loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Viongozi Dom wapewa neno

MENEJA Msaidizi wa Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), Christopher Mangwella amewashauri viongozi wa mkoa wa Dodoma kuweka mkakati wa kupanga miji kwa kupima ardhi katika maeneo ambayo zitajengwa stesheni za reli Gulwe, Ihumwa na Kikuyu mkoani humo.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa SRG kipande cha Morogoro- Makutupora kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge, Mangwella alisema, upangaji wa miji katika maeneo hayo ni muhimu kwani maeneo hayo yatakua kimakazi, kibiashara na kwa shughuli nyingine.

Alisema maeneo kama Ihumwa ambapo itajengwa karakana za kukarabati mabehewa na treni, yanatakiwa kupangwa na kubuniwa kwa ajili ya kuanzisha ukanda wa viwanda. Mangwella alisema eneo la Ihumwa ambalo pia lipo mkabala na bandari kavu, inatakiwa kupendekezwa kuanzishwa ukanda wa viwanda ili kuvutia wawekezaji kuwekeza sehemu ambayo malighafi na bidhaa zao zitasafirishwa na kuingia kwenye viwanda vyao.

Aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuthubutu kuanzisha ujenzi wa reli hiyo ya kisasa nchini, jambo ambalo lilishindikana kufanyika katika awamu nyingine. Aidha, Mangwella alisema, SGR ikikamilika itachochea mipango mingi ya Serikali katika kutekeleza sera ya viwanda na kuifikisha nchi kwenye uchumi wa kati ifikapo 2025.

“Reli hiyo itachochea mapinduzi ya kiuchumi kwa kanda nzima ya Afrika Mashariki na Kati hususani nchi ambazo hazina bandari ambazo zitaitumia kusafirisha abiria na bidhaa zao,” alisema.

Mangwella alisema kipande cha Morogoro- Makurupora kina urefu wa kilomita 422, ambapo njia kuu ni kilomita 336 na njia ya kupishana ni kilomita 86, alisema mkandarasi yupo kazini na mradi unaendelea kwa kasi.

Alisema kipande hicho ambacho mkataba wake ulisaniwa Septemba 29, mwaka juzi na ujenzi wake kuanza Februari 26, mwaka jana, kitakamilika Februari 25, 2021, hivyo ni matarajio yao kipande cha Dar es salaam hadi Makutupora (Singida) kitakamilika Febaruri 2021.

Alisema kipande cha Morogoro-Makurupora kinachojengwa na kampuni ya Yapi Merkezi pekee, kitasaidia sana kuinua uchumi na kuboresha maisha ya wananchi wa mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida kutokana na kutoa ajira na fursa nyingine.

“Gharama za mradi katika kipande hicho ni Shilingi trilioni 4.4, wakati kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro ni Shilingi trilioni 2.7 na hivyo kufanya gharama za kipande cha Dar es Salaam hadi Makutupora kuwa shilingi trilioni 7.1.” Mangwella alisema kwa sasa mkandarasi ameshakamilisha ujenzi wa makambi katika eneo la Kilosa na Ihumwa, kambi ndogo katika eneo la Mkata na anaendelea na ujenzi wa kambi nyingine katika eneo la Gulwe wilayani Mpwapwa.

Alisema kambi kubwa zitakuwa na uwezo wa kutumiwa na watu kati ya 900 hadi 1,000 huku kambi ndogo zikiwa na uwezo wa kuhudumia watu kati ya watu 500 na 600. Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Mahenge alipongeza kwa juhudi wanazofanya lakini akawataka kuwapa kipaumbele cha ajira wakazi wa maeneo inakopita reli hiyo maadamu wana sifa zinazostahili.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Jabir Shekimweri aliwataka wenyeji wa maeneo hayo inakopita reli kutumia fursa hiyo kuandika barua kuomba kazi na kuanzisha shughuli za kusaidia wanaojenga reli kupata huduma mfano za chakula.

BEKI  wa zamani wa ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Mpwapwa

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi