loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Majaliwa ataka uwekezaji viwanda vikubwa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametaka Watanzania wanaoweza kuunganisha nguvu na wawekezaji kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kufanya hivyo kwa kuwekeza kwenye viwanda vikubwa.

Aidha, Majaliwa aliyeeleza kuvutiwa na Maonesho ya Wiki ya SADC, amesisitiza Watanzania kutumia maonesho ya viwanda ya SADC kukaribisha wageni kwa ukarimu, kutangaza mambo mazuri ya nchi ikiwamo vivutio vya utalii.

Alitoa mwito huo jana jijini Dar es Salaam baada ya kutembelea mabanda ya maonesho na kujionea bidhaambali mbali, zinazooneshwa na washiriki kutoka nchi wanachama wa jumuiya. Waziri Mkuu alisema kupitia maonesho hayo, nchi wanachama wa jumuiya wanayo fursa ya kuanzisha viwanda nchini. SADC inaundwa na nchi 16.

“Watanzania mnaoweza kuunganisha nguvu na nchi wanachama huu ndiyo wakati,” alisema Majaliwa na kusisitiza kuwa maonesho hayo ni fursa kubwa ya upatikanaji masoko ya bidhaa mbali mbali miongoni mwa nchi wanachama.

Akipongeza maonesho hayo, alisema ameona bidhaa za aina mbali mbali zinazozalishwa nchini zikiwa kwenye kiwango cha ubora wa hali ya juu, jambo aliloshauri Watanzania kujitokeza kwa wingi kujionea.

Alisema ni vyema watanzania wakatembelea kuona wengine wanafanyaje na pia kujionea bidhaa ambazo wapo baadhi ambao hawafahamu kama zinazalishwa nchini.

Miongoni mwa bidhaa zitokanazo na viwanda vikubwa, vya kati na vidogo zinazooneshwa ni pamoja na nguo, vyakula, kazi za mikono na bidhaa za ngozi.

“Ni fursa kubwa kwetu Tanzania kutumia nafasi hii kutangaza biadhaa zetu za ndani,” alisema.

Alisisitiza kuwa ni wakati mzuri wa kuhakikisha nchi inaendelea kuhamasisha wawekezaji wa nje kuja kuwekeza nchini kwani mazingira ni mazuri.

Kupitia maonesho hayo, Majaliwa alisema Tanzania inao uwezo mkubwa wa teknolojia ya kuendesha mitambo na upatikanaji wa mazao. Alitoa mfano wa miwa na kusema Tanzania haina shida ya sukari kwani fursa ipo nchini.

Akisisitiza ukarimu kwa wageni waliofika kushiriki maonesho hayo, alisema “maandalizi yote yamekamilika kwa kiasi kikubwa. Watanzania tutumie nafasi hii kuwakaribisha kwa ukarimu. Tutangaze vivutio vya utalii.”

Alitaja vivutio vya utalii kama vile mbuga za wanyama, mlima Kilimanjaro, fukwe na eneo la Oldupai Gorge ambalo ndilo chimbuko la binadamu, akisema ni wakati mzuri wa kuhakikisha wageni wanayafahamu na kuelewa yalipo.

Alitoa mfano wa mlima Kilimanjaro kuwa wapo watu wengine ambao wamekuwa wakitangaza kuwa ni wao. “Watanzania ni fursa kutangaza mambo yote nchini ikiwamo uwekezaji,” alisisitiza.

Alisema inafahamika kwamba Wizara ya Maliasili na Utalii inafanya kazi ya kutangaza utalii na vivutio vilivyopo lakini kwa kipindi hiki cha mkutano kila Mtanzania kwa nafasi yake anapaswa kuutangaza kwa wageni.

Maonesho ya viwanda ya SADC yalifunguliwa juzi na Rais John Magufuli ambaye alihimiza nchi wanachama kujizatiti kuwekeza kwenye viwanda.

Wageni kutoka nchi wanachama wanaendelea kuwasili nchini kushiriki maonesho hayo yatakayofungwa kesho na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein. Baadaye watawasili wakuu wa serikali na nchi za SADC kwa ajili ya mkutano wao wa 39 utakaofanyika Agosti 17 na 18.

SERIKALI imesema nchi ina chakula cha kutosha, lakini kuna uwezekano ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi