loader
Picha

Madaktari, polisi walaumiwa kukwama kesi za udhalilishaji

IMEELEZWA kwamba, kitendo cha baadhi ya madaktari kukataa kutoa ushahidi mahakamani na polisi kushindwa kufanya uchunguzi unaojitosheleza ni miongozni mwa vikwazo kwa kesi za udhalilishaji wa kijinsia kushindwa kusikilizwa kwa wakati.

Hayo yalisemwa na Hakimu wa Mahakama ya Mkoa wa Kaskazini Unguja, Makame Mshamba, baada ya kuwasilishwa kwa ripoti ya matukio ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwa mikoa ya Kaskazini Unguja na Mkoani Pemba juzi.

Alisema baadhi ya madaktari wamekuwa wakisumbua kutoa ushirikiano, huku wakikataa kufika mahakamani wakati wanapotakiwa kutoa ushahidi kwa mtu aliyefikwa na tukio la udhalilishaji wa kijinsia ikiwamo kubakwa au kulawitiwa. Alisema ni kosa kwa mtu anapoitwa mahakamani kutoa ushahidi kukataa wito huo na inachukuliwa ni sawa na kukwamisha Mahakama kutekeleza majukumu yake.

“Madaktari wanatusumbua sana katika uendeshaji wa kesi zetu kwa sababu wamefanya kazi ya uchunguzi wa kitabibu kwa muathirika sasa wanapoitwa waje wathibitishe mahakamani hawataki, hii si sawa,” alisema.

Alisema zipo baadhi ya kesi zimekwama kwa sababu ya kushindwa kupatikana kwa ushahidi kutoka kwa madaktari waliofanya kazi ya kupima mtu aliyedhalilishwa. Alipoulizwa kwa nini madaktari hao wanakataa kufika mahakamani kutoa ushahidi wa mtu waliyemfanyia uchunguzi, alisema wanadai kwamba hiyo si kazi yao.

Naye ofisa kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Rashida Ahmed, alisema baadhi ya kesi zinazowasilishwa kutoka Jeshi la Polisi uchunguzi wake kwa kiasi kikubwa huwa haujakamilika huku ukiacha maswali mengi ya msingi yanayotakiwa kufanyiwa kazi.

“Tunaletewa baadhi ya kesi za udhalilishaji wa kijinsia kutoka polisi lakini uchunguzi wake kwa kiasi kikubwa huwa haujakamilika na ndiyo maana tunazifuatilia zaidi kwa kutaka kujua mambo ya ziada,” alisema.

Kwa mujibu wa taarifa fupi ya uchunguzi wa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia iliyofanywa na Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa) Zanzibar, matukio hayo yamekuwa yakiongezeka ukiwamo ubakaji na ulawiti kwa watoto wa kiume na wanawake visiwani hapa.

BODI ya Ithibati inayotajwa katika Sheria ya Huduma ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman, Zanzibar

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi