loader
Picha

Wanafunzi wavumbua mmea unaovuta nyuki kwenye mzinga

NASRA Mpochi na Editha Barde ambao ni wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Chief Dodo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara ni miongoni mwa washiriki wa maonesho ya tisa ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania (YST).

Maonesho ya YST hufanyika nchini kila mwaka yakilenga kuwakutanisha wanafunzi wa masomo ya sayansi wa shule mbalimbali za sekondari kutoka mikoa 27 hapa nchini ambao huonesha ubunifu au tafiti walizozifanya kwa ajili ya kuisaidia jamii.

Kwa mwaka huu, wanafunzi hao, Nasra na Editha wameibuka washindi wa jumla wa maonesho hayo kupitia mradi wao unaojaribu kujibu swali la: ‘‘Je, mmea wa kivumbasi ni suluhisho kwa wafugaji nyuki?’’

Nasra anayesoma kidato cha nne, anasema walipata wazo la kuanzisha mradi huo kutokana na bustani iliyopo shuleni kwao ambayo ilikuwa ikiwavutia nyuki wengi. Anasema mimea aina ya kivumbasi ilikuwa imejiotea kwenye bustani hiyo hivyo, nyuki hao walikuwa wakienda kwa wingi na kuwasumbua wakati wakifanya shughuli zao. Kutokana na hali hiyo waliamua kufanya uchunguzi ili kujua sababu ya nyuki kupendelea kwenda kwenye mmea wa kivumbasi.

“Tulienda kujaribu kwa wafugaji wa nyuki. Tulichukua majani ya kivumbasi na kupaka kwenye sehemu za juu za mizinga na kukaa mbali kidogo ili nyuki wasiweze kutudhuru. Mara moja tuliona nyuki wanajaa kwenye sehemu ya mzinga,’’ anasema Nasra.

Anaongeza kuwa wingi wa nyuki hao katika mzinga kwa kutumia maji maji ya kivumbasi yalisaidia kupata asilimia 50 ya asali ambayo katika mizinga midogo hufikia hadi kilo sita ya asali.

Nasra anafafanua kwamba mti wa kivumbasi una harufu nzuri inayovutia nyuki kuingia kwenye mizinga. Hata hivyo, katika utafiti wao wamegundua kwamba mti huo huweza pia kutumika katika shughuli mbalimbali kama vile kutengeneza mafagio na kuoshea vyungu vinavyotumika kuwekea maziwa. Anasema mti huo pia ni kiungo kwenye chai au kufukuza mbu kwa kuuchoma na pia huweza kutumika kama dawa kwa kutibu vidonda vya tumbo na kuondoa gesi tumboni.

“Mmea huu unapatikana maeneo yanayolimwa kwani unaonekana kama magugu, kwenye mapori na maeneo mbalimbali,’’ anasema.

Kadhalika anasema katika mradi wao walichukua mizizi minne ya mmea wa kivumbasi pamoja na majani yake na kutengeneza kimiminika ambacho mtu akikipaka kwenye mzinga pamoja na kuweka majani hutoa harufu inayovutia nyuki. Anasema baada ya kuona matokeo katika mradi wao walianza kushawishi wanakijiji wanaofuga nyuki kutumia kivumbasi kwani ni mti unapatikana sehemu nyingi kwa gharama rahisi. Anasema walianza kuuza majani ya kivumbasi kwa shilingi mia moja kwa kila jani, hivyo kuongeza mtaji katika mradi wao.

“Shule imetusaidia kutupa eneo la kuotesha mmea wa kivumbasi na walitupa uwezo wa kutembelea vijiji vingine ili kuhamasisha matumizi ya mmea huu na kuona namna ya kuwatembelea wafugaji nyuki ili kuona uzalishaji wa asali katika mizinga yao,’’ anasema.

Msichana huyo anasema YST imewasaidia katika kuutambulisha mmea huo kwa jamii ili kuutumia kuvuta nyuki kwenye mizinga kwa unapatikana kwa gharama nafuu kwa kuwa ni hatua itakayowasaidia kuongeza uzalishaji wa asali ambayo huhitajika sana sokoni kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Anasema wanashukuru YST kupokea wazo lao kwani wanaamini wataendelea kuwasaidia kubadilisha mchanganyiko waliokuwa wanaufanya kutoka kimiminika kuwa gesi ili ianze kuuzwa nchini na kutumika kwa wafugaji nyuki.

Kwa upande wake, Editha anayesoma kidato cha tatu anasema mradi wao unaweza kuwasaidia watu kwa namna mbalimbali kwani mtu anaweza kuchukua mbegu za kivumbasi na kutengeneza bustani na kuwauzia wafugaji wa nyuki.

Anasema mtu anayetaka kutumia mmea wa kivumbasi anatakiwa kuchukua majani yake na kuyasaga nyumbani na kisha kuyajaza kwenye chupa zenye maji kiasi cha nusu lita. Binti huyo anaamini kwamba matumizi ya mmea huo, mbali na kuongeza ajira kwa watakaoulima kama zao la biashara lakini pia yataongeza manufaa kwa wafugaji wa nyuki na kuchangia katika ukuaji sekta ya viwanda.

Anasema malengo yao ya baadaye ni kuhakikisha wanabadilisha matumizi ya kivumbasi kutoka kimiminika kama ilivyo sasa na kuwa gesi ili waweze kuiuza ndani na nje ya Tanzania. Akizungumzia ushindi wao katika maonesho hayo ya YST, Editha anawataka vijana wenzake waendelee kutafiti na kuibuka na mambo makubwa zaidi na wale ambao hawakushinda wasikate tamaa.

“Tunashukuru YST Tanzania kwa kutuwezesha kuendeleza mradi wetu. Tunawashauri wenzetu wasikate tamaa bali wajitahidi na tunawahamasisha wasichana wengine wasikate tamaa bali wapende masomo ya sayansi kwani tunaweza,” anasema.

Mwalimu wa masomo ya Fizikia na Hisabati wa shule wanayosoma mabinti hao, Jackson Warae anasema kwa kushirikiana na wanafunzi wake waliamua kufanya mradi huo baada ya kuona kuna fursa kwenye uzalishaji wa asali.

Anasema walihoji baadhi ya wafugaji wa nyuki wakagundua kwamba moja changamoto walio nayo ni kurahisha makundi ya nyuki kuingia kwenye mizinga kwa sababu hakuna kitu chochote kinachowavutia nyuki kuingia hadi wanaposubiri msimu wa maua.

Mtaalamu wa nyuki kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Kanda ya Magharibi, Karimu Solyambungu aliwahi kuliambia gazeti hili kwamba wafuga nyuki wamekuwa wakipaka mafuta ya samli na hata kinyesi cha ng’ombe ili kuvutia nyuki kwenye mzinga lakini akasema njia inayotumika zaidi ni kupaka nta ya nyuki kwenye mzinga.

Solyambingu anasema mzinga unatakiwa uwe umening’inizwa mahali pazuri na mfugaji ahakikishe hali ya usafi na kusiwe na wadudu kwani nyuki hawapendi kukaa kwenye mzinga mchafu. Mtaalamu huyo anasema kwa mfugaji wa nyuki Tanzania kuna uhakika wa kufuga nyuki kokote kwa sababu tunayo makundi mengi ya nyuki tofauti na Ulaya ambapo makundi ni haba na bado yanakufa kutokana na baridi.

“Mfugaji nyuki wa Ulaya analazimika kununua pia makundi ya nyuki kutoka kwa mtu ambaye anayo, lakini huku kwetu ukishatundika mzinga wako unaweka kivutio (chambo) na kundi la nyuka linakuja lenyewe,” anasema.

Mwalimu Warae anasema huu ni mwaka wa nne kushiriki kwenye mashindano ya YST bila mafanikio hadi walipotafuta wazo jipya na kushinda. Anasema shuleni kwao kuna mti wa kivumbasi ambao umekuwa ukistawi na kutoa harufu nzuri na kwamba wakati wanaanza mradi huo, ilikuwa kipindi cha masika ambapo waliona nyuki wengi ambao wanapenda kukaa kwenye mmea huo kutokana na maua yake.

Anasema waliona kwamba wakifunga mzinga eneo lile kutakuwa na kivutio kikubwa cha nyuki ambao wataingia wenyewe kwenye mzinga bila kuwafuata eneo lingine “Wanafunzi hawa wanauelewa mzuri wa lugha ya Kingereza, wanauelewa darasani na kwa kujiamini walitetea mradi huu mpaka wakashinda,’’ anasema. Mwalimu Warae anaipongeza YST kuwa imekuwa msaada mkubwa katika kuibua vipaji na ubunifu kwa watoto. Anaiomba serikali isisitize ufundishaji wa masomo ya sayansi na utumiaji sahihi wa maabara katika shule nchini.

Mwalimu huyo anaamini kwamba wanafunzi wote wanaoshiriki kwenye maonesho hayo watakuwa watafiti wazuri kwani wameanza kujifunza masuala hayo kuanzia ngazi ya sekondari. Asali, mbali ya kuwa chakula bora kabisa, hutumika pia kama dawa kwa kuila yenyewe au kutibia vidonda. Asali pia hutumika kutegenezea dawa mbalimbali na vipodozi. Nta hutumika kutengenezea vidonge vya rangi mbili (capsules), pia kuna mazao ya asali kama vile maziwa ya nyuki, gundi, mkate na sumu ya nyuki vinazotumika pia kwa shughuli mbalimbali ikiwemo tiba.

Akitoa zawadi kwa washindi, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, anasema maonesho hayo yanaashiria kuwa elimu inayotolewa nchini inakidhi viwango vya ubora kwani watoto wameonesha bunifu zenye uwezo wa kutatua changamoto katika jamii. Anasema amefurahi kuona miradi iliyooneshwa imeongezeka kutoka 81 hadi kufikia 95 pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wasichana walioshiriki maonesho hayo.

Profesa Ndalichako alitumia mwanya huo kueleza kwamba katika kipindi hiki kumekuwa na mwamko mkubwa wa wasichana kupenda masomo ya sayansi kuliko hapo awali. Anawahimiza walimu kuwafundisha wanafunzi namna ya kufanya tafiti ambazo zitasaidia ukuaji wa uchumi.

“Tutatumia mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kuona namna ya kuwasaidia wabunifu mbalimbali nchini kwani suala la kuwatambua na kuwaendeleza wabunifu limepewa kipaumbele zaidi na SADC,’’ anasema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk Amos Nundu anasema kwa muda mfupi vijana kupitia YST wamefanya tafiti ambazo zikiendelezwa zitaleta mabadiliko chanya katika taifa na ujenzi wa viwanda.

Anasema mfumo huo ni mzuri kwa kuwa unasaidia kuwajenga vijana uwezo wa kufanya tafiti zenye tija zitakazochangia ukuaji wa uchumi wa viwanda. Mwanzilishi Mwenza wa YST, Dk Gozbert Kamugisha ameiomba serikali kuendeleza kazi za kibunufu zilizofanywa na wanafunzi wote walioshiriki.

“NILIANZA kuzaa nikiwa binti mdogo wa miaka 19 na mtoto ...

foto
Mwandishi: Francisca Emmanuel

Weka maoni yako

1 Comments

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi