loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Maombi kuepusha majanga yatawala swala ya Iddi

WATANZANIA wametumia Swala ya Idd el – Haji kuombea nchi kuepukana na majanga kama lile la watu 75 kupoteza maisha baada ya lori la mafuta kulipuka katika eneo la Msamvu mjini Morogoro, Jumamosi iliyopita.

Akizungumza katika Swala ya Idd el Haji Kitaifa iliyofanyika katika viwanja vya Msikiti wa Kibadeni Chanika jijini Dar es Salaam jana; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo aliyekuwa mgeni rasmi, aliwawataka watanzania kuungana pamoja kuendelea kuliombea taifa kuepuka na majanga mbalimbali.

Waziri huyo alisema Watanzania wanapaswa kuliombea Taifa ili liondokane na majanga kama lile la Morogoro ambapo pia aliwataka watanzania kuwaombea watu waliopoteza maisha na waliojeruhiwa kutokana na tukio hilo.

“Janga hili la juzi linatukumbusha janga lililotokea katika Kijiji cha Isongore Mkoani Mbeya miaka ya nyuma, lilitokea na watu wengi walipoteza maisha, janga kama hili si Tanzania pekee, sehemu nyingine kama Ghana, Nigeria, Congo limeshawahi kutokea hivyo tujitahidi kuombea majanga kama haya yasitokee,” alisema Waziri Jafo.

Kwa upande wake Shehe Mkuu wa Tanzania, Abubakary Zubeir amekemea shutuma kuwa baadhi ya kauli ndani Bakwata zinaipotosha serikali na kusema hawatavumilia kusemwa vibaya.

Mufti Zubery alisema, baraza hilo hutoa elimu hivyo watu wasiwachonganishe na serikali kwa kutafsiri vibaya kauli zake. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Taifa Bakwata, Hamisi Mataka alisema ni muhimu baraza hilo kufanya mazungumzo ili kuondoa tofauti inayoendelea ya Waislamu wa nchi moja kuswali Sikukuu ya Idd siku tofauti na kwamba hali hiyo inaondoa umoja.

Kutoka Dodoma; Shehe wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu amesema kazi ya Mola haina makosa alipangalo Mola huwa hakuna wa kulaumiwa kutokana na vifo vya ajali ya moto vilivyotokea mkoani Morogoro ambapo amewaomba Watanzania kuwaombea waliofariki dunia pamoja na majeruhi wa tukio hilo.

Akizungumza jana katika Swala ya Iddi iliyofanyika katika Msikiti wa Gaddaf jijini hapa, Shehe Rajabu pia alipongeza viongozi wa ngazi za juu katika serikali kwa kuwasaidia majeruhi wa tukio hilo pamoja na kuwahifadhi wale ambao wamefariki dunia mjini Morogoro.

Kutoka Mwanza; Bakwata Mkoa wa Mwanza imetoa salaamu za pole kwa Rais Magufuli, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk Stephen Kebwe na wakazi wa mkoa wa Morogoro kwa ujumla kufuatia tukio la ajali ya moto iliyotokea mkoani Morogoro Agosti 10 mwaka huu na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 70.

Shehe wa Mkoa wa Mwanza Hassan Kabeke akihutubia waumini wa dini ya kiislamu kwenye sherehe za Sikukuu ya Idd el Haji ambayo ilifanyika katika uwanja wa Nyamagana alisema tangu kutokea kwa ajali hiyo, serikali yote imehamia mkoani Morogoro akiwemo Waziri Mkuu, Mawaziri na viongozi wengine wa serikali ambao wameonesha ushirikiano wa pamoja katika kukabiliana najanga hilo.

Kutoka Zanzibar; Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein ameitaka jamii kuacha kusuluhishana matukio ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia. Akilihutubia Baraza la Idd katika uwanja wa Dole Kizimbani Wilaya ya Magharibi Unguja, Dk Shein alisema hakuna mtu aliye juu na sheria na anayefanya vitendo vya udhalilishaji afikishwe mbele ya vyombo vya dola.

Aidha amewataka viongozi wa dini ya kiislamu pamoja na mashehe kwa ujumla kutoa elimu na mawaidha kuhusu njia ya kukabiliana na vitendo hivyo ambavyo haviendani pamoja na tabia ya binadamu. Imeandikwa na Regina Mpogolo, Dar, Magnus Mahenge, Dodoma, Nashon Kennedy, Mwanza na Khatib Suleiman, Z’bar

BODI ya Michezo ya Kubahatisha nchini kwa kushirikiana na Mamlaka ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi