loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tanzania yataja vipaumbele 9 SADC

TANZANIA imeainisha mambo tisa itakayosukuma kuhakikisha yanapata mafanikio katika kipindi cha uenyekiti wake wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) miongoni mwake ikiwa ni kuhakikisha Kiswahili kinakuwa lugha rasmi ya jumuiya.

Mengine ni kuendeleza harakati za kutaka jumuiya ya kimataifa iondoe vikwazo vya kiuchumi kwa Zimbabwe; kusisitiza kuongeza ajira kwa vijana, kusukuma masuala ya wanawake, watoto, jinsia na afya, wanawake na afya, Maendeleo ya Viwanda na kuongeza kasi ya biashara ya kikanda.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi aliwaambia hayo waandishi wa habari jana baada ya kukabidhiwa Uenyekiti wa Baraza la Mawaziri kutoka kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa wa Namibia, Netumbo Nandi Ndaitwah.

“Tanzania ikiwa mwenyekiti wa mkutano huo sambamba na wa wakuu wa nchi utakaofanyika Jumamosi na Jumapili, tumekuja na kauli mbiu ambayo ilichaguliwa na Rais John Magufuli na ndiyo itakayoongoza uenyejiti wa SADC katika mwaka huu mpaka mwakani Agosti,” alisema Profesa Kabudi.

Akizungumza baada ya kufunguliwa mkutano wa baraza hilo la mawaziri jijini Dar es Salaam, Profesa Kabudi alisema kauli mbiu hiyo ni ‘maendeleo shirikishi kwa ajili ya maendeleo ya viwanda endelevu kuongeza biashara ya kikanda na kuongeza ajira’.

Kuhusu Kiswahili kuwa lugha rasmi ya SADC, alisema watawasilisha suala hilo kwa nchi wanachama kwa kujenga hoja tofauti ikiwamo ya kwamba lugha hiyo ilitumika wakati wa kupigania uhuru.

“Hatuna sababu ya kusema tunaleta Kiswahili kama jambo jipya. Tunalofanya sasa ni kwamba hii ni lugha ya ukombozi waliyoitumia wakati wa kupigania uhuru, sasa iwe moja ya lugha rasmi,” alisema.

Alisema Kiswahili kinafundishwa zaidi ya vyuo 58 duniani na ni ya 10 kwa lugha zinazozungumzwa kwa wingi duniani; Hivyo Tanzania itatilia mkazo isiwe lugha ya Afrika Mashariki pekee bali iwe ya SADC na hatimaye lugha unganishi na jumuishi ya bara lote.

Alisisitiza, “taratibu itakuwa lugha ya Afrika kwa sababu hata Umoja wa Afrika (AU) unatumia Kiswahili. Kwa Afrika Kusini imeshaamua kufundisha Kiswahili katika shule za msingi na sekondari. Pia Zimbabwe hivyo hivyo.”

Profesa Kabudi alisema moja ya jitihada za kusambaza lugha katika ngazi ya kanda ameifanya Rais Magufuli wakati wa ziara aliyofanya mwaka huu Malawi Afrika Kusini , Namibia, Zimbabwe ambako kote alipelekea viongozi wa nchi kamusi ya Kiswahili .

Kwa mujibu wa Profesa Kabudi, mwenyekiti SADC (Rais Magufuli) katika hotuba zake atatumia Kiswahili lakini yeye kwa kuwa ni mwenyekiti wa kikao cha baraza la mawaziri, kabla ya hakijatoa uamuzi, atatumia lugha rasmi za jumuiya ambazo ni Kifaransa, Kireno na Kiingereza.

“Mkutano ujao Kiswahili kitakuwa lugha rasmi kutumika,” alisema.

Akizungumzia Zimbabwe, alisema imeshafanya uchaguzi wake, rais amepatikana na nchi inaendelea vizuri hivyo hakuna sababu za kuendelea kuiwekea vikwazo vya kiuchumi.

Waziri Kabudi alisema Tanzania itahakikisha nchi zote za Afrika zinakuwa na amani na utulivu kujiletea maendeleo. Alisema Tanzania itahakikisha kunakuwa na maendeleo ya viwanda endelevu na kuongeza biashara katika ukanda kwani iko chini kwa asilimia 20.

Pia itasisitiza kuongeza ajira miongoni mwa vijana. Alisema asilimia 60 ya raia katika nchi za SADC ni vijana na njia pekee ya kuwafanya kuwa na tija ni kuhakikisha wanakuwa na ajira.

Wakati huo huo alisema katika mkutano huu, suala la maombi ya Burundi kujiunga na SADC ni miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa. Akizungumza kabla ya kukabidhi madaraka kwa Profesa Kabudi, Ndaitwah alisema ajenda za SADC ni kuhakikisha inafanyia kazi changamoto zinazoikabili jumuiya hiyo kwa kuboresha mipango mkakati ya maendeleo ambayo ni RISDP na SIPO.

BEKI  wa zamani wa ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi