuna nchi mbili nyingine za Afrika Mashariki ambazo ni rahisi kufikika kutokea hapa kwetu,” alieleza Gaguti.

Alitaja nchi zinazopakana na mkoa wa Kagera kuwa ni Uganda, Burundi na Rwanda zinazofikika kiurahisi na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na Sudan Kusini.

Alisema kupakana na kuwa karibu na nchi hizo ni fursa adhimu, ambayo haipo katika nchi yoyote, kwani katika nchi hizo zote, kuna idadi kubwa ya watu wanaokadiriwa kufikia milioni 190, ambao ni soko kubwa la bidhaa zinazozalishwa au zinazoweza kuzalishwa mkoani Kagera.

Akielezea fursa zilizopo mkoani humo, mkuu huyo wa mkoa alisema katika kilimo, Kagera inalima kwa wingi zao la ndizi, kahawa asilimia 50 ya inayozalishwa nchini inatoka mkoani humo, vanilla na mpunga.

Pia, alisema mkoa huo una fursa za kiuchumi kupitia misitu mikubwa iliyopo pamoja na utalii, ambapo hivi karibuni serikali imeyapandisha hadhi mapori matano ya akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika kuwa hifadhi za taifa.

Alisema pia kuna fursa ya uvuvi kutokana na uwepo wa vyanzo vingi vya maji, kama vile Ziwa Victoria, mito na maziwa madogo yapatayo 15.

Mbali na fursa hizo, ipo fursa ya ufugaji wa kisasa wa wanyama kama ng’ombe, mbuzi na kondoo kupitia ranchi za Taifa chini ya NARCO yenye ukubwa wa hekta 120,000, ambazo zinahitaji kuwekezwa kiasi cha kutosha ili kuleta tija na kuvutia ujenzi wa viwanda vya mazao ya mifugo, kama vile nyama, maziwa na ngozi.

SERIKALI imesema nchi ina chakula cha kutosha, lakini kuna uwezekano ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha, Bukoba

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi