loader
Picha

Mwanri atoa wiki 2 kutekelezwa hoja za CAG

MKUU wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri ametoa muda wa wiki mbili kwa Ofi si ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa Tabora kutekeleza hoja zote za ukaguzi zilizobainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG).

Alitoa agizo hilo jana katika kikao maalumu cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo cha kujadili taarifa ya ukaguzi ya CAG kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Alisema kuwepo kwa hoja zisizojibiwa katika taarifa ya hesabu za halmashauri yoyote ile kwa kiasi kikubwa kunasababishwa na watendaji wasiowajibika ipasavyo katika idara na vitengo vyao.

Alisema kati ya hoja 50 zilizoainishwa na CAG kwa manispaa hiyo, 26 tu ndiyo zimetekelezwa kikamilifu, zingine bado, hivyo akamuagiza Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Bosco Ndunguru kuhakikisha hoja hizo zinatekelezwa kikamilifu ndani ya wiki mbili kuanzia sasa na si vinginevyo.

Mwanri aliagiza kila mtumishi anayehusika na hoja hizo kutimiza wajibu wake ili hoja zote hizo zifutwe, alimtaka mkurugenzi kuchukua hatua stahiki kwa yeyote atakayezembea kutekeleza agizo hilo.

Alisisitiza kuwa taarifa ya CAG imetoa maelekezo ya kile kinachotakiwa kufanyika kwa kila hoja, hivyo akaagiza mapungufu yote yaliyobainishwa katika mikopo, masurufu, mapato na matumizi kurekebishwa haraka iwezekanavyo.

Ili kukomesha uzembe unaofanywa na baadhi ya watumishi wa manispaa hiyo, Mkuu wa wilaya ya Tabora mjini, Komanya Kitwala alimuagiza mkurugenzi na madiwani wa manispaa hiyo kuwachukulia hatua watumishi wote waliozembea na kusababisha hoja hizo kutofutwa hadi sasa.

Mkaguzi wa nje, Erasto Juma alisema katika ukaguzi wa hesabu za mwaka 2017/2018 manispaa hiyo ilipata hati inayoridhisha lakini hiyo haimaanishi kuwa wana ufanisi wa asilimia 100 katika udhibiti wao wa ndani.

Aliwataka kuhakikisha hoja zote zilizoainisha na CAG ambazo hadi sasa hazijajibiwa ikiwemo maagizo mawili ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kufanyiwa kazi ili zisijirudie tena katika taarifa ijayo.

Meya wa manispaa hiyo, Leopold Ulaya aliwataka madiwani wote wa halmashauri hiyo kutoa ushirikiano ili kuhakikisha hoja zilizobaki zote zinafutwa ndani ya muda wa wiki mbili.

BODI ya Ithibati inayotajwa katika Sheria ya Huduma ...

foto
Mwandishi: Lucas Raphael, Tabora

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi