loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kagera ilivyojipanga kutumia uvuvi kiuchumi

ZIWA Victoria, ni ziwa la kwanza kwa ukubwa Afrika na la pili duniani baada ya ziwa Superior ambalo lipo Amerika ya Kaskazini. Lina ukubwa wa kilometa za mraba 69,484.

Ziwa hilo ambalo liko Tanzania, Uganda na kwenye mpaka wa Kenya, kijiografia linapitiwa na msitari wa ikweta katika eneo lake la kaskazini na pia lipo katikati ya sehemu ya mashariki na magharibi mwa Bonde Kuu la Ufa.

Eneo la maji ya ziwa limegawanywa ambapo Tanzania ina eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 33,700, Uganda kilometa za mraba 31,000 na Kenya kilometa za mraba 4,100.

Ziwa Victoria lina zaidi ya aina za samaki 400, na baadhi ya samaki hao hawapatikani mahali pengine popote ulimwenguni.

Ziwa hilo lina aina aina 13 za samaki ambao ni pamoja na sato, sangara, ngege, mbiru, furu, ningu, kuyu, mbofu au hongwe, domodomo au mbete, soga, gogogo, kambale mumi, kambale mamba au kamongo na dagaa. Sangara ndio samaki wakubwa zaidi ambao huweza kufika hadi kilo zaidi ya 100.

Nchini Tanzania ziwa hilo linapita katika mikoa ya Mara, Geita, Simiyu, Mwanza na Kagera ambayo kwa sasa inaongoza kwa biashara ya uvuvi wa samaki wa maji baridi nchini hasa wale maarufu kama sato na sangara.

Mkoa wa Kagera ni moja ya mikoa inayonufaika kwa namna moja au nyingine na ziwa hilo kupitia uvuvi lakini pia mkoa huo una maziwa takribani 15 madogo yanayotumika katika kukuza shughuli za uvuvi.

Unapoingia mkoani Kagera upande wa ziwa hilo, utakaribishwa na mandhari nzuri ya ziwa hilo lenye maji yanayong’aa kama kioo kikubwa chenye kumetameta.

Halmashauri za wilaya zilizo karibu na ziwa Victoria mkoani Kagera ni pamoja na Manispaa ya Bukoba, Bukoba Vijijini, Muleba na Biharamulo ambazo zote pamoja na kilimo wakazi wake wanajishughulisha na uvuvi.

Pamoja na halmashauri hizo kuendesha shughuli za uvuvi kutokana na kupitiwa na Ziwa Victoria, Kagera pia imebarikiwa kuwa na maeneo mengi yenye maji ikiwemo mito kama mto Ngono, Mto Kagera na Mto Ruvuvu ambayo yote inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuchochea shughuli za uvuvi.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Marco Gaguti anasema kati ya fursa nyingi ambazo mkoa huo umebarikiwa kuwa nazo ni pamoja na fursa ya uvuvi kupitia ziwa hilo. Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Bernard Limbe anasema katika manispaa hiyo wakazi wake pamoja na kujishughulisha na kilimo, uvuvi ndio shughuli yao kubwa inayowapatia mapato lakini pia chakula.

Anaeleza kuwa eneo kubwa la manispaa ya Bukoba linapakana na Ziwa Victoria linalotoa samaki wa kila aina hususani sato, dagaa na sangara.

Hata hivyo, anaeleza kuwa bado biashara ya samaki haijawa kubwa kutokana na uhaba wa viwanda vya kuchakata mazao ya samaki ambapo kwa sasa kipo kiwanda kimoja tu cha kusindika minofu.

“Ipo fursa nzuri tu ya uwekezaji na tumetenga eneo jirani kabisa na ziwa lenye ukubwa wa mita za mraba 400 kwa ajili ya viwanda vya kusindika mazao ya samaki pekee, kwa sasa samaki wengi wanaovuliwa soko lake ni la ndani,” anaeleza.

Anasema tayari manispaa hiyo katika kukuza na kuhamasisha uvuvi wenye tija inafikiria kuanzisha teknolojia ya uvuvi wa vizimba kwa lengo la kudhibiti uvuvi haramu lakini pia kuhamasisha uvuvi wenye tija.

Tayari teknolojia hiyo imeanza kutumika katika nchi za Uganda na Kenya ambapo kwa Tanzania haikuanza kutumika kutokana na Sheria iliyopo ya Uvuvi Na 22 ya mwaka 2003 kukataza uvuvi wa vizimba. Kwa sasa sheria hiyo iko kwenye mchakato wa kufanyiwa marekebisho kuruhusu vizimba hivyo.

Kwa upande wake, Ofisa Uvuvi wa manispaa hiyo ya Bukoba, Ignatio Rwinwa anaelezea uvuvi wa vizimba kuwa ni utaratibu wa kugawa maeneo ya uvuaji ndani ya ziwa na kugawiwa kwa mwekezaji.

“Kwa sasa na kwa hali ilivyo kila mtu ana uhuru wa kuvua kwenye ziwa huku wengine wakitumia uhuru huo vibaya na kufanya uvuaji haramu unaoharibu mazingira ndani ya ziwa hilo Victoria. Sasa teknolojia hii ya vizimba itadhibiti matatizo yote haya,” anasema.

Anasema mwekezaji wa uvuvi wa samaki akiweka kizimba chake atakuwa huru kuwalisha samaki chakula cha nyongeza kwa lengo la kuwaongezea ukubwa hali itakayomuwezesha kuvua samaki hadi tani mbili na hivyo kupata faida.

Hata hivyo, Rwinwa anafafanua kuwa pamoja na kuwepo kwa mpango huo wa manispaa bado sheria iliyopo hairuhusu uvuaji huo kwa kuepuka mtu mmoja kutawala eneo la ziwa lakini suala hilo linafanyiwa kazi na huenda kwenye marekebisho ya sheria ya uvuvi vizimba vikaruhusiwa.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Muleba Emmanuel Sherambi anasema Muleba uvuvi ndio shughuli kubwa ya wakazi wa wilaya hiyo kutokana na uwepo wa ziwa Victoria.

Anabainisha kuwa sehemu kubwa ya wilaya hiyo iko ndani ya ziwa hilo ambapo wilaya hiyo ina ukubwa wa kilometa za mraba 10,739 kati ya hizo kilometa za mraba 7295 zipo ndani ya ziwa hilo. “Kwa hali ilivyo uvuvi ndio shughuli kuu ya wakazi wetu.

Ndani ya ziwa kuna visiwa 31 kati ya hivyo visiwa 25 ni makazi ya watu na vilivyobaki ni vitupu. Ni wazi kuwa iko fursa nzuri sana ya uwekezaji katika viwanda vya kusindika samaki,” anafafanua.

Kwa upande wa halmashauri ya wilaya ya Kyerwa, Mkurugenzi wake, Shedrack Mhagama, anasema uvuvi katika wilaya hiyo unatokana na mto Kagera unaotengeneza maziwa madogo.

Anaeleza kuwa takribani kilometa za mraba 10,071 wilayani Kyerwa ni eneo la maji linalotokana na maziwa hayo madogo sita ambayo ni Kalenge, Mitoma, Katwe, Merule, Rushwa, Kitega, Ruko na Rumanyika. Anasema kuwa mpaka sasa wilaya hiyo imetoa leseni 98 za uvuvi, ina takribani wavuvi waliosajiliwa 301 na vyombo vya uvuvi vilivyosajiliwa 45 na visivyosajiliwa 143.

HUDUMA bora za afya ya msingi zinapunguza uhitaji, gharama na ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi