loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kiswahili lugha rasmi SADC

HATIMAYE Kiswahili kimetangazwa kuwa lugha rasmi ya nne ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) hatua itakayowezesha kutumika katika shughuli rasmi za jumuiya.

Kiswahili ambayo ni lugha ya Taifa ya Tanzania, itatumika sambamba na lugha nyingine za rasmi za SADC ambazo ni Kiingereza, Kireno na Kifaransa. Kiswahili kilitangazwa rasmi lugha ya nne ya jumuiya hiyo jana, Dar es Salaam na aliyekuwa Mwenyekiti wa SADC, Dk Hage Geingob alipohutubia Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa jumuiya hiyo kabla ya kukabidhi madaraka kwa Mwenyekiti mpya, Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli.

Dk Geingob ambaye ni Rais wa Namibia alisema, “natangaza rasmi kwamba Kiswahili kitakuwa lugha rasmi ya nne ya SADC.”

Kauli hiyo aliyoitoa muda mfupi kabla ya kukabidhi madaraka kwa Rais Magufuli kuelekea hitimisho la hotuba yake, iliufanya ukumbi kulipuka kwa vigelele na shangwe hasa kutoka kwa wananchi wa Tanzania waliokuwa wengi kutokana na wenyeji wa mkutano.

Baada ya kutangaza, hali katika Ukumbi wa Selous wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), ilibadilika huku baadhi ya washiriki wa ufunguzi huo wakishangilia kwa kusimama na kuungwa mkono na watu wengi (wasio Watanzania) waliohudhuria tukio hilo.

Awali akitoa hotuba ya makaribisho, Rais Magufuli alianza kuzungumza kwa Kiingereza na kueleza jinsi Kiswahili kilivyotumika kama lugha ya ukombozi wakati wa harakati za kutafuta uhuru kwa nchi nyingi za Afrika. Dk Magufuli alisema mapambano ya ukombozi wa Afrika yalifanikiwa na nchi zote za Afrika katika miaka ya 1990 zilipata uhuru kwa sababu ya matumizi ya Kiswahili.

Akifafanua alisema Kiswahili ni lugha ya 10 duniani kuzungumzwa na watu wengi na ya 13 Afrika na ya sita katika nchi za SADC.

“Ni lugha rasmi Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni lugha rasmi kwa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na kutokana na hayo, ninaomba niendelee na mazungumzo yangu kwa Kiswahili, itachochea kuifanya kuwa lugha rasmi,” alisema Rais Magufuli na kuendelea kuiwakaribisha wageni kwa Kiswahili.

Rais Magufuli alipofungua Maonesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda, alitoa hutuba yake kwa Kiswahili kudhihirisha umuhimu wa lugha hiyo iliyotumiwa na wapigania uhuru wa nchi za kusini mwa Afrika kwa ukombozi.

Viongozi wengine kabla ya lugha hiyo kutangazwa rasmi jana, katika matukio mbali mbali ya mikutano ya waandishi wa habari na mijadala mbali mbali walitumia Kiswahili.

Awali, Baraza la Mawaziri wa SADC lilipendekeza lugha hiyo kuwa lugha rasmi lilipotoa mapendekezo yake 107 waliyoyawasilisha kwenye Mkutano huo wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa jumuiya hiyo kwa uamuzi.

Mwenyekiti wa baraza hilo, Profesa Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, alieleza mapendekezo hayo kwa waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa baraza hilo Agosti 14, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kuhusu Kiswahili, Profesa Kabudi aliwashukuru wajumbe wa baraza kuona Kiswahili kinafaa kupendekezwa kuwa lugha rasmi ya SADC na hatua hiyo inadhihirisha kuthamini mchango wa Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere katika ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika.

Akifafanua, Profesa Kabudi alisema Kiswahili kilitumika kama lugha ya ukombozi kwa wapigania uhuru, lakini pia kinatumika kwenye nchi nyingi Afrika.

Alizitaja nchi hizo kuwa ni Somalia, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Kaskazini mwa Zambia.

Alisema pia kuwa Kiswahili kinafundishwa kwenye vyuo vikuu 53 duniani. Afrika Kusini inaanza kukifundisha katika shule za msingi na sekondari.

Marais waliozungumza maneno ya Kiswahili jana katika hotuba zao kabla ya kutangazwa rasmi kuwa lugha ya nne ya SADC ni Rais wa Comoro, Azali Assoumani, Dk Geingob wa Namibia na Felix Tshisekedi wa DRC.

MGOMBEA ubunge Jimbo la ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi