loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Watanzania changamkieni fursa SADC

NIMEPATA tena fursa ya kuendelea na makala zangu kwa ‘Maslahi ya Taifa’.

Leo natoa angalizo kwamba kufuatia kazi kubwa na nzuri ya uhamasishaji wa mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), tusiishie kuchangamkia mkutano pekee bali fursa za soko la SADC ambalo ndilo jambo muhimu zaidi.

Mimi ni mmoja wa waandishi wa habari tuliohudhuria mkutano wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi alipozungumza na wamiliki na wakuu wa vyombo vya habari nchini katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere.

Profesa Kabudi aliwaeleza wamiliki na wakuu hao wa vyombo vya habari kuhusu Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa SADC unaofanyika nchini mwetu wakati huu.

Profesa Kabudi aliwasihi wakuu hao kushirikiana na Serikali hususani katika kuelimisha umma juu ya SADC pamoja na kutoa elimu kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kuhusu fursa za mkutano huo na zile zinazopatikana katika nchi wanachama wa SADC.

Nilipopata fursa ya kuzungumza katika mkutano huo, nilisema Watanzania ni wazungumzaji wazuri wa mipango na mkakati, lakini ikija kwenye utekelezaji, bado hatujajenga mifumo wezeshi, yaani kuwawezesha Watanzania kuchangamkia fursa nyingikiuchumi.

Nikatolea mfano wa Wizara yake ya Mambo ya Nje kwamba katika sera yetu ya nje, ingawa tumeazimia kutekeleza diplomasia ya uchumi, lakini hatujabadili muundo na mfumo wa balozi zetu ili kuitekeleza vyema sera hii.

Nikasema ni vyema sasa balozi zetu ziwe na mwambata wa uchumi ili kuendana na sera hiyo ya diplomasia ya uchumi na hivyo kuwawezesha Watanzania kuchangamkia fursa za kiuchumi. Watanzania wanapaswa wawe ndio madereva wa uchumi kwa kuzifikisha bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa.

Hoja yangu kuu katika muktadha huu ni kwanza kutoa pongezi kwa kazi kubwa na kazi nzuri inayofanywa kuhamasisha mkutano huu wa SADC ambao umerudi tena kufanyika nchini Tanzania baada ya miaka 16. Kiukweli uhamasishaji ni mkubwa na Watanzania tumehamasika vyema, na kila kanda imejipanga kuchangamkia fursa za mkutano huu. Sisemi ni kosa kujipanga vyema kwa ajili ya mkutano lakini la muhimu zaidi ni kujiuliza tunachangamkia vipi fursa za soko la SADC lenye watu takribani milioni 350?

Pia ninapenda nitoe angalizo kwa viongozi wetu kwamba katika kuwapatia wafanyabiashara fursa kupitia mkutano huu wasiwe na mategemeo na matazamio makubwa sana (too much expectations) kiasi cha kuwafaya wengine wakakopa kwa kutegemea kwamba pesa zitarudi wakati wa mkutano. Ingawa nimechelewa kidogo kulisema hili lakini ni vyema nikalisema.

Hili nililishuhudia kwenye mkutano wa Sullivan. Ulikuwa ni mkutano wa fursa pia kama huu na wakazi wa Arusha wakajitoa kwelikweli, lakini mwisho wa siku kuna wafanyabiashara waliishia kujuta. Na kwa kweli sikubahatika kupata mrejesho ni fursa zipi za Sullivan, Tanzania tuliendekea kunufaika nazo baada ya mkutano ule.

Ninachotaka kuzungumza leo hasa kinaanza namna hii. Nilipata bahati ya kuwemo kwenye kundi la waandishi wa habari wa Tanzania, waliopelekwa nchini Marekani kuelimishwa kuhusu fursa za Mkataba unaotoa Fursa za Biashara kwa Afrika katika soko la Marekani (AGOA).

Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID) liligharimia viongozi wa wizara ya Viwanda na Biashara na viongozi wa Bodi ya Biashara ya Kimataifa (BET) (sasa TanTrade) kwenda Marekani kuonyeshwa bidhaa zinazotakiwa ili kuchangamkia fursa za soko la AGOA.

Wengine waliopata bahati hiyo ya kwenda Marekani ni viongozi wa vyama vya wafanyabiashara kupitia Chama cha Wafanyabiashara, wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA), Chama cha Wenye Viwanda (CTI) na kundi kubwa la wafanyabiashara zaidi ya 100.

Kule tulionyeshwa soko la Marekani linataka bidhaa gani, zenye ubora gani, viwango gani, ufungashaji gani na taratibu za kufuata. Soko hilo ni kubwa na linahitaji bidhaa nyingi za kila aina zaidi ya 1,000 kutoka Tanzania zikiwemo bidhaa za kiutamaduni, vinyago, mapambo na maua.

Wamarekani wakafanya vivyo hivyo kwa Kenya, Uganda, Ghana, Rwanda na Burundi na nchi mbalimbali. Wafanyabishara wa Tanzania wakahamasika sana na waliporejea nyumbani Tanzania, maombi ya kupeleka bidhaa Marekani yakaanza kumiminika.

Kuna kikundi cha akinamama wasuka mikeka ya majani, wakapewa ombi la kupeleka kontena la futi 40 la mikeka inayosukwa na akinamama wa vijijini katika mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara.

Akinamama wale na kikundi chao, walitembea na hilo ombi (offer) la upelekaji bidhaa Marekani wakitafuta mtaji wa kulitekeleza hadi muda wa siku 90 waliopewa ukaisha.

Kanuni zilikuwa kwamba ukishindwa kutekeleza ombi hilo ndani ya siku 90 basi unakuwa umeshindwa na nafasi hiyo anapewa mtu au nchi nyingine yenye uwezo wa kulitekeleza.

Inaelezwa kwamba Watanzania waliposhindwa makampuni ya jirani zetu hapo Kenya, walikuja nchini, wakaenda Pwani, Lindi na Mtwara wakawalipa wale akina mama na kununua mikeka yote kwa bei ya karibu na bure na kuisafirisha hadi Nairobi, kisha wakaipakia kwenye makontena na kuifikisha sokoni Marekani.

Ingawa mikeka hiyo asili yake ni Tanzania, lakini iliingizwa sokoni na Wakenya ambao ndio walionekana wazalishaji na ndio walionufaika zaidi huku Watanzania tukiwa tumelala.

Na hivi ndivyo inavyofanyika kwa vinyago vyetu, maparachichi yetu, madini yetu na kadhalika. Inaelezwa kwamba katika awamu ya kwanza ya kipindi cha miaka 10 ya Agoa, Tanzania tulishindwa kutumia kikamilifu fursa hiyo ya kupeleka bidhaa zetu Marekani huku jirani zetu wakijivinjari kwa kuzinunua bidhaa zetu na wao kuzifikisha sokoni na kupata faida maradufu huku takwimu zikionesha wao wanafanya vyema katika soko hilo kulinganisha na sisi.

Agoa imeongeza miaka 10 mingine, na bado sisi Tanzania unufaikaji wetu na soko hilo ni mdogo sana wakati taarifa zinaonesha kwamba bidhaa nyingi zinazowabeba majirani zetu kwenye soko hilo zinatoka Tanzania. Katika soko la Afrika Mashariki, Tanzania ndio nchi inayoongoza kwa fursa nyingi.

Ndio nchi inayoongoza kwa utajiri wa kila kitu, kuanzia vivutio vya utalii, maliasili, madini, vyanzo vya maji, ardhi ya kutosha kwa kilimo, udongo wenye rutuba, na sasa tuna gesi asilia lakini baadhi ya wenzetu wanaonekana kama wako juu katika biashara kuliko sisi.

Tanzania tunapakana na nchi nane, kati ya hizo, nchi sita ni nchi zisizopakana na bahari hivyo sekta tu ya usafiri na usafirishaji ingeweza kututoa kimasomaso toka kwenye lindi hili la umasikini uliotopea.

Kufuatia Tanzania kuwa na bandari ya Dar es Salaam, Kariakoo ilikuwa kitovu cha biashara ya bidhaa kwa nchi za Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, Malawi na DR Kongo, lakini sasa, mzigo unashukia bandari ya Dar, unasafirishwa kwenda Uganda, halafu wafanyabishara wa nchi hizo sasa wananunulia Uganda!

Hivyo Tanzania tuna kila sababu ya kuwa ni nchi tajiri sana kwa kuchangamkia tu fursa, lakini hali si hivyo, bado tunaendelea na umasikini. Ukijiuliza kwa nini Tanzania ni masikini, huwezi kupata jibu sahihi. Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere aliwahi kusema: “umasikini mkubwa na umasikini mbaya zaidi ni umasikini wa fikra”.

Fikra ni kama kauli kwani huumba.

Ukijifikiria kuwa wewe ni masikini, unakuwa masikini kweli, ndio maana msimamo wa Rais John Magufuli na kauli yake kuwa Tanzania sio masikini bali ni nchi tajiri na tunakwenda kuwa nchi ya kutoa misaada kwa wengine (a donor country) ni msimamo mzuri sana.

Watu wote wenye mapenzi mema na nchi yetu Tanzania, tunapaswa kuunga mkono msimamo huu na tuache kujiita masikini ili tusiendelee kujiumbia umasikini, tuanze kujiita Tanzania ni nchi tajiri huku tukichangamkia fursa zinazotuzunguka ili kujiumbia utajiri.

Kama tulivyotumia nguvu kubwa kuhamasisha ushiriki wetu katika mkutano wa SADC, tutumie nguvu hiyo hiyo katika kuhamasisha watanzania kuchangamkia soko la SADC. Uhamasishaji huo utakuwa na manufaa ya muda mrefu zaidi baada ya mkutano kumalizika.

Kinachofanya jirani zetu Wakenya, watushinde kwenye kuchangamkia fursa ni serikali yao kuingiza mkono wake kusaidia, hivyo sasa serikali ya awamu ya tano imeshaonesha njia, kwanza kwa Rais Magufuli kukaa na wafanyabiashara na kusikiliza kero zao ikiwemo kuchukua hatua za papo kwa papo.

Bila mkono wa serikali katika kuweka mazingira wezeshi, wafanyabiashara wenyewe tu kama wafanyabiashara, hawataweza kuliteka soko kubwa na muhimu la SADC. Nawatakia Mkutano Mwema wa SADC.

Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili anayepatikana kupitia simu 0754 270403 au pascomayalla@ gmail.com

HUDUMA bora za afya ya msingi zinapunguza uhitaji, gharama na ...

foto
Mwandishi: Pascal Mayalla

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi