loader
Picha

Idi ya kuchinja na manufaa ya hija

TAARIFA zilizopo zinaonesha kwamba Idi ya Kuchinja (Idi al-Adh-ha) au Idi Kuu inatazamiwa kusherehekewa hapa Tanzania Jumatatu. Lakini wale wanaofuata mwezi wa kimataifa na wanaoamini kwamba siku ya Arafa ambayo Waislamu wamehimizwa kufunga inapaswa iende sambamba na mahujaji wanaposimama katika viwanja vya Araf katika mji wa Mtakatifu wa Makka, Saudi Arabia, watasherehekea Idi Jumapili.

Idi katika mwezi huu ambao kwa Kiislamu hujulikana kama Dhulhija, hufanyika siku ya 10 tangu kuandama kwa mwezi na funga ya Arafa hufanyika siku ya 9. Kwa mwandamo wa mwezi wa Saudi Arabia leo ni Dhulhija 7 lakini kwa wasiofuata mwezi wa Kimataifa kama Tanzania, leo Alhamisi Agosti 8 ni Dhulhija 6. Waislamu bado wanaendelea kutofautiana miongoni mwao kama usahihi ni kufuata mwezi kokote unakoonekana duniani kwa sababu dunia haipishani saa 24 au kila watu wafuate mwandamo wao wa mwezi.

IDI YA KUCHINJA NI NINI?

Idi ya Kuchinja ni sherehe inayofuatia kumalizika kwa ibada ya Hija ambayo ni moja ya nguzo kuu tano za Uislamu. Kwenda kuhiji katika mji mtakatifu wa Makka ni lazima kwa kila Muislamu mwenye uwezo wa kifedha na siha njema. Anayekataa kwenda huko makusudi wakati ana uwezo huo huandikiwa dhambi. Mwenyezi Mungu katika Kurani alimwamuru Mtume wake Ibrahimu akisema: “Na uwatangazie watu.

Watakujia wewe watu hali ya kuwa ni wenye kutembea kwa miguu kuelekea kwenye nyumba tukufu ya Mungu kwa ajili ya kufanya ibada ya Hija na ibada ya Umra. Kuna watakaokuja wakiwa wamepanda vipando na wale watakaokuja kwa kutembea kwa miguu tena kutoka maeneo ya mbali kabisa kwa ajili ya kutii na kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu.

Ni kushuhudia na kutekeleza yale ambayo manufaa yatawaendea wao kwa kutaja jina la Mwenyezi Mungu katika masiku maalumu.” Kuchinja mnyama ni kuungana na kisa cha Mtume Ibrahim ambaye aliweka nadhiri ya kumchinja mwanawe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na alipomzaa mwanawe huyo (Ismael) uzeeni, Mwenyezi Mungu akamkumbusha kutekeleza nadhiri hiyo. Alipoanza kumchinja ndipo, Mwenyezi Mungu akamletea kondoo kama mbadala wa mwanawe baada ya kuridhika kumwona mja wake akiwa tayari kumchija mwanawe kwa ajili yake.

MASHARTI YA HIJA

Hija ina masharti matano kwa mwanamume na kwa mwanamke linaongezeka sharti moja. Masharti hayo ni pamoja na kuwa Muislamu, kuwa na akili timamu, kufikia umri wa balehe na kuwa na uwezo wa kifedha na kiafya. Kwa mwanamke linaongezeka sharti moja la kuandamana hija akiwa na maharimu wake, yaani mtu kama mumewe, baba au kaka.

NGUZO ZA HIJA

Kuna nguzo nne za hija ambazo ni pamoja na kutia nia ya dhati moyoni kwamba kinachokupeleka Makka ni ibada na siyo kitu kingine, kisha kusimama viwanja vya Arafa, kutawafu na kisha kufanya safari baina ya vilima vya Safa na Mar-wa (kama alivyokuwa akifanya Hajira, mke wa Ibrahim baada ya kuachwa pekee jangwani). Mahujaji wote katika siku ya Arafa huimba wimbo mmoja wa “Labeik Allahumma Labeik, Labeika la sharika laka Labeik, innalhamda waniimata, laka walmulk. Laa shariika laka.

Maana yake ni: Nimekuitikia Mola wangu, nimekuitikia. Nimekuitikia ewe usiye na mshirika nimekuitikia. Hakika, sifa njema na neema na ufalme ni vyako wewe tu. Huna mshirika. Nimekuitikia.

WAJIBU KATIKA HIJA

Hujaji anatakiwa kufanya wajibu zifuatazo ambazo ni pamoja na kuhirimia (kutia nia) kufanya ibada na kulala Mina siku tatu au mbili. Jua likizama baada ya siku ya pili bado mahujaji wakiwa Mina hulazimika walale hapo Mina. Wanazuoni wengi wanasema kulala Mina ni wajibu lakini wengine wanasema si wajibu.

Wajibu wa tatu kwa hujaji ni kusimama Arafa hadi jua kuzama (asiposimama hadi jua kuzama anapaswa kutoa faini ya mnyama). Wajibu wa nne ni kulala katika viwanja vya Muzdalifa ambako hujaji hutakiwa, mbali na ibada za swala kuleta dua yoyote. Na wajibu mwingine ni kupiga nguzo kwa mpangilio kama ishara ya kumfukuza shetani. Hili ni tukio pia lililofanywa na Mtume Ibrahim. Wajibu mwingine kwa hujaji ni kunyoa au kupunguza nywele. Kunyoa ni bora zaidi kwani Mtume Muhammad (SAW) aliwaombea wenyekunyoa mara mbili na wenye kupunguza mara moja. Nguzo ya saba ni kuaga mji wa Makka (Twawaf alwadai).

MANUFAA YA HIJA

Safari ya hija inaelezwa kwamba inasaidia sana kuimarisha imani ya moyo kwa Mwenyezi Mungu na pia ni tiba ya mwili, kwa sababu ni safari inayogusa mambo mbalimbali yanayomhusu mtu. Mosi, katika kipindi cha Hija, mahujaji wote huvaa aina ya vazi la kawaida sana. Kila Muislamu huondoa vazi lake alilozoea na kuvaa vazi hilo linalojulikana kama ihram.

Vazi hili la ihram lina athari kubwa ya kisaikolojia kwa mahujaji. Pamoja na kuweka kando nguo walizozoea kuvaa katika maisha ya kawaida, kadhalika wanaweka kando madaraja yao ya duniani na kujiona ni watu walio sawa mbele ya muumba wao ambao ndio wamesafiri kwa ajili yake.

Kwa mantiki hiyo, hujaji ambaye ni askari polisi kwa mfano, anakuwa nje ya gwanda lake alilozoea, mkulima hayuko tena katika mavazi yake ya shambani, daktari au muuguzi hayuko tena katika nguo zake nyeupe na wala meneja hayuko kwenye suti yake... Wote wako pamoja wala hujui nani ni nani. Hija inaelezwa kuwa ni mfano wa namna binadamu watakapokusanyika na kusimama mbele ya Mola wao siku ya Kiyama kwa ajili ya kulipwa yale waliovuna duniani.

Pili, mahujaji hufanya matendo ya aina moja yaliyoelezwa katika sheria kama vile kufanya tawwaf (kuzunguka Kaaba) katika mwelekeo mmoja, au kufanya sa`i (kutembea baina ya vilima vya Safa na Mar-wah. Katika matendo yote ya Hija hakuna tofauti baina ya tajiri na maskini, wenye misuli na walio dhaifu, wenye vyeo na wasio na vyeo, weusi na weupe, wanaotoka Magharibi na wanaotoka Mashariki wala Magharibi na Mashariki. Wote wanakuwa sawa. Tatu, hija pia ni sehemu ya kumpa mtu nafasi ya kujitazama upya maisha yake yaliyopita na yale yaliyosalia katika hii dunia.

Ni kipindi kizuri cha kuomba msamaha kwa Mwenyeazi Mungu Mtukufu kuhusu madhambi mtu aliofanya na kupanga maisha mapya ya ucha Mungu yanayofuata. Nne, Safari ya Hija inaaminika kutibu magonjwa mengi ya mwili na ya kiroho. Matendo kama kufanya tawwaf, sa`i, na kusimama katika Mlima Arafah yanasaidia hujaji kujenga misuli yake.

Shughuli hizi za msuli husaidia kupunguza sukari katika damu hususan kwa watu wanaosumbuliwa na kisukari. Kunywa maji ya kutosha kutoka kisima cha Zamzam husaidia mfumo wa mkojo na husaidia kuondokana na vijiwe katika mirija ya mfumo wa mkojo na kwenye figo. Kwa hiyo Hija inamtoharisha mtu kutokea ndani ya mwili wake kama ambavyo kushika udhu (kuosha uso, mikoni, kupaka maji kichwani na kuosha miguu) kunanavyotwaharisha mtu juu ya ngozi. Mashehe wanasema Hija humpa mtu tohara ya mwili na roho.

Tano, Hija ni mfano pia wa kumfanya mtu kuwa imara pale anapokuwa ameamua kufuata njia iliyo madhubuti. Mahujaji katika safari yao pia humkumbuka Bibi Hajar, wakati Mtume Ibrahim alipomwacha peke yake kwenye jangwa, yaani Makkah akiwa peke na mwanae aliyekuwa ndiye kwanza tu amezaliwa. Sita, Mahujaji wanatazamiwa kutumia pesa nyingi katika kipindi chote cha Hija kwa sababu tu ya kutekeleza wito wa muumba wao. Hii ni njia nyingine ya mtu kujitibu ubahili kwa ajili ya kutekeleza ibada.

WANAOBAKI MAJUMBANI

Ili kuungana na waloko Hija, wanaobaki majumbani nao kuna mengi ya kufanya, ambayo ni pamoja na kuzidisha ibada katika siku 10 za mwezi huu tangu ulipoandama, kuswali Idi na kisha kuongeza ibada katika siku tatu zinazofuata. Kimsingi, mwezi wa Dhulhija ni moja ya misimu ya heri ambao Mwenyezi Mungu amewapa Waislamu ili ‘wajipinde’ kwa ajili ya ibada na hivyo wapate kufaulu siku ya Kiyama.

Licha ya Mwenyezi Mungu kutaja siku hizo 10 katika Kurani, hadithi nyingine iliyopokelewa na ibn Jabr kutoka kwa Mtume Muhmmad (SAW) inamkariri akisema kwamba katika siku bora duniani zilizoangaziwa na jua, ni siku 10 za mwezi wa Dhulhija. Hadithi hii ameipa usahihi mwanazuoni wa zama hizi, Albany. Kwa usiku, inaelezwa kwamba siku 10 bora ni za mwisho wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kwa mchana ni hizi za Dhulhija.

Mashehe wanasema ubora unaopatikana katika hizi siku 10 za mwezi wa Dhulhija si kingine bali ni kule kukusanyika kwa watu Makkah kwa ajili ya kufanya ibada. Na siku nyingine bora zaidi ni siku ya Idi ambayo ni siku ya kuchinja na kisha siku inayofuata, kwa maana ya siku ya 11 pia ni siku bora.

Kimsingi, mbali na siku 10 za Dhulhija, siku tatu zinayofuata nazo ni bora na Waislamu wanatakiwa kukithirisha ibada mbalimbali kwani Mtume Muhammad anasema siku hizo ni za kula na kunywa na kumtaja kwa wingi Mwenyezi Mungu Mtukufu. Mtu pia anaweza kuchinja katika siku mbili zinazofuata endapo alishindwa kuchinja siku ya Idi.

TANGU maambukizi ya virusi vya corona yabishe hodi nchini Machi ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi