loader
Picha

Tuchukue hatua kuzuia majanga

TAIFA linaendelea kuomboleza vifo vya watu zaidi ya 71 na majeruhi wengine zaidi ya 60 wa ajali kubwa ya moto, iliyotokana na kulipuka lori la mafuta ya petroli iliyotokea Morogoro, Jumamosi.

Tunaungana na Watanzania wote kuomboleza vifo vya wananchi wenzetu na kuwaombea Mwenyezi Mungu awape pumziko la milele, huku tukiwaombea uponaji wa haraka majeruhi waliolazwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Hospitali ya Taifa Muhimbili na Mloganzila.

Wakati serikali ikiendelea kusimamia maziko ya marehemu katika makaburi ya Kola, Morogoro, juzi na jana, kumetokea tukio lingine la moto ulioteketeza shamba la ngano la Chuo cha Kilimo, Uyole, Mbeya.

Ajali hiyo ni mwendelezo wa ajali kama hiyo na nyingine za magari na moto kwa nyumba za makazi na ofisi mbalimbali za taasisi, zinazotokana na visababishi mbalimbali vya ajali za moto katika maeneo hayo.

Ajali ya Morogoro imeelezwa kutokana na wananchi, kuchota mafuta ya petroli yaliyomwagika kutoka kwenye lori lililopinduka wakati dereva wake akimkwepa mwendesha bodaboda.

Ajali ya Uyole imedaiwa kusababishwa na moto, ulioanza kwa kijana aliyekuwa akivuta sigara katika eneo hilo na hivyo moto wa sigara yake kushika ngano iliyokuwa imekauka tayari kuvunwa.

Ingawa ajali haina kinga, tumelazimika kuwataka wananchi kuchukua hatua za tahadhari, kuona wengi wao hawana uelewa wa jinsi ya kujikinga na majanga, lakini wengine wakionekana kuyasababisha.

Ingawa magari yanakatiwa bima ya mali zilizobebwa na magari yenyewe, hali hiyo haipaswi kuchukuliwa na watu, kama kigezo cha kuamua kuchukua mali hizo, pale inapotokea gari imepata ajali bali kuiacha kama ilivyo.

Hatua yoyote ya kukimbilia kuchukua mali iliyo kwenye eneo la tukio kinyume cha sheria, siku zote ndio huchochea watu kugombania mali hiyo bila utaratibu na kuishia kusababisha majanga.

Kuna haja ya wananchi kuelimishwa na mamlaka husika kuhusu kujikinga na majanga kama moto inayotokea katika maeneo yao, inayosababishwa na visababishi vya ajali au kitu kingine kile.

Lakini, pia iko haja kwa wananchi wenyewe, kuchukua tahadhari binafsi kila wafanyapo kazi au kutembea, wakiepuka kuwa chanzo cha maafa kwa namna yoyote, kwa kuhakikisha hawana visababishi vya majanga.

Mfano wa hatua hizo ni wavutaji sigara na vitu vyenye asili ya moto maeneo yenye hatari ya kushika moto, kama mashamba ya ngano au mpunga au mahindi yaliyokauka kama ilivyotokea huko Uyole juzi.

Tuchukue hatua kuzuia maafa kama haya ya uzembe, yanayoleta hasara kwa Taifa. Kinga ni bora.

KATIKA gazeti la HabariLEO jana, kulikuwa na habari ya Moto ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi