loader
Picha

Uchumi, siasa vyatajwa kubadilisha fedha

FEDHA za Tanzania zimebadilishwa mara tisa tangu kuanzishwa kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mwaka 1966 kutokana na sababu za kiuchumi, kisasa na kijamii.

Akizungumza na gazeti hili wakati wa Maonesho ya Nane Nane yaliyomalizika hivi karibuni jijini Dodoma, Ofisa Mwangalizi wa Fedha Mkuu BoT, Rehema Zongo amesema fedha hizo hazibadilishwi hivihivi tu bali huwa zinabadilishwa kwa lengo maalumu kutokana na hali ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

“Fedha hizo zilibadilishwa miaka ya 1966, 1978, 1985, 1986, 1992, 1997, 2003 na 2010. Mabadiliko hayo yalitokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kiuchumi, kisiasa na kijamii,” amesema.

Fedha zilitumika wakati wa utawala wa Kiingereza na baada ya Uhuru hadi mwaka 1966 ambapo Bodi ya Fedha ya Afrika Mashariki (EACB) ilikuwa ikitoa fedha zilizokuwa zikitumika Afrika Mashariki.

Bodi hiyo ilivunjwa baada ya uamuzi wa kuanzishwa Benki Kuu za Tanzania, Kenya na Uganda. Sheria ya Benki Kuuu ya Tanzania ilipitishwa na Bunge Desemba 1965 na BoT ikaanza rasmi Juni 14, 1966.

Zongo alisema tangu kuanzishwa, BoT imetoa matoleo ya sarafu na noti ambapo mabadiliko ya mwaka 1966, fedha za kwanza zilitolewa zilikuwa na picha ya Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na upande mwingine zilionesha utamaduni, shughuli za kiuchumi na maliasili ya nchi.

“Fedha za mwaka huo, 1961 tulipopata uhuru zilikuwa za seti tano, senti 10, senti 20 na shilingi moja. Noti zilikuwa za shilingi tano, 10, 20 na 100,” alisema.

Zongo amesema toleo la mwaka 1977-1978, mabadiliko yalifanyika kwa noti za Sh 10, 20 na 100, picha ya Mwalimu Nyerere iliboreshwa na iliendelea kutumika ikiongeza maandishi ya Kiingereza na Kiswahili ya BoT na majina ya watia saini pia, Waziri wa Fedha na Gavana yaliyoandikwa kwa lugha zote mbili.

“Toleo la fedha la mwaka 1985, BoT walitoa toleo lingine jipya la noti ya shilingi 50 na ikaondolewa kwenye mzunguko noti ya shilingi 10. Noti hizi zilisababishwa na manung’uniko ya jamii kwa sababu ramani iliyokuwa nyuma ya noti haikujumuisha visiwa vya Mafia, Pemba na Zanzibar,” alisema.

Zongo alisema katika toleo la fedha la mwaka 1986, fedha mpya zilitolewa na neno Tanzania likaonekana kwenye noti hizo, lakini lilihamishiwa upande wa kushoto ili kuvipa nafasi visiwa vya Mafia, Pemba na Zanzibar ambavyo havikuwemo kwenye noti zilizotangulia kutolewa hapo awali.

“Matoleo ya 1987, BoT ilitoa toleo lingine la noti za shilingi 20,50 na kuongeza noti mpya ya shilingi 200.

Picha ya mbele ya noti ilibadilishwa na kuwekwa picha ya Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwini aliyeingia madarakani Novemba 5, 1985,” alisema.

Alisema katika toleo la fedha la mwaka 1990-1992, kulikuwa na mabadiliko ya noti kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kiuchumi.

“Noti mpya zilikuwa za viwango vya shilingi 50, 100, 200, zilitolewa mwaka 1987 isipokuwa picha ya Rais Mwinyi ilibadilishwa. Aidha BoT iliongeza aina mpya ya noti za viwango vya sh 500 na 1,000.”

“Katika toleo la 1993-1995, BoT ilitoa noti zilizokuwa sawa na zilizotangulia isipokuwa ukubwa wake ulipunguzwa na wanyama wengine wapya waliongezwa upande wa kushoto wa mbele na nyuma. Hivyo noti za shilingi 5,000 na shilingi 10,000 zilionekana katika mwonekano mpya,” alisema.

Katika toleo la mwaka 1997, baada ya kipindi cha Ali Hassan Mwinyi kumalizika Novemba 23, 1995, picha yake ilibadilishwa na michoro wa kichwa cha twiga upande wa mbele ya noti mpya hizo iliingizwa.

“Katika toleo hilo jipya, noti za shilingi 100, 200 ziliondolewa kwenye mzunguko na zikawepo za Sh 500, 1,000, 5,000 na 10,000 yenye picha ya twiga.

Upande wa kulia wa twiga huyo kuna alama maalumu zinazoparuza na kuitambulisha thamani ya noti kwa kuipapasa kwa wenye ulemavu wa macho,” alisema. Alisema katika toleo la mwaka 2000, BoT ilitoa noti ya Sh 1,000 sawa na ile iliyotangulia, lakini picha iliyokuwa upande wa mbele, ilibadilishwa kuwa ya Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa kwanza mwasisi.

“Katika toleo la mwaka 2003, BoT walitoa noti zenye viwango mchanganyiko na kuingiza noti ya kiwango kipya ya shilingi 2,000. Noti zilikuwa na jina la BoT kwa Kiswahili upande wa mbele na kwa Kiingereza upande wa nyuma, haikuwa na tarehe ya kupigwa chapa, mstari wa usalama lakini ilikuwa na uzi wa chuma unaonesha mwaka wa kuingizwa BoT (2003) kwenye mzunguko.”

Zongo alisema katika toleo la 2010, BoT ilichapisha noti mpya zenye viwango mchanganyiko, lakini zilikuwa ndogo kuliko zilizotangulia, picha ya upande wa mbele ni sura ya wanyamapori isipokuwa noti za Sh 1,000 na 500 zenye sura ya Mwalimu Nyerere na Abeid Karume, Rais wa kwanza wa Zanzibar.

Ofisa wa Idara ya Operesheni BoT mkoani Dodoma, Emmy Chamberlain alisema hakuna fedha ambayo imetolewa nchini ambayo BoT haitunzi, kila fedha ipo na inatunzwa na ndio maana wakati wa mishahara kuna senti ambazo zinatolewa kutoka Benki Kuu hiyo.

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ametoa maagizo ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi