loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Nchi 5 EAC zaanika fursa kwa Watanzania

MABALOZI watano wa Tanzania katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wametaja fursa za biashara na uwekezaji, zinazoweza kutumiwa na Watanzania katika nchi hizo ikiwemo mazao ya kilimo, bidhaa za viwandani, uchukuzi na madini.

Pamoja na hayo, mabalozi hao wameshauri kuanzishwa kwa masoko ya kimataifa katika mikoa ya mipakani ili kurahisisha na kuhamasisha biashara baina ya mikoa hiyo na nchi hizo inazopakana nayo.

Mabalozi hao wanaotoka katika nchi za Uganda, Kenya, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), waliyasema hayo kwa nyakati tofauti mjini Bukoba jana, walipokutana na wafanyabiashara wa Tanzania katika siku ya kwanza ya Wiki ya Uwekezaji mkoani Kagera.

Balozi wa Tanzania nchini DRC, Paul Meela alibainisha kuwa nchi hiyo ya Congo ni soko kubwa kwa Tanzania, endapo litatumiwa vizuri, kwani inahitaji chakula, usafiri wa uhakika, walimu wa Kiswahili na bidhaa za viwandani kama vile nondo na chuma.

Alieleza kuwa nchi hiyo ina utajiri wa madini yenye thamani ya dola za Marekani trilioni 24, eneo kubwa linaloingia mara mbili ya Tanzania ikiwa ni watu milioni 81 wakati Tanzania ina watu milioni 55. DRC ni ya 12 kwa ukubwa duniani na ya pili kwa ukubwa Afrika. Alieleza kuwa kutokana na ukubwa huo, nchi hiyo inaweza kuzalisha vyakula vya kulisha Afrika nzima, lakini pamoja na faida hizo nchi hiyo haijatumia vyema fursa hizo ilizonazo.

“Hii ni fursa kwetu kuitumia vyema hasa hapa Kagera, tunaweza kuuza chakula kama ndizi, mahindi, maharage. Lakini pia kutokana na ukaribu wetu na nchi hii tunaweza kuanzisha viwanda vidogo vya kuchakata madini yanayotoka Congo, tukaongeza ajira lakini pia kuingiza kipato,” alifafanua.

Alitahadharisha kuhusu hali ya usalama nchini humo katika baadhi ya maeneo, huku akisisitiza wafanyabiashara wa Tanzania ikiwemo Kagera, kujenga tabia ya kwenda katika nchi hizo za EAC kujionea wenyewe fursa zilizopo.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Ernest Mangu, alisema Rwanda ni mlango wa biashara na soko kubwa kwa Tanzania, kwani pamoja na nchi hiyo kuwa karibu na Tanzania, pia inafanya biashara na Mashariki ya Congo. Alitaja bidhaa zinazoweza kuuzwa kwa wingi nchini humo kuwa ni mchele, muhogo uliokaushwa, mboga, pilipili na bidhaa za viwandani kama saruji, nondo na chuma.

Aidha, alisema Rwanda pia wanatumia zaidi mahindi kama chakula, lakini pia kama chakula cha mifugo ambayo wao kutokana na uhaba wa ardhi, hufuga mifugo yao kisasa na hivyo kuwa na mahitaji makubwa ya chakula cha mifugo hiyo.

“Pia kuna soko kubwa la dagaa na samaki. lakini pia Tanzania inaweza kutumia fursa ya utalii wa hoteli unaotumiwa na Rwanda unaoiwezesha nchi hiyo kupata wageni wengi na hivyo kuwauzia bidhaa za chakula lakini pia kuvutia utalii,” alisema.

Alimuomba Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Marco Gaguti kutumia fursa ya uzinduzi wa hifadhi tatu za taifa za Burigi Chato, Rumanyika na Ibanda, kuzitangaza kwa nchi hizo za EAC hasa Rwanda ili kupata watalii wengi zaidi wanaotembelea nchi hizo.

Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Edmund Kitokezi alieleza kuwa pamoja na kwamba Burundi ni nchi ndogo kwa ukubwa, inazo fursa nyingi za kibiashara na uwekezaji ikiwemo nchi hiyo kupitisha takribani asilimia 95 ya mizigo yake katika bandari za Tanzania.

Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Pindi Chana na Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Aziz Mlima, kwa nyakati tofauti walieleza fursa zinazoweza kutumiwa na watanzania katika nchi hizo ikiwemo kufunguliwa kwa masoko makubwa katika maeneo ya mipakani.

“Naomba niwasilishe hili wazo, kwa sababu kwa sasa unakuta raia wa Kenya au Uganda anakwenda hadi Kahama kutafuta mchele au mahindi wakati vitu hivyo vinaweza kupatikana Kagera au Arusha. Masoko haya yatafungua fursa nyingi sana za biashara baina ya nchi hizi za Afrika Mashariki,” alisema Mlima.

Awali, akifungua mkutano huo baina ya mabalozi hao na wafanyabiashara, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Gaguti alisema mkoa huo umejipanga kuwa kitovu cha biashara baina ya Tanzania na nchi EAC, kutokana na kupakana na nchi nne na mbili kuwa karibu zaidi.

Kagera imepakana na Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya kupitia ziwa Vicoria lakini pia iko karibu zaidi na nchi za DRC na Sudan Kusini. Wiki ya Kagera ilianza jana na kesho Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kufungua kongamano la biashara na uwekezaji mkoani humo.

BODI ya Michezo ya Kubahatisha nchini kwa kushirikiana na Mamlaka ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi