loader
Picha

Hifadhi ya Ifisi, eneo usilotakiwa kukosa uwapo jijini Mbeya

RAFIKI yangu mmoja kutoka Finland, Kristoffer Ville alinitania akisema kuwa, Watanzania na Waafrika kwa jumla hawathamini ipasavyo urithi wa wanyamapori, badala yake huuona kuwa tu chanzo cha chakula na fedha.

Alishangaa wakati fulani alipozuru nchini na kuona kuwa mbuga za wanyama hujaa watalii kutoka nchi za magharibi na huku wenyeji wakiwa wachache. Akasema, hata hao wachache wanaozuru ni wa wale wenye mwonekano wa hali nzuri kiuchumi, jambo linalotafsiriwa na wengi kama kutembelea vivutio ni anasa.

Kristoffer akaongeza kuwa, hata hivyo, hana shaka kuwa wanyamapori wanapendwa sana katika sanaa za Kiafrika, kama vile utakavyoona ukizuru maduka ya vinyago. Akiolojia inabainisha, wanyamapori ni kitu kikubwa cha sanaa za Kiafrika kutokea enzi za kale.

Japo sikumwuliza Kristoffer kama hilo la wanyamapori kupendwa sana katika sanaa za Kiafrika ni uthibitisho wa kuthamini uzuri wa wanyamapori, lakini kauli yake imenikumbusha mwaka 2016 baada ya suala la utalii wa ndani kuonekana kuzorota nchini.

Ndipo Bodi ya Utalii Tanzania na asasi binafsi za utalii wakaanza mikakati ya kusaidia kuamsha ari ya wananchi kutembelea vivutio vyao na kuachana na dhana kuwa, utalii ni kwa ajili ya wanaotoka nchi za Ulaya tu.

Nakumbuka kampuni ya Utalii ya Kili Base Adventures ilizindua Tamasha maalumu la kila mwaka (ingawa sina hakika kama linaendelea) la mwana ndondi mstaafu wa ngumi za kulipwa, Rashid Matumula kuongoza hamasa hiyo huku likihitimishwa na watalii wazawa kuupanda Mlima Kilimanjaro.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Kili Base Adventures, Sifael Malle aliwahi kuliambia Shirika la Habari za Uingereza (BBC) kuwa, kutokana na utafiti wao, walibaini kuwa raia wengi katika nchi za Afrika Mashariki hawaoni umuhimu wa kufanya utalii wa ndani na hawana ueledi mkubwa wa vivutio vilivyo katika maeneo yao.

Licha ya kuonekana kuwa watalii huvutiwa zaidi kutembelea hifadhi kubwakubwa za wanyama pori katika mbuga za kitaifa kama Serengeti, Ngorongoro, Mikumi na kadhalika, labda kutokana na mikusanyo mikubwa zaidi wa wanyama wakubwa wa porini, lakini pia tunayo mengi ya kuvutia katika hifadhi ndogo za wanyamapori maarufu kwa jina la kigeni la ‘zoo’.

Kwa mfano, licha ya Mbeya kuwa mji unaosifika kwa kuwa na ardhi nzuri inayovutia na yenye rutuba ya kutosha, lakini kuna vingi vilivyojificha katika mkoa huu vitakavyokufanya ufurahie uwepo wako mkoani humo. Kwanza, hali ya hewa ya Mbeya haichoshi kutembea ili kujionea vivutio mbalimbali vilivyopo katika mji huu uliobarikiwa kuwa na safu za milima na madhari nzuri ya kijani. Ndiyo maana, wenyeji huita Mbeya “Green City” yaani Jiji la Kijani.

Hata utakapoamua kwenda kupanda Mlima Loleza au kutembelea katikati ya jiji, eneo maarufu Uhindini, kuna mahali hautakiwi kukosa kufika iwapo wewe ni mpenzi wa kutazama wanyamapori. Eneo hilo ni Hifadhi ya Wanyamapori na Makumbusho ya Ifisi.

Hifadhi hiyo, ambayo wengine huitazama kama “Bustani” ya wanyama iliyopo kilometa 4.3 kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe, inalo korongo kwa ajili ya kwenda kuzunguka na kuangalia wanyamapori wafugwao wakiwemo swala, fisi, ngedere, nyumbu, sungura, nyoka kama chatu na wengine wengi.

Ukiwa Hifadhi ya Wanyamapori na Makumbusho ya Ifisi, utaweza pia kumuona kasuku mwenye umri wa zaidi ya miaka 32 ambaye ni kivutio katika zoo hiyo huku kukiwa na tausi wa kiume wazuri na wenye rangi za kuvutia. Vilevile utaona nungunungu pamoja na bata aina mbalimbali watakaokufanya ufurahie mandhari hayo ambayo huchagizwa na ubaridi kidogo wa jiji hilo.

Sanjari na utalii wa wanyama hao, kwa watu wanaofika katika kivutio hicho hufanikiwa kuona nyumba ya utamaduni au makumbusho yenye vifaa vya kitamaduni kutoka kwa watu wa makabila ya Nyanda za Juu Kusini, wakiwemo Wanyakyusa, Wafipa, Wasafwa, Wahehe na Wabena. Kinachovutia zaidi ni jinsi utakavyoweza kupanda kibao maalumu ambapo utaona kwa karibu madhari ya bustani ya wanyama kwa ukaribu zaidi na utapata bahati ya kuzungushwa porini na kuona swala wakiwa katika harakati zao za kujitafutia chakula.

Kwa wapenzi wa kuweka kambi maarufu ‘camping’ na watu wanaopenda kupumzika sehemu ambapo watakuwa huru na utulivu wa kutosha, eneo hilo nalo ni suluhisho kwa muda wakati wakijipanga kwenda kwenye hifadhi kubwa za wanyama, wakipenda waanaweza kwenda zilizo jirani na mkoa huo kama Kitulo, Ruaha au Katavi. Hifadhi ya Wanyamapori na Makumbusho ya Ifisi ilifunguliwa mwaka 2008 na Rais mstaafu Jakaya Kikwete. Ipo umbali wa kilometa 19 kutoka Mbeya Mjini, ikiwa pembezoni mwa barabara inayoelekea nchini Zambia.

Pamoja na fursa ya kutoa utalii katika mkoa huo, Hifadhi hii ya Wanyamapori na Makumbusho ya Ifisi inakabiliwa na changamoto za miundombinu kutembelea wanyama waliopo porini katika eneo hilo. Juhudi zinapaswa kuongezwa kasi ili katika kipindi chote cha mwaka zikiwamo nyakati za masika, barabara na njia zinazotumika kuingia katika korongo hilo ziendelee kutumika bila shaka yoyote.

Pia, ili kuona wanyama wote baadhi ya watalii watapaswa kulala maeneo hayo kwa kuwa baadhi ya wanyama hawaonekani nyakati za mchana na uongozi umelazimika kuruhusu wageni kuingia usiku.

Kama ilivyo kwa vivutio vingine vya kitalii nchini, Hifadhi ya Wanyamapori na Makumbusho ya Ifisi imechangia kuwapa ajira baadhi ya wakazi wa mji huo wanaofanya shughuli za uhudumu, watoa usafiri kama teksi na pikipiki maarufu kama bodaboda, na wanaouza vyakula na watoa huduma za malazi. Kuingia na kufurahia vivutio vya Hifadhi ya Wanyamapori na Makumbusho ya Ifisi lazima uvunje ‘kibubu’ kidogo ili ufurahie zaidi na zaidi ziara (utalii) yako.

Kama alivyowahi kunukuliwa Msimamizi Msaidizi wa Hifadhi ya Wanyamapori na Makumbusho ya Ifisi, Stanley Kiduko, ada ya kuingia ni nafuu huku ikitofautisha wakubwa, wanafunzi wa sekondari na wale wa shule za msingi na watoto.

Kutokana na nia ya hifadhi hiyo kualika wageni wengi kwa gharama nafuu wanachoweza kumudu watu, wageni na wenyeji hulipa kiingilio kilicho sawa katika makundi hayo. Kiduko anasema sehemu kubwa ya wanaotembelea Hifadhi ya Wanyamapori na Makumbusho ya Ifisi ni wageni huku kundi kubwa la wenyeji wanaofika kutembelea kivutio hicho wakiwa wanafunzi, jambo linaloonesha kuna wenyeji wengi ambao hawajabahatika kufanya utalii huo wa ndani.

Kauli ya Kiduko inanipeleka moja kwa moja kwenye kile alichokiongea rafiki yangu Kristoffer: huenda ni kweli hatuuthamini sana urithi wa wanyamapori bali tunauona kuwa tu chanzo cha chakula na fedha.

Kwa kipindi kirefu kumekuwa na mikakati ya kuongeza pato la ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi