loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kampuni za simu kitanzini kwa kuibia wateja

NAIBU Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, (Mawasiliano), Atashasta Nditiye ametoboa siri ya kampuni za simu kwenda kinyume na bei elekezi ya serikali ya kupiga simu kwa Sh 10.40 kwa dakika moja na badala yake kutoza kwa sekunde, kinyume cha mwongozo wa watumiaji huduma na bidhaa za mawasiliano.

Kutokana na wizi huo kwa wananchi, Naibu Waziri huyo ameagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzichukulia hatua kampuni hizo mara moja. Alitoa maelekezo hayo wakati wa ziara ya Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Sira Ubwa Mamboya alipotembelea TCRA.

Dk Mamboya alifanya ziara hiyo katika mamlaka hiyo ambayo ni miongoni mwa taasisi za mawasiliano nchini ili kujifunza utendaji kazi wake kwa kuwa mawasiliano ni suala la Muungano.

Nditiye alisema, mwishoni mwa mwaka jana, serikali ilitoa bei elekezi kwa kampuni za simu za mkononi wakati wa uzinduzi wa Mwongozo wa Watumiaji wa Huduma na Bidhaa za Mawasiliano kwamba ifikapo Januari Mosi, mwaka huu, gharama za kupiga simu lazima zipungue na kuwa Sh 10,40 kwa dakika moja wala si kwa sekunde.

“Kampuni zimekuwa zikitoza tofauti wakati makubaliano yalikuwa gharama ya kupiga simu kutoka mtandao mmoja kwenda mtandao mwingine itakuwa shilingi 10.40 kwa dakika moja na si kwa sekunde kwa kuwa tulikuwa tumetoka kupiga kwa shilingi 15.60 kwa dakika moja,” alisema.

Nditiye alisema, hadi sasa anasikia matangazo kutoka kampuni za mawasiliano za simu wanajinadi kuwa kupiga simu mtandao wowote ni Sh moja kwa sekunde hiyo ina maana ukipiga sekunde 60 ni Sh 60 na inakuwa imezidi mara tano ya gharama ambayo ni mwongozo wa serikali kwa kampuni ya simu.

“Nawataka TCRA sasa waanze kufuatilia kampuni yoyote ambayo imekwenda kinyume na bei elekezi ya serikali, kwanza, wachukue hatua za kinidhamu na wawapige faini.

“Lakini pia TCRA wahakikishe fedha yetu ambayo hizo kampuni zimekuwa zikichukua isivyo halali, irudi kwa sababu mpango wa serikali ni kwamba inapofika mwaka 2022 iwe Sh mbili kwa dakika kupiga mtandao wowote wa simu.”

Nditiye pia aliipongeza TCRA kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha kuwa sekta ya mawasiliano inakuwa juu nchini, kwani sekta ya mawasiliano kupitia wadau kama TCRA kwa miaka mitatu mfululizo imekuwa ikichukua nafasi tatu za mwanzo kuchangia pato la serikali.

BEKI  wa zamani wa ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi