loader
Picha

Kampuni za simu zitende haki kwa wateja

KAMPUNI za simu nchini zimedaiwa kwenda kinyume na maagizo ya serikali kuhusu tozo za bei elekezi za kupiga simu kwa wateja wake.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi, Mawasiliano (Mawasiliano), Atashasta Nditiye ametoboa siri ya kampuni za simu kwenda kinyume na bei elekezi ya serikali kupiga simu Sh10.40 kwa dakika moja badala ya sekunde.

Ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzichukulia hatua kampuni zote za simu zinazodaiwa kukiuka maelekezo hayo.

Tumeshtushwa na habari hizo na tunaungana na waziri huyo kuitaka TCRA kuzichukulia hatua kwa mujibu wa sheria za nchi na sheria za mawasiliano na kanuni zake.

Inashangaza kidogo kwamba pamoja na serikali kutaka biashara ya simu iwe ya uwazi kwa kila mtu, watumiaji simu na kampuni za simu, bado kuna kampuni inaendelea kufanya isivyo.

Ni kwa msingi huo tunasema, tumesikitishwa na habari hizo na tunaomba hili lisijirudie tena kwa kampuni kutotii maelekezo ya serikali na sheria.

Kama kampuni hizo zina hoja ya msingi kuhusu suala hilo, zina fursa ya kuwasilisha malalamiko yake kwa mamlaka husika ili yafanyiwe kazi.

Vinginevyo, wananchi hasa wateja watatafsiri hatua hiyo kama kuwaibia fedha zao kwani tozo hizo zinakuwa kinyume cha sheria na kanuni. Wahenga walisema kufanya kosa siyo kosa bali kurudia kosa.

Hivyo, hatutarajii baada ya waziri kuwaumbua wenye kampuni hizo, zitaendelea kutoza kiwango hicho bali zitafuata maelekezo.

Tunaomba kampuni za simu ziwe mstari wa mbele kuwawezesha wateja wao kutumia simu kwa mawasiliano kwa bei nafuu zaidi ya sasa.

Tunasema hivyo kwa sababu serikali inaendelea kuboresha sekta ya mawasiliano kwa lengo la kurahisisha maisha ya wananchi na kukuza uwekezaji kuinua uchumi kwenda wa kati 2025.

Hivyo basi ni muhimu kwa kampuni za simu nchini kushiriki mkakati huo wa serikali kwani ni wadau muhimu katika maendeleo kwa kuwa mawasiliano ni nyenzo muhimu ya maendeleo.

Kwa kampuni nyingine ambazo hazijawekeza nchini, tunazikaribisha zilete mitaji yao hapa kwani serikali imeweka mazingira mazuri zaidi ya biashara na uwekezaji hivyo watanufaika pia.

Kwa wadau na hasa wateja watumiaji wa simu, tunaomba watoe taarifa haraka kwa serikali na TCRA mara waonapo hawatendewi haki na kampuni za simu ili haki itendeke kwa kila mtu.

Wafanye hivyo wakijue serikali yao makini iko tayari siku zote kuhakikisha wanatendewa haki na kampuni zozote kwa sababu inawajali sana.

JUMAMOSI iliyopita dunia ilishuhudia Sudan Kusini ikifungua ukurasa mpya wa ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi