loader
Picha

Majaliwa kuwa mgeni rasmi wiki ya uwekezaji Kagera

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kufungua kongamano la Wiki ya Uwekezaji Kagera leo pamoja na kitabu za mwongozo wa uwekezaji mkoani humo, ambapo jumla ya wadau wa biashara na uwekezaji 300 watashiriki.

Kati ya washiriki hao magavana wa majimbo ya nchi zilizo mpakani mwaka mkoa wa Kagera kutoka Burundi, Rwanda na Uganda pamoja na wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na Rwanda wanatarajiwa kuhudhuria kongamano hilo.

Pamoja na hayo, Mkoa wa Kagera umepanga kuanzia mwezi Novemba kuanza kufanya ziara katika nchi za jirani zinazopakana na mkoa huo, Burundi, Uganda, Rwanda, Kenya na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), kwa ajili ya kuangalia fursa za kibiashara na uwekezaji katika nchi hizo.

Hayo yalielezwa mjini Bukoba jana na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti wakati akizungumzia kuanza kwa maonesho hayo juzi na maandalizi ya uzinduzi wa wiki hiyo unaofanyika leo mjini hapa.

“Maonesho yanaendelea na yameanza jana (juzi), leo (jana) tunatarajia kupokea wageni kutoka nchi zinazotuzunguka kutoka DRC, magavana kutoka Burundi, Rwanda na Uganda na wafanyabiashara kutoka Rwanda na DRC,” alisisitiza.

Mkuu huyo wa mkoa alisema jambo kubwa ni kwamba leo kutakuwa na ugeni maalumu wa Waziri Mkuu Majaliwa ambaye pamoja na kuzindua rasmi wiki hiyo ya uwekezaji Kagera pia atazindua kitabu maalumu cha mwongozo wa uwekezaji Kagera.

“Kitabu hiki kimeanisha fursa zote za uwekezaji na biashara zinazopatikana mkoani hapa. Kinatoa mwongozo wa namna ya kuwekeza na kuanzisha biashara,” alieleza Gaguti.

Akielezea mkutano wa juzi uliowakutanisha mabalozi watano wa Tanzania katika nchi za EAC, Burundi, DRC, Uganda, Kenya na Rwanda, alibainisha kuwa mkutano huo umezaa matunda mazuri kwani umehuisha maeneo yenye fursa zinazopatikana katika nchi hizo.

Alisema ndio maana kupitia mkutano huo wamekuja na maazimio ya ofisi ya mkoa kuungana na jamii ya wafanyabiashara wa Kagera kufanya ziara maalumu katika nchi hizo za EAC kujionea fursa hizo na namna ya kuzitumia. Alisema tayari wameshapanga tarehe ya kufanya ziara hiyo ambayo ni wiki ya tatu ya mwezi Novemba mwaka huu.

“Dhamira kubwa ni kwamba hatuna muda wa kupoteza, wakati ni sasa ni lazima tujikite katika kutumia masoko haya katika nchi zinazotuzunguka zenye watu takribani milioni 190,” alisisitiza.

Aidha, alieleza kuwa pia mkoa huo umejipanga kuhakikisha unakuwa kitovu cha biashara kanda ya ziwa kwa kuanzisha masoko ya mipakani ambayo bidhaa zote za Tanzania ikiwemo Kagera zitapatikana.

“Tunataka kufanya Kagera kuwa hub ya biashara katika kanda ya ziwa. Na ili tuwe hub ni lazima tuwe na masoko ya mipakani. Sisi tuna mipaka ya ardhini mitatu Burundi, Rwanda na Uganda, ukiacha huo wa majini kwenda Kenya, pia tunaweza kufikia nchi za Sudan Kusini na DRC,” alisema.

foto
Mwandishi: Halima Mlacha, Bukoba

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi