loader
Picha

Vigae kulipa mabilioni ya kodi

KAMPUNI inayotengeneza vigae vya Twyford ya KEDA (Tanzania) Ceramic, imesema inatarajia kutoa kodi ya zaidi ya Sh bilioni 27.12 ifikapo 2026.

Msaidizi wa Mkurugenzi wa kampuni hiyo inayomilikiwa na raia wa China, Bruce Ni, alisema malengo hayo yanatokana na ushirikiano mzuri wanaopata kutoka serikalini.

Alisema tangu waanze uzalishaji Novemba 2017, wameshalipa kodi ya takribani Sh bilioni 22.6.

Alikuwa akitoa taarifa kwa ujumbe wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) waliotembelea kiwanda hicho mwishoni mwa wiki.

Alisema uzalishaji unaendelea vizuri na wana ushirikiano mzuri na serikali kutokana na kutembelewa na watendaji akiwamo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Bruce alisema wanashirikiana vizuri kufanyia kazi changamoto mbalimbali wanazokutana nazo. Hata hivyo, alisema uingizaji mkubwa wa vigae kutoka nje ni changamoto inayowayumbisha katika soko la ndani.

Alisema kuanzishwa kwa kiwanda hicho ni kutekeleza sera ya viwanda ya Rais John Magufuli. Kwa mujibu wa Bruce, kiwanda hicho kilichopo Chalinze, mkoani Pwani, kimewezesha ajira za moja kwa moja kwa Watanzania zaidi ya 1,000 na wasio wa moja kwa moja zaidi ya 3,000.

“Pamoja na kuwezesha ajira kiwandani, tuna hoteli na madereva kwa magari tunayotumia, tumechangia vifaa vya ujenzi kwa kliniki ya Ruvu na nyumba za wahudumu,” alisema Bruce.

Malighafi ya kuzalisha vigae kiwandani hapo asilimia 95 zinatoka nchini hususani mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Iringa na Dodoma.

Alisema mahitaji ni tani 370,000 kwa mwaka sawa na zaidi ya tani 1,000 kwa siku na wanazalisha vigae meta za mraba milioni 11 kwa mwaka.

Bruce alisema hivi sasa wanafanyakazi na zaidi ya wachimbaji wadogo 100 na wanatarajia kuongeza kutokana na mpango wa kuingia katika soko la nchi nyingi za SADC.

Kampuni hiyo inauza bidhaa zake kwa asilimia 30 katika soko la nje na nchini inauza kwa asilimia 70.

Katika nchi za SADC wana soko Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) .

Katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanauza Uganda, Rwanda na Burundi. Kiwanda hicho kilianza uzalishaji mwaka juzi kwa uwekezaji wa Dola za Marekani milioni 56. Pia wamewekeza Kenya, Senegal na Ghana.

SHIRIKA la Taifa la Biashara (ZSTC) limesema ni makosa kwa ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi