loader
Picha

Simba,Yanga kimataifa zaidi

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya kimataifa Yanga, Simba na KMC leo wanashuka dimbani kwenye viwanja tofauti ndani na nje ya nchi kusaka ushindi katika michezo yao ya awali.

Yanga itakuwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kuanzia saa 12:00 jioni ikiwakaribisha Township Rollers ya Botswana katika mchezo wa Ligi ya mabingwa Afrika.

Mchezo wa Yanga ni wa kisasi hasa baada ya kufungwa mabao 2-1 na timu hiyo msimu wa mwaka juzi kwenye uwanja huo na baadaye kurudiana ugenini na kutoka suluhu na hivyo Yanga kung’oka kwenye michuano.

Hautakuwa mchezo rahisi kwa timu zote mbili kutokana na kila mmoja atataka kupata matokeo kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua inayofuata. Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera alisema juzi kuwa kutokana na usajili waliofanya msimu huu ana matumaini ya kuwakilisha vizuri.

“Wanayanga wajitokeze kwa wingi uwanjani kwasababu tuna kikosi kizuri cha msimu huu chenye kasi, ambacho kitafanya vizuri, lengo letu tunataka kupambana kwenye uwanja wa nyumbani na kupata matokeo mazuri,”alisema.

Kocha huyo baada ya kumaliza wiki ya wananchi kwa mechi ya kirafiki waliyotoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Kariobangi Sharks alitaka mechi nyingine kuangalia wachezaji wake kwa mara ya mwisho.

Tayari katika kambi ya muda mfupi waliyoweka Zanzibar aliwajaribu wachezaji wake katika mechi mbili za kirafiki dhidi ya Mlandege walioshinda mabao 4-1 na dhidi ya Malindi waliotoka sare ya bao 1-1 hivyo huenda amepata kikosi chake cha kwanza kwa ajili ya kuwakabili Township.

Kaimu Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Dismas Ten alisema huenda wakakosekana wachezaji watatu baada ya kuchelewa kwa leseni zao ambao ni kipa Farouk Shikalo, David Molinga na Mustapha Selemani lakini wakati wowote zinaweza kupatikana.

Kocha mkuu wa Township Rollers, Thomas Trucha alisema anatarajia mchezo wenye upinzani mkubwa kutoka kwa Yanga kwakua kikosi cha wenyeji wao kimebadilika tofauti na walivyokutana mwaka juzi. Viingilio katika mchezo wa Yanga ni sh. 5000 kwa viti vya mzunguko, 15,000 kwa VIP B na C na 50,000 kwa VIP A.

Kwa upande wa Simba itakuwa ugenini Msumbiji dhidi ya UD Songo utakaochezwa saa 11:00 jioni. Timu hiyo awali iliweka kambi Afrika Kusini na baadaye kurejea Dar es Salaam kwa tamasha la wiki ya Simba lililohitimishwa hivi karibuni kwa ushindi wa mabao 3-1 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Power Dynamos ya Zambia.

Kasi waliyoanza nayo inaleta matumaini kwa mashabiki wake kuwa msimu huu huenda pia wakafanya vyema zaidi kutokana na usajili mzuri waliofanya. Kabla ya kuwafuata Songo, Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Patrick Aussems alisema walifanya mazoezi bila wachezaji saba hivyo, anafikiri mchezo utakuwa mgumu.

Alisema wamejipanga kupambana kiushindani na kupata matokeo mazuri ingawa anafikiri watakuwa bora zaidi baada ya wiki mbilii zijazo. “Tumejipanga vizuri na tayari tumewasoma wapinzani wetu na kuwajua ila haitoshi kuridhika kwasababu matokeo yanapatikana zaidi uwanjani,”alisema.

Kwa upande wa Kombe la Shirikisho, KMC itachuana na AS Kigali ya Rwanda kuanzia saa 10:00 jioni, nayo iko katika ubora baada ya kushiriki michuano ya Kagame na kuonyesha ushindani mzuri. Usajili wao bora waliofanya msimu huu unaleta imani kuwa wanaweza kuwakilisha vizuri kwa mara ya kwanza chini ya Kocha mwenye uzoefu Jackson Mayanja ambaye aliwahi kuzifundisha Simba na Kagera Sugar.

Kocha Mayanja alisema utakuwa mchezo mzuri ingawa anafikiri hautakuwa rahisi. “Tunatarajia kupata matokeo kule, tatizo wachezaji wetu wa kigeni wataukosa mchezo kwasababu hawajapata leseni lakini tutajiandaa kwa mbinu,”alisema.

Nahodha wa kikosi hicho kipa mkongwe mwenye uzoefu wa kimataifa Juma Kaseja alisema atakayejiandaa vizuri ndani ya uwanja ndiye atakayepata matokeo mazuri. “Naamini kwa uzoefu wangu na wengine tutasaidia vijana ambao wanaenda kucheza kwa mara ya kwanza kuwaongoza na kucheza kwa umoja kwa kulenga kupata ushindi,”alisema.

TIMU ya Tanzania Bara ya wasichana walio chini ya Umri ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi