loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Afrika yahitaji Dola tril 6/- za miundombinu

AFRIKA ikiwemo Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), inahitaji Dola za Marekani trilioni sita katika kujenga na kuimarisha miundombinu ya uwekezaji ikiwemo barabara, bandari, reli, nishati, teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehema) ifikapo mwaka 2030.

Hayo yamebainishwa na wadau na washiriki wa Wiki ya Maonesho ya Nne ya Viwanda ya SADC, yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Akiwa miongoni mwa watoa mada, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko alisema Afrika na SADC zinahitaji fedha hizo Dola za Marekani trilioni sita katika kutekeleza miradi ya miundombinu mbali mbali ya uwekezaji ili kukuza uchumi na maendeleo ya kitaifa na kikanda.

Kakoko alisema tofauti na Asia na Ulaya na mabara mengine, suala la uwekezaji katika miundombinu halijapewa umuhimu wa kutosha barani Afrika.

Hivyo, alisema kuna haja kwa serikali za bara hilo na SADC kuona namna gani zinaweza kuongeza uwekezaji katika miundombinu ili kuongeza uzalishaji, mapato, ajira, kuimarisha ajira zilizopo pamoja na kuboresha maisha ya watu.

Katika hilo, alitoa mfano kuwa asilimia 80 ya biashara ya kimataifa, inafanyika kwa njia ya maji, hivyo ni muhimu kuimarisha miundombinu ya bandari kwa kuwa ndiyo milango inayotumika kuingiza bidhaa au kusafirisha bidhaa nje ya nchi.

“Maendeleo ya ukanda wa SADC yanategemea sana miundombinu imara kama bandari au reli kwa sababu ukosefu wa miundombinu au uwepo wa miundombinu duni inadumaza ufanisi wa kibiashara wa kikanda, kwa mfano Bandari ya Dar es Salaam inahudumia nchi sita kwa upande wa magharibi ambazo pia zinafanya biashara na nchi zingine kama Japan, China na India, kwa upande wa mashariki inazihudumia nchi za Mashariki ya Kati na Mashariki ya Mbali, hayo yote yanawezekana kwa sababu Tanzania iko kati kati kijiografia na inaweza kufanya biashara ya kibandari na nchi zingine,” amesema Kakoko.

Alisema asilimia 40 mpaka 50 ya bajeti ya Tanzania, inaelekezwa kwenye ujenzi na uimarishaji wa miundombinu mbali mbali ikiwemo ya usafiri na usafirishaji, nishati na mawasiliano, jambo ambalo ni muhimu katika kukuza uchumi na kuchochea maendeleo ya watu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Profesa Damian Gabagambi alisema moja ya changamoto zinazozikabili nchi za Afrika na SADC ni upatikanaji wa fedha za kuwekeza katika ujenzi na uimarishaji wa miradi ya miundombinu.

Alisema pamoja na hilo, pia kuna ugumu katika SADC wa kuvutia mtaji kutoka sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa miradi ya miundombinu, kwa kuwa hawana uhakika wa usalama wa fedha zao.

Kwa mujibu wa Profesa Gabagambi, katika kipindi cha miaka 50 sasa, Afrika imeshindwa kuvutia sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu kutokana na hatari mbali mbali zinazoweza kujitokeza na kuwatia hasara.

SERIKALI imesema nchi ina chakula cha kutosha, lakini kuna uwezekano ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi