loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wahitimu vyuo vikuu kuwezeshwa ajira

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amesema Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kutengeneza fursa nyingi za ajira ili kuwezesha wahitimu wengi wa vyuo vikuu nchini na waliosoma nje kupata ajira na kutumia utaalamu walioupata kujenga taifa lao.

Aliyasema hayo wakati akizungumza kwenye mahafali ya kwanza kwa wanafunzi waliosoma nje ya nchi kupitia Kampuni ya Global Education Link yaliyofanyika Mlimani City Dar es Salaam.

Waziri Kabudi alisema serikali inaendelea kushirikiana na wadau wa sekta binafsi kuweka mazingira mazuri yatakayoongeza fursa nyingi za ajira kwa vijana wanaomaliza vyuo vya nje na ndani ya nchi.

Aliwapongeza wahitimu hao kwa kwenda kusoma nje ya nchi na kurudi na ujuzi watakaoutumia kujenga taifa lao kwenye sekta mbalimbali kama ujenzi wa miundombinu na katika sekta nyingine zilizopo.

“Serikali inaendelea kutekeleza awamu ya pili ya Mpango wa Maendeleo kwa ufanisi mkubwa. Inataka kujenga uchumi wa kati utakaoongeza nafasi nyingi za ajira kwa vijana wetu,” amesema Profesa Kabudi.

Alisema serikali imejipanga kuendelea pia kudhibiti mianya ya ufisadi ili fedha zinazopatikana zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo na kupunguza umasikini kwa Watanzania wa mijini na vijijini.

Aliipongeza Global Link Education kwa namna ambavyo imeweza kuwapeleka zaidi ya wanafunzi 5,600 kwenda kusoma vyuo vikuu nje ya nchi na kufuatilia maendeleo yao mpaka walipohitimu masomo yao.

Mkurugenzi Mkuu wa Global Link Education, Abdulmalik Mollel alisema mahafali hayo ni ya kwanza kufanyika nchini na mwaka huu pekee kampuni hiyo inatarajia kupeleka wanafunzi 1,000 kusoma nje.

Alisema mamia ya wanafunzi waliopelekwa nje kusoma wengine wamepata bahati ya kuwa wakurugenzi wa kampuni na wengine wamejiajiri na wengine wameajiriwa kwenye taasisi mbalimbali hapa nchini.

Alisema baadhi ya wahitimu hao bado wanatafuta fursa hivyo aliwaomba wawekezaji nchini kuhakikisha wanawapa kipaumbele vijana hao kwenye nafasi za ajira badala ya kuajiri wataalamu kutoka nje.

“Tuna vijana wenye ujuzi wa kutosha kwenye taaluma mbalimbali, Mheshimiwa Waziri nakuomba hili ulibebe utusaidie zinapotokea nafasi za ajira vijana wetu wapate nafasi kwani ujuzi wa kutosha wanao.

“Hawa vijana wamesoma kwao wanajua tamaduni zao wanajua kila kitu kuhusu nchi zao. Huu ni muda muafaka wawekezaji wanaokuja watoe kipaumbele kwa vijana hawa wapate ajira,” amesema Mollel.

WATOTO 84,625 waliokuwa na utapiamlo mkali, wametibiwa kuanzia mwanzoni mwa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi