loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Maonesho ya wakulima yavuke EAC

KILA mwaka Julai 31 hadi Agosti nane katika Tanzania hufanyika Maonesho ya Wakulima, maarufu Nanenane.

Maonesho hayo ya siku tisa, hufanyika katika kanda saba, lakini pia kila mkoa hufanya maonesho hayo. Katika maonesho hayo, wakulima na wafugaji hupata nafasi ya kuonesha mazao yao kwa lengo la kutafuta masoko.

Lakini, hupata nafasi ya kupata mafunzo ili kuweza kuboresha shughuli zao. Haiishii hapo, bali pia teknolojia mbalimbali za kilimo na ufugaji, huoneshwa na kufundishwa kwa lengo la kuboresha kilimo na kuongeza thamani za mazao yao.

Taasisi mbalimbali za serikali hushiriki katika maonesho hayo, kuelezea kazi zao na kutoa nafasi za washiriki kutumia huduma zao na hasa katika kusajili shughuli mbalimbali.

Hapa nchini zaidi ya asilimia 80 ya wananchi, wanategemea kilimo kama ajira yao huku serikali ikihamasisha wakulima kuanza kulima kwa tija ili kuongeza mazao yaweze kuuzwa hapa nchini na nje ya nchi. Katika kuuza nje ya nchi, kuna faida zaidi ambapo kwanza uzalishaji utaongezeka kukidhi mahitaji na pia kilimo kitaboreshwa. Bidhaa huongezwa thamani ili kuvutia soko na kuongeza ushindani kibiashara.

Katika maonesho ya wakulima, tumezoea kuona waoneshaji na waoneshwaji ni watanzania, hivyo soko linakuwa ni lilelile miaka nenda rudi.

Maonesho haya yangeweza kutanua wigo kwa kuwaalika wakazi wengine wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kwa lengo la kupanua masoko ya wazalishaji wetu.

Ikumbukwe kwamba tuna Soko la Pamoja la Afrika Mashariki lililoanza Julai mwaka 2010, ambapo nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi zilitia saini mkataba wa soko hilo.

Marais wa nchi hizo walikubaliana kuwepo kwa biashara huru na watu kuvuka kutoka nchi moja hadi nyingine, bila ya vizuizi katika eneo lote.

Naamini Tanzania kuna vitu vizuri, ambavyo huoneshwa hasa katika maonesho hayo ya wakulima, kuanzia teknolojia zinazooneshwa na wabunifu, ubora wa mazao na bidhaa zinazoongezwa thamani.

Mara nyingi wabunifu wetu, hujitahidi kubuni na kutengeneza vitu mbalimbali, lakini tatizo ni kupata soko la vitu.

Hivyo, naamini endapo washiriki kutoka nchi za EAC wataalikwa, itasaidia kuwapatia masoko.

Kuna mazao ambayo yanapatikana hapa nchini pekee, ambayo hayapatikani katika nchi nyingine ya jumuia, kwa hiyo kuwaalika kuja ni soko zuri kwao.

Kwa mujibu wa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Happiness Rugiko, mazao yanayozalishwa hapa nchini hasa mazao ya chakula kama mchele, unga na maharage, yana soko mbili.

Akizungumza katika maonesho hayo, yaliyofanyika kitaifa katika mkoa wa Simiyu wilayani Bariadi, mbunge huyo alihamasisha wakulima kulima zaidi ili waweze kupata masokokwa wingi kupitia maonesho hayo.

Katika maonesho hayo wafanyabiashara wengi kutoka nchi za EAC, watajionea wenyewe na kuingia makubaliano ya kibiashara ili kuanza kusafirisha bidhaa zao.

Natambua Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, zinajitahidi kukwamua wananchi kupunguza uduni wa mavuno yao, kukabiliana na changamoto zao na kuwaunganisha na masoko.

Lakini, mkazo unatakiwa kuwekwa katika kuwasaidia wakulima hapa nchini, kulima zaidi na pia kuwahamasisha kuachana na kilimo cha kusubiri mvua, badala yake wajikite zaidi katika kilimo cha umwagiliaji ambacho ni cha uhakika.

JIMBO Katoliki la Mpanda jana lilipata rasmi kiongozi wa kuliongoza ...

foto
Mwandishi: Regina Mpogolo

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi