loader
Picha

Waliofariki lori la mafuta wafikia 75

VIFO vya ajali ya kulipuka kwa lori la mafuta mjini Morogoro Jumamosi vimeongezeka baada ya majeruhi wengine wanne waliokimbizwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MHN) kupoteza maisha usiku wa kuamkia jana na hivyo kufanya idadi ya waliopoteza maisha kufi kia 75.

Ajali hiyo ilitokea Agosti 10, mwaka huu saa mbili na dakika 20 asubuhi baada ya lori aina ya Scania lenye namba za usajili T 717 DDF likiwa na trela namba T 645 CAN likiwa limebeba mafuta ya petroli na dizeli kupinduka.

Hospitali hiyo ilipokea majeruhi 46 kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya matibabu zaidi hata hivyo hadi sasa saba kati yao wamefariki dunia. Akizungumza na gazeti hili jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano MNH Aminiel Aligaesha alisema kwa sasa idadi ya majeruhi wanaoendelea kupatiwa matibabu ni 39.

Kuhusu hali za majeruhi Mkuu huyo wa Kitengo cha Mawasiliano alisema wanaendelea vizuri na wapo wanaoonesha matumaini. Naye Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura Muhimbili, Dk Juma Mfinanga alisema majeruhi wengi wameungua maeneo ya tumboni na mfumo wa chakula.

Wakati huo huo Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Elisha Osati amewataka watanzania kujitokeza kuchangia damu kwa ajili ya majeruhi wa ajali hiyo. Lori lingine lalipuka Songea Katika hatua nyingine lori lingine la mafuta limewaka moto katika kijiji cha Ngadinda katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma.

Ajali hiyo imehusisha lori la Kampuni ya Njombe Filling Station lenye namba za usajili T 243 BCU lenye trela namba za usajili T685 DCV lilikuwa likitokea Dar es salaam kwenda Songea mkoani Ruvuma kupeleka shehena ya mafuta. Akizungumza katika eneo la tukio Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema alisema, ajali hiyo ilitokea saa tano usiku ambapo lori hilo lilipata ajali kabla ya kuwaka moto.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa wilaya, gari hilo lilisafiri likiwa na dereva peke yake na limeungua sehemu ya kichwa na matairi yote, lakini trela lililobeba mafuta halijaungua. Hata hivyo Mkuu huyo wa wilaya alisema, mpaka sasa dereva wa lori hilo aliyefahamika kwa jina la Hubert Mpete bado hajapatikana na inasadikiwa amepoteza maisha kwa kuungua moto katika ajali hiyo.

Kwa upande wake, Meneja wa Kituo cha Njombe Filling Station Daud Mwinuka alisema, lori hilo lilitoka Njombe saa 8.30 mchana likiwa na lita 33,000 za mafuta aina ya petroli kwenda Songea.

Alisema, mara ya mwisho kufanya mawasiliano na dereva ilikuwa majira ya jioni akiwa mji mdogo wa Madaba wilayani Songea, lakini baada ya hapo hawakuwa na mawasiliano mengine hadi pale alipopta taarifa ya ajali majira ya saa 5 usiku kutoka kwa Mkuu wa wilaya Mgema. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Kamishina Msaidizi wa Polisi Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo ambapo alisema, imetokea juzi saa 4.30 usiku katika kijiji cha Hanga.

Majaliwa aahidi watu wote kutambuliwa Katika tukio lingine; Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali itahakikisha watu waliofariki dunia kwa kuungua moto katika tukio hilo wanatambuliwa na ndugu zao kupitia vinasaba ambavyo vimechukuliwa kwa miili yote.

Aliyasema hayo jana katika eneo la Makaburi ya Kola wakati wa kutoa shukrani kwa viongozi mbalimbali wakiwemo wa dini na wananchi na kuomba dua kwa marehemu katika eneo moja la makaburi.

Alisema tayari sampuli za vinasaba vya marehemu wote vimechukuliwa hivyo kwa wale ambao bado hawajatambuliwa na ndugu zao, sampuli zao zitatumika kuwatambua mara tu ndugu zao watakapojitokeza. Imeandikwa na Vicky Kimaro, Dar, Muhidin Amri, Songea, na John Nditi, Morogoro.

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ametoa maagizo ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi