loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wafanyakazi 257 hotelini kupunguzwa

KAMPUNI ya kitalii ya Impala Group inayoendesha Hoteli ya Impala na Naura Springs jijini hapa, inatarajia kupunguza wafanyakazi 257 kwa madai ya kutaka kuboresha huduma zake na kumudu ushindani katika hoteli za kitalii jijini humo.

Kwa mujibu wa dokezo la Agosti 9, mwaka huu, lililotolewa na uongozi wa kampuni hiyo kwenda kwa wafanyakazi, hoteli hizo pacha zimeshindwa kujiendesha kutokana na mabadiliko ya kiuchumi, hivyo kuamua kupunguza wafanyakazi, kama njia mojawapo ya kujiboresha na kuleta ufanisi.

Meneja Rasilimali Watu katika Hoteli ya Impala, Vivian Mollel amethibitisha kuwa hoteli hizo, zipo katika hatua ya kupunguza wafanyakazi wake kuanzia sasa, baada ya kufanyika upembuzi yakinifu kwa kuzingatia vigezo muhimu vitakavyotakiwa.

Vivian amesema ofisini kwake kuwa, upunguzaji huo utakwenda sanjari na uboreshaji wa huduma katika hoteli hizo ili kuendana na uwekezaji wenye tija, utakaomudu ushindani katika sekta ya hoteli za kitalii nchini.

Mmoja wa viongozi wa hoteli hiyo, Joram Lemanya amesema hoteli hizo zimekumbwa na wafanyakazi hewa, ambao wamekuwa wakilipwa mshahara bila kuwepo kazini, hivyo kusababisha kuingia hasara na kushindwa kujiendesha kwa faida.

Katika hatua nyingine, Lemanya alithibitisha kusimamishwa kazi kwa Meneja wa siku nyingi wa Hoteli ya Naura, Beatrice Dallaris kutokana na sababu mbalimbali ambazo bado zinafanyiwa uchunguzi.

Lemanya alisema kuwa Beatrice amesimamishwa kazi na hajafukuzwa kutokana na tuhuma mbalimbali ili kupisha uchunguzi na kwamba ataendelea kulipwa mshahara hadi hapo itakapothibitika kuhusika na tuhuma hizo, ambazo hakupenda kuziweka bayana.

Wakati huo huo, Lemanya amekanusha taarifa kuwa hoteli hizo za Impala na Naura zimefilisika, kiasi cha kushindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi wake, akidai kuwa taarifa hizo hazina ukweli, japo alikiri kuwepo changamoto za ucheleweshaji wa mishahara, unaotokana na hali ya kibiashara.

Hata hivyo, aliwahakikishia wateja wake kwamba uongozi wa hoteli hizo zilizoachwa na marehemu Melau Mrema, aliyefariki dunia mwaka 2017, zitaendelea kusimama kama ilivyokuwa mwanzo.

“Hoteli yetu haijafilisika, tupo katika hatua ya kuboresha huduma zetu na maboresho hayo ni pamoja na kuwaondoa wafanyakazi walioshindwa kutuvusha,” alisema Lemanya.

BEKI  wa zamani wa ...

foto
Mwandishi: John Mhala, Arusha

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi