loader
Picha

Taasisi zinazomiliki malikale zatakiwa kuzitunza

WIZARA ya Maliasili na Utalii imeziagiza taasisi zote zinazomiliki malikale ikiwemo majengo, kuhakikisha zinazitunza na kuzifanyia ukarabati ili ziwe endelevu kwa vizazi vya sasa na baadaye, kwa ajili ya kulinda utamaduni wa Mtanzania.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda, alipokuwa mjini Morogoro hivi karibuni wakati akizungumza na baadhi ya viongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) pamoja la Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).

Profesa Mkenda alisema, malikale zilizopo ni za kutosha na kwamba nia ya kuzitoa kwenye taasisi hizo ni kwa ajili ya kutunza na kubaki kama zilivyo ikiwa ni pamoja na kujenga mazingira rafiki zaidi ya watu kutembelea.

Kwa mujibu wa Mkenda, taasisi ya TFS imekabidhiwa Bagamoyo na Kaole pia michoro ya miambani ya Kondoa na kwa kufanya hivyo itatenga bajeti kwa ajili ya kuendeleza malikale hizo.

Alisema malikale hizo zitabakia kuwa chini ya uangalizi wa Mkurugenzi wa malikale na Shirika la Makumbusho la Taifa, na utaalamu wa kutunza utabaki kwa idara ya malikale, kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, alisema kwenye utawala na fedha imekabidhiwa TFS na imefanyika hivyo kwenye maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Butiama, nyumbani kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambayo imekabidhiwa kwa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA).

“Mageuzi yaliyofanyika yanatoa fursa kutumia rasilimali fedha kutoka kwenye taasisi zake kubwa ili kujenga mazingira rafiki zaidi ya kuvutia, na lengo kubwa ni kuwafikia wananchi waweze kuona na kujua na kujivunia.

“Hii ni kuona fahari kuwa Tanzania ndio chimbuko la binadamu wa kwanza na hata watu wa zamani waliweza kuchora picha nzuri hivyo lazima maeneo hayo yatengenezwe vyema na huo ni uwekezaji na kumbukumbu kwa watoto ikiwa ni pamoja na kuvutia watalii ili kupatikana kwa fedha,” alisema.

Meneja Msaidizi anayesimamia rasilimali za misitu wa TFS, Bernadetha Kadala alisema kuwa watahakikisha wanatumia teknolojia za kisasa kuwafika wananchi ili waweze kupata elimu ya kutambua umuhimu wa utunzaji wa maliasili zetu kwa faida ya sasa na kizazi kijacho.

foto
Mwandishi: John Nditi, Morogoro

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi