loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

SADC kuanzisha mfuko wa pamoja wa maendeleo ya miundombinu

JUMUIYA ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) inatarajia kuanzisha mfuko wa pamoja wa maendeleo ya miundombinu kuongeza kasi ya kukuza uchumi kupitia viwanda na biashara kwa nchi za jumuiya hiyo.

Aidha, mfuko huo utaanzishwa kwa fedha za wanachama ili kuondoa utegemezi kutoka kwa wafadhili, ikiwa ni hatua ya kuiwezesha jumuiya hiyo kujitegemea kiuchumi katika kutekeleza miundombinu.

Mkurugenzi wa Miundombinu na Huduma katika Sekretarieti ya SADC, Mapolao Mokoena, aliwaambia waandishi wa habari jana Dar es Salaam kuwa, hatua za kuanzishwa kwa mfuko huo zinaendelea vizuri.

Alisema kanuni zinataka nchi 11 ziridhie ili uweze kuanza na tayari nchi nane zimekubali na kuridhia na ikifika idadi inayopaswa kwa mujibu wa miongozo, mfuko huo utaanza.

“Nchi wanachama wanasema imetosha. Tuna mengi ya kufanya kwa pamoja. Ni wazi kutegemea fedha za wafadhili kunatuchelewesha, uamuzi ni kwamba tutumie fedha zetu za ndani za wanachama kuanzisha mfuko wa pamoja wa jumuiya ili tuzidi kusukuma mbele uchumi,” alisema Mokoena kutoa Lesotho.

Alisema jumuiya hiyo imekuwa ikipata ufadhili kupitia Mfuko wa Kuwezesha Uandaaji wa Miradi wa SADC (SADC-PPDF) na kuzijengea uwezo nchi wanachama kwa kuzipa ruzuku za kuandaa miradi na kutekeleza miradi inayounganisha jumuiya hiyo kimiundombinu na kwamba pamoja na ufadhili huo, SADC inapaswa kujitegemea kifedha.

Kwa mujibu wa Mokoena, hadi mwishoni mwa mwaka jana PPDF kwa ufadhili iliidhinisha jumla ya dola za Marekani milioni 19.6 kwa maandalizi ya miradi tisa ya kikanda inayohusu nishati, usafirishaji na maji inayokadiriwa kutengeneza dola za Marekani bilioni 5.8 kwenye uwekezaji wa miundombinu.

Miradi hiyo tisa inayotekelezwa ni wa umeme kati ya Msumbiji, Zimbabwe na Afrika Kusini (MoZiSa); awamu ya pili ya mradi wa Alaska- Sherwood wa kv 400 wa Zimbabwe na Mradi wa Umeme wa Pamoja Kusini mwa Afrika (SAPP); na mradi wa barabara wa Kasomeno-Mwenda kati ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Zambia.

Mradi mingine ni maboresho ya Ushoroba wa Reli ya Kaskazini-Kusini inayounganisha Botswana, DRC, Afrika Kusini, Zambia na Zimbabwe; mradi wa umeme wa Luapula (DRC na Zambia); wa Angola na Namibia; wa Mulembo(Zambia, DRC na SAPP) wa wanachama wote wa Afrika Green na wa Mauritius.

Mokoena aliyekuwa akizungumzia namna SADC inavyotekeleza masuala ya miundombinu na huduma chini ya Mpango kazi wake wa Maendeleo ya Miundombinu wa mwaka 2012-2027 kwa waandishi wa habari, pamoja na kwamba hakueleza hasa lini mfuko huo utaanza, alisema utekelezaji wa kuanzishwa kwake ni sehemu ya mambo muhimu katika mpango kazi huo

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi