loader
Picha

SADC itokako na iendako sasa

HISTORIA ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) inaturudisha nyuma hadi miaka ya 60 na 70 wakati viongozi wa nchi huru za Kiafrika na vyama vya ukombozi waliposhirikiana katika masuala ya kisiasa, kidiplomasia na kiukombozi.

Lengo lao lilikuwa kupiga vita utawala wa kikaburu katika nchi za Kiafrika kama vile Afrika Kusini, Zimbabwe, Msumbiji, Angola na Namibia.

Harakati hizi ziliongozwa na nchi zilizo msitari wa mbele zikiongozwa na Tanzania chini ya Rais wake, Mwalimu Julius K. Nyerere. Ndiyo maana, vyama vya ukombozi kutoka nchi hizo vilifungua ofisi zao Tanzania na zikaendesha mafunzo ya kijeshi kwa makada wao katika kambi zilizokuwa Tanzania.

Kimsingi, nchi za msitari wa mbele zilikuwa Angola, Botswana, Msumbiji, Tanzania, Zambia, Afrika Kusini, Namibia (wakati ule South West Africa) na Zimbabwe (wakati ule ikiitwa Rhodesia).

Umoja wa nchi za msitari wa mbele ulikuwa ni jukwaa la kuratibu harakati za mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na utawala wa Wazungu wachache waliokuwa wakitawala Kusini mwa Afrika.

Vita ya ukombozi ilifanikiwa kuung’oa utawala wa makaburu na Angola, Msumbiji, Namibia na Afrika Kusini zikawa nchi huru. Mwaka 1994, uchaguzi wa kwanza ulio huru na wazi ukafanyika nchini Afrika Kusini na Mzee Nelson Mandela akachaguliwa rais wa nchi hiyo iliyojikomboa.

Ndipo kazi ya kikundi cha nchi za msitari wa mbele ikamalizika na kuanzia hapo, viongozi wa Kusini mwa Afrika wakaona kuwa baada ya kuleta ukombozi wa kisiasa sasa kazi inaayowakabili ni ukombozi wa kiuchumi na kijamii Wakaamua kuunda jukwaa la kuratibu harakati za maendeleo au SADCC (Southern African Development Coordination Conference).

Hii ilitokana na mkutano wa nchi tisa zilizokutana mjini Lusaka (Zambia) tarehe 1 Aprili 1980 na kupitisha azimio la Lusaka lililopelekea kuzinduliwa kwa SADCC.

Nchi zenyewe ni Angola, Botswana, Lesotho, Malawi, Msumbiji, Swaziland, Tanzania, Zambia, Zimbabwe. Kundi la nchi za mstari wa mbele likajizatiti zaidi kwa kuanzisha jukwaa la kuratibu harakati hizo (SADCC), hususan katika kujenga uwezo wa kujitegemea kiuchumi.

Hii iliendelea hadi Agosti17,1992 SADCC ilipogeuka na kuwa SADC yaani Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika. Namibia nayo ikajinyakulia uhuru na ikajiunga na SADC. Tofauti na SADCC, lengo la SADC likawa ni kuleta maendeleo ya kiuchumi, ustawi wa jamii na ushirikiano wa kisiasa na kiusalama.

Agosti 2008, SADC ikaazisha eneo la biashara huru likiwa na nchi 13. Baada ya miezi miwili yaani Oktoba, 2008, SADC ikaungana na Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili kuunda eneo la biashara huru barani Afrika.

Nchi 26 kutoka jumuiya tatu zikajiunga katika eneo hili likiwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa za Dola bilioni 624. Nia ilikuwa kuepukana na migongano ya kibiashara miongoni mwa nchi za Afrika zikiwa katika jumuiya za kikanda tofauti.

SADC imekuwa ikishughulika katika nyanja mbali mbali kama vile biashara, usafirishaji, fedha, utalii, nishati, kupambana na maafa, utunzaji wa vyanzo vya maji, utunzaji wa amani na ushirikiano wa kisiasa.

Mfano mmoja ni kuhusu malori ya kusafirisha bidhaa. Hapo zamani, lori kama hilo lilipovuka mpaka wa Zambia na Zimbabwe ilichukua takriban siku sita ili kukaguliwa na kutimiza masharti ya kirasimu.

Na kila siku lori linapolala hapo mpakani inagharimu Dola 300. Leo hii inachukua siku moja tu. Matokeo yake, gharama za usafirishaji na muda wa usafirishaji unapungua.

Hii ni kutokana na ujenzi wa kituo cha pamoja kwenye mipaka. Sera ya SADC ni kuwa na vituo kama hivi katika mipaka ya nchi zote wanachama.

Mafanikio kama haya yanaonekana siyo katika nchi za SADC, bali hata nje ya Kanda ya SADC. Mei 30, mwaka huu, nchi za Kiafrika zimepitisha makubaliano ya biashara ya pamoja kwa bara zima la Afrika (AfCFTA).

Hii ni baada ya nchi 25 za Umoja wa Afrika (AU) kuridhia makubaliano hayo. Julai 7, 2019 AfCFTA ikazinduliwa wakati wa mkutano wa kilele wa AU uliofanyika nchini Niger.

Utekelezaji wake unategemea kuanza Julai mwakani. Hii inaenda sambamba na lengo la SADC la bidhaa kuvuka mipaka bila vikwazo vya forodha au ushuru.

Lengo kuu ni kupanua biashara miongoni mwa nchi za Kiafrika wakati Waafrika nao watakuwa na pasipoti mpya ya bara zima. Yaani watakuwa wakivuka mipaka bila ya urasimu.

Wakati huohuo, Machi mwaka huu Baraza la Mawaziri wa SADC liliunda kikosi kazi ili kufanya mipango ya kugeuza jukwaa la wabunge wa SADC liwe bunge la SADC.

Wachunguzi wanasema kwa hili, ni vizuri jukwaa la wabunge wa SADC lijifunze kutoka mafanikio ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA).

Ukweli ni kuwa, kila nchi mwanachama wa SADC inakabiliwa na kiasi fulani cha changamoto katika masuala mbalimbali kuanzia masuala ya kiuchumi, kibiashara, kielimu, kiafya hadi kidiplomasia, kiusalama, kijeshi na kisiasa.

Inawezekana nchi moja ikakabiliwa na ugonjwa wa ebola au magonjwa ya mifugo au nafaka. Nchi nyingine inawezekana ina makundi ya uhalifu au ugaidi.

Nchi nyingine inaweza ikapigwa na kimbunga au ukame au mafuriko. Matatizo kama haya hayawezi kuwa ya nchi moja peke yake, bali kwa kawaida huvuka mipaka na kuhusisha nchi za jirani.

Ndipo kuna umuhimu wa jumuiya ya kikanda kama SADC. Nchi mbili zikiwa na viwango tofauti vya bidhaa au ushuru tofauti inakuwa vigumu kwa nchi hizo kuwa na uhusiano mzuri wa kibiashara.

Hali kadhalika, nchi moja ikiachwa nyuma katika maendeleo ya miundombinu kama barabara au reli au bandari nchi za jirani zinahusika. Hii ni kwa sababu bandari au reli ya nchi moja huwa inasaidia nchi za jirani.

Ndiyo maana Bandari ya Dar es Salaam inasaidia nchi kama Uganda, Zambia, Malawi, Rwanda, Burundi na DRC. Hali kadhalika Bandari ya Beira (Msumbiji).

Ndipo jumuiya kama SADC inakuwa muhimu sana kwa maendeleo na ustawi wa nchi wanachama. Wakati huohuo, kuna changamoto ya nchi moja ya SADC kuwa wakati huohuo mwanachama wa jumuiya nyigine ya kikanda.

Inawezekana jumuiya hizo zikawa na vipaumbele au viwango tofauti. Kwa mfano, Afrika Kusini, Namibia na Botswana ni wanachama wa Umoja wa Forodha wa Kusini mwa Afrika (Southern Africa Customs Union - SACU ).

Zambia na Zimbabwe ni wanachama wa Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (Common Market for Eastern and Southern Africa –COMESA).

Tanzania nayo ni mwanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Wakati huohuo nchi zote hizi ni wanachama wa SADC. Bado kuna jumuiya nyingine za kikanda kama ECOWAS, IGAD na CENSAD.

Ndiyo maana kuna haja ya jumuiya hizi za kikanda barani Afrika kuratibu kazi zao ili zisigongane. Hii hufanyika kila mwaka wakati wa mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika (AU).

Wakati huo, hufanyika mkutano maalum unaowakusanya watendaji wakuu wa jumuiya za kikanda pamoja na wasaidizi wao kama wakurugenzi na makamishna.

Wakuu hawa hubadilishana mawazo kuhusu jinsi ya kushirikiana na kusaidiana. Changamoto nyingine inayowakabili viongozi wa SADC, ni kuhusu mahakama ya jumuiya hiyo (SADC Tribunal) ambayo hivi sasa imesitisha kazi zake.

Mahakama hii ilianzishwa mwaka 1992 kwa mujibu wa Kifungu cha 4 cha Katiba ya SADC. Ina jukumu la kusikiliza kesi na malalamiko kutoka serikali za nchi wanachama na raia wa nchi hizo.

Makao yake makuu yako Windhoek (Namibia). Majaji waliteuliwa na kuapishwa mwaka 2005, lakini ilipofika mwaka 2012 Mahakama hiyo ikasitishwa. Mahakama Kuu ya Afrika Kusini ilitoa uamuzi kuwa, usitishwaji huo ni kinyume cha Katiba ya SADC.

Kuna matumaini kuwa, Mahakama hiyo itahuishwa ili iweze kutimiza majukumu ya SADC. Ni vizuri tukajifunza kutoka mfano wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Magharibi (ECOWAS Community Court of Justice) inayofanya kazi kama ilivyokusudiwa.

WATOTO yatima na wanaoishi kwenye mazingira wa magumu wa shule ...

foto
Mwandishi: Nizar Visram, Dar es Salaam

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi