loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ndayiragije: Tuko tayari kuivaa Simba

KOCHA Mkuu wa Azam FC, Ettiene Ndayiragije amesema wako tayari kuwakabili Simba katika mchezo wa ngao ya jamii mwishoni mwa wiki hii akiamini utakuwa wenye ushindani kwa sababu timu zote zinawakilisha kimataifa.

Azam FC tayari imewasili Dar es Salaam ikitokea Ethiopia ilipopoteza kwa bao 1-0 mchezo wa awali wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Fasil Kenema ya huko.

Akizungumzia mchezo huo katika taarifa yake iliyotumwa na msemaji wao, Jaffar Maganga, Ndayiragije alisema wanahitaji kucheza kwa nidhamu kubwa kutokana na kuwa na jukumu kubwa la kujipanga na mchezo wa marudiano dhidi ya Waethiopia.

“Mchezo wetu dhidi ya Simba ni mchezo mzuri kwa sababu timu zote zinawakilisha nchi, kutakuwa na ushindani wa hali ya juu, tunahitaji kuwa na nidhamu hasa ikitegemewa kuwa kuna mchezo wa kimataifa mbele yetu,”alisema.

Ndayiragije alisema anakiamini kikosi chake kitafanya vizuri katika mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi na kuwahimiza mashabiki wajitokeze kwa wingi kupata burudani nzuri.

Simba inawakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ilicheza mechi yake ya kwanza ugenini dhidi ya UD Song ya Msumbiji na kutoka nayo suluhu ambapo mchezo wa marudiano ni Agosti 25.

Akizungumzia kikosi chake, Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema wachezaji wake walifanya mazoezi jana asubuhi na jioni walitarajiwa kuingia kambini Mbweni.

Mara ya mwisho Simba na Azam zilikutana kwenye Ligi Kuu msimu uliopita ambapo mechi ya kwanza Simba ilishinda mabao 3-1 na mechi ya pili zilitoka suluhu.

Mechi ya ngao ya jamii msimu uliopita Simba ilicheza na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi