loader
Picha

Tuchangie damu kuokoa walioungua Morogoro

IDADI ya majeruhi wa ajali ya lori la mafuta lililopinduka na kulipuka moto mkoani Morogoro waliokuwa wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam imeendelea kupungua kwa kasi, ambapo sasa wamebakia 15 kati ya 47 waliofikishwa hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu baada ya wengine 29 kufariki dunia.

Ajali hiyo ilitokea Jumamosi ya Agosti 10, mwaka huu katika eneo la Mzambarauni, Msamvu mjini Morogoro baada ya kutokea mlipuko mkubwa katika lori hilo la mafuta aina ya Scania lenya namba za usajili T 717 DDF na trela namba T 645 CAN na kuunguza watu wengu wao wakiwa ni wale waliokimbilia eneo hilo kwa ajili ya kuchota mafuta.

Mpaka sasa idadi kamili ya watu waliokufa kutokana na ajali hiyo imefikia 100.

Majeruhi waliobaki wanaendelea kupatiwa huduma hospitalini hapo katika Chumba cha Uangalizi Maalum (ICU).

Hata hivyo, pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na serikali na madaktari kuokoa maisha ya majeruhi waliobaki hospitalini hapo na waliopo katika hospitali ya mkoa wa Morogoro, tunatoa wito kwa mashirika, taasisi na watu binafsi kuendelea kusaidia majeruhi hao kwa hali na mali ikiwamo kuchangia damu, dawa na vifaa tiba ili kuokoa maisha yao yaliyohatarini.

Tunatoa wito huo kwa sababu bado kuna uhitaji mkubwa wa damu kwa ajili ya majeruhi hao, hali iliyokilazimu kitengo cha damu salama kusaka damu mtaani.

Kitengo hicho cha damu salama juzi Jumatatu Agosti 19 na jana Agosti 20 kilipiga kambi Kigamboni kituo cha Bodaboda na kuhamasisha watu kuchangia damu.

Neema Maro, muuguzi kutoka Kitengo cha Damu Salama Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), amesema mpaka sasa uniti 660 zimeshakusanywa tangu walipoanza Agosti 11 na kwamba licha wa muitikio kubwa wa watu kujitokeza lakini damu bado haijatosha kwani mahitaji ni makubwa.

Alisema Agosti 11 walikusanya uniti 70, Agosti 12 uniti 63, Agosti 13 uniti 120, Agosti 14 uniti 95, Agosti 15 uniti 66, Agosti 16 uniti 91, Agosti 17 uniti 48, Agosti 18 uniti 61 na Agosti 19 zilikusanywa uniti 46 na kufanya idadi ya uniti 660 zilizokusanywa hadi kufikia 660.

Daktari John Bigambalaye ambae ni ofisa uhamasishaji wa damu salama (MNH) ametoa wito kwa watu ambao hawajachoma sindano yoyote ya kinga kama ya homa ya ini, manjano na kinga kinyingine hivi karibuni kujitokeza kuchangia damu.

Hivyo, Watanzania kwa umoja wetu na kila moja kwa dini na imani yake tuendelee kuwaombea ndugu zetu hawa ili wapate nafuu na hatimaye wapone haraka waweze kurejea katika maisha yao ya kawaida na kushiriki ujenzi wa taifa pamoja na kuzisadia familia zao.

TAHADHARI iliyotolewa juzi na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi