loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Moto waua watu 68 Morogoro

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Kebwe Stephen Kebwe amesema, hadi sasa idadi ya watu waliokufa kutokana na ajali ya kupinduka na kulipuka kwa lori la mafuta imefikia 68.

Amemweleza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mjini Morogoro kuwa, watu 62 walikufa kwenye eneo la ajali na wengine sita wameaga dunia hospitalini.

Majaliwa amekwenda kwenye eneo ilipotokea ajali hiyo na kushuhudia mabaki ya gari lililolipuka jana saa mbili asubuhi.

Lori hilo aina ya Scania lilipinduka sehemu ya Mzambarauni eneo la Msamvu, Manispaa ya Morogoro katika Barabara Kuu ya Dar es Salaam – Morogoro jana.

Ajali hiyo ilitokea saa 2:20 asubuhi ambayo mashuhuda walieleza ilisababishwa na mwendesha bodaboda aliyekuwa na abiria wake mwanamke na mtoto kukatisha barabara hali iliyomfanya dereva wa lori hilo kuwakwepa, lakini likapinduka kiubavu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Wilboad Mutafungwa amethibitisha kuwa lori lililobeba mafuta aina ya petroli likitoka Dar es Salaam kabla ya kufika Msamvu Stendi lilipinduka upande wa kushoto wa barabara.

Kamanda Mutafungwa akiwa eneo la ajali, alisema baada ya kupinduka katika eneo hilo lenye makazi wa watu na karibu ya barabara, ghafla ukajitokeza moto mkubwa ambao ulilipuka na kuwaunguza watu wengi takribani watu 62 walifariki dunia papo hapo kwa kuungua moto.

“Miili iliopolewa kwenye eneo la tukio na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ili kuhifadhiwa na kubaini majina yao ni akina nani na ufuatiaji unaendelea ili kujua ni akina nani,” alieleza Kamanda Mutafungwa.

Alisema eneo la ajali, zaidi ya pikipiki 26 na baiskeli sita ziliteketea na moto huo na uchunguzi utafanyika ili kubaini zilifikaje hapo na kwa lengo gani, ikihisiwa walitaka kuiba matufa yaliyokuwa yakitiririka baada ya lori kupinduka.

“Tumefanikiwa kuuzima moto huu mkali wa petroli majira ya saa nne na nusu asubuhi hii kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na wananchi pamoja na Tanesco kwa kuzima umeme maeneo haya,” alieleza Kamanda Mutafungwa.

Alisema baada ya kutokea kwa ajali hiyo, walielekeza magari ya kutoka Dar es Salaam kupita njia mbadala ikiwa na magari yanayotoka mikoa ya Iringa na Dodoma kupita njia ya zamani ya Dar es Salaam.

Kamanda Mutafungwa pia aliwaonya wananchi waliokuwa wameiba matuta ya petroli na kuyafadhi majumba mwao kuyasalimisha Polisi kabla ya msako kufanyika katika maeneo hayo.

Kwa mujibu wake, kwa vile gari hilo limeteketea na moto imekuwa ni vigumu kutambua namba zake, mmiliki wake ama kampuni yake, na lilikuwa linaelekea mkoa. Alisema uchunguzi unafanyika kubaini yote hayo. Licha ya kuungua vibaya sehemu ya mbele ya gari hilo, lakini namba za tela la mafuta zilisomeka T645 CAN.

Aidha, katika gari kulitolewa miili mitatu ambayo haijatambuliwa kama ni dereva au watu walikuwapo eneo la ajali. Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen alisema ajali hiyo imeleta maafa makubwa kwa kuwapoteza watu hao na kusababisha majeruhi wengi waliolazwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.

“Nimeagiza watumishi wa hospitali na madaktari wasiende mapumziko na wale waliopo majumbani waitwe hospitali wanapaswa kufika kazini kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa hao na kutengwa kwa wodi mbali mbali za kuwalaza,” alisema Dk Kebwe.

Mkuu wa mkoa pia alisaidia kuwahudumia majeruhi wakiwa wodini kutokana na taaluma yake ya daktari bingwa wa magonjwa ya binadamu.

Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood pamoja na kutoa mablanketi 100, maji na dawa vyenye kufikia thamani ya Sh milioni tano, alitumia nafasi hiyo kuwatahadharisha wananchi kuacha tabia ya kukimbilia ajali zinapotokea hasa magari ya kubeba mafuta, bali waliokoe maisha yao kwanza.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa, Noel Kazimoto alisema pamoja na wadau akiwemo mbunge kutoa misaada huo, pia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa imewasilisha ombi kwa Bohari ya Dawa (MSD) la kupatiwa dawa za dharura ikiwa na magari 10 ya kubeba majeruhi wanaohamishiwa Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Rita Lyamuya alisema walipokea miili 62, kati ya hiyo 58 ni ya wanaume na wanne ni wanawake akiwamo mtoto mmoja na pia majeruhi 70 na kati ya hao, 39 walipatiwa rufaa ya kwenda kutibiwa Muhimbili.

Shuhuda Raymond Stephen alidai dereva wa lori hilo alikuwa akijaribu kukwepa mwendesha bodaboda aliyekuwa amebeba abiria mwanamke na mtoto wake, ndipo likazidi kushoto mwa barabara na kupinduka.

Stephen alisema baada ya kupinduka na wakiwa katika jitihada za kuwaokoa waliomo ndani ya gari hilo, walijitokeza watu wengi hasa wa bodaboda kwa akili ya kuiba mafuta yaliyokuwa yakitiririka kutoka juu ya tangi na chini, lakini alitokea kijana ambaye ni mtumiaji wa dawa za kulevya “teja” kuanza kuchomoa betri.

Alisema baadhi walioona watu wanazidi kuiba mafuta na “teja” huyo, wengi wao waliacha kutoa uokozi na kulikimbia eneo hilo na ndipo teja hilo alipoona anashindwa kung’oa betri hiyo, hivyo alichukua chuma na kuigonga na kung’oa kwa nguvu.

Shuhuda mwingine, Alawi Abdulrahman alidai chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa bodadoda, lakini kutokea kwa moto uliosababisha vifo na majeruhi ni mtu mmoja ambaye ni mtumiaji wa dawa za kulevya, kuichomoa betri kwa nguvu na hivyo kusababisha tangi la mafuta ya petroli kulipuka na kuleta maafa hayo.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo alizungumza na wananchi waliofika hospitalini alisema licha ya kuwepo kwa akiba ya damu, kutokana na kiwango kikubwa cha majeruhi, walikuwa wanahitaji damu ya kutosha.

“Tumepungukiwa akiba ya damu…umejitokeza upungufu wa damu na hamjawahi kuona DC akitangaza kuomba damu. Nimekuja kwenu kuwaomba jitokezeni kutoa damu ili kunusuru majeruhi waliopo wodini,” alisema Chonjo.

Chonjo alisema kati ya majeruhi hao, 39 wanapaswa kuhamishiwa Muhimbili na madaktari wameeleza kuwa hawawezi kuwasafirisha bila kuwawekea damu, hivyo ni jukumu la kila mwananchi mwenye mapenzi mema kujitokeza kuchangia damu ili kuokoa maisha yao.

Pamoja na hayo, aliwafahamisha wananchi wa Manispaa ya Morogoro kuwa majina ya waliojeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, aliyasoma hadharani na yamebandikwa Uwanja wa Jamhuri.

Alisema baadhi ya miili 63 iliyohifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, baadhi inaweza kutambulika na ndugu zao na mingine imeungua vibaya na kwamba madaktari wameeleza kuwa ile isiyotambulika wanatumia vinasaba DNA ili kuwezesha ndugu na jamaa kuwatambua.

Baada ya kutokea janga hilo, baadhi ya viongozi waliotembela majeruhi wodini ni Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba pamoja na baadhi ya wabunge wa Mkoa wa Morogoro.

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Liberatus Sabas na Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye walifika eneo la ajali na kuhakikisha wanashirikiana na wenyeji kufanikisha uokozi pamoja na kusaidia kwa jambo lolote linalohitaji msaada.

Hii ni ajali kubwa ya moto wa mafuta ya petroli kutokea nchini baada ya ile iliyotokea Kijiji cha Isongole wilayani Rungwe mkoani Mbeya ambalo wananchi wengi walipoteza maisha na jingine Mbezi jijini Dar es Salaam.

BODI ya Michezo ya Kubahatisha nchini kwa kushirikiana na Mamlaka ...

foto
Mwandishi: John Nditi, Morogoro

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi