loader
Picha

Ushahidi waendelea kesi ya akina Aveva

MCHUNGUZI Mkuu kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Frank Mkilanya ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu ya Simba, Zacharia Hanspoppe, alimueleza kuwa alitumia Dola za Marekani 32,316.64 kulipia malipo ya awali wakati wa ununuzi wa nyasi bandia za klabu hiyo.

Mkilanya amedai katika Mahakama ya Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, wakati akitoa ushahidi wake katika kesi inayowakabili vigogo wa klabu hiyo.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Leonald Swai, shahidi huyo alidai katika ununuzi wa nyasi hizo, Hanspoppe ndiye alianzisha mchakato wa ununuzi wa nyasi hizo pamoja na kufanya mawasiliano kati ya mnunuzi na muuzaji.

Amedai wakati akiandika maelezo ya mshitakiwa huyo wa tatu, alimueleza kuwa walinunua nyasi hizo kutoka kwa wakala anayetambulika kwa jina la Hamis kutoka China aliyenunua nyasi hizo kutoka kampuni ya Ninah Trading Company.

“Kesi hii ilianza kufunguliwa kabla ya kuandika maelezo ya mshitakiwa kwakuwa alikuwa hajapatikana lakini baada ya kupatikana ndio maelezo yake yakachukuliwa na hayo ndio nilichukua,” alidai Mkilanya.

Alidai, hundi ya manunuzi ya nyasi inaonesha zilinunuliwa kwa Dola za Marekani 109,499 ambapo Hanspoppe baada ya kupata hundi hiyo alifanya malipo ya awali ya Dola za Marekani 32,316.64 kwa fedha zake binafsi.

Mkilanya alidai, mshitakiwa huyo alimueleza kuwa hundi hiyo baadaye alimkabidhi aliyekuwa rais wa klabu hiyo Evans Aveva na wakala (Hamisi) alipokuja nchini na kumpa fedha taslimu Dola za Marekani 15,000.

Alidai kuwa, Hanspoppe alimueleza kuwa wakala huyo ameshafariki.

Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi kesho kwa ajili ya kusikilizwa. Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa makamu wa rais wa klabu hiyo Godfrey Nyange ‘Kaburu’.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka 10 ikiwemo kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi, kutoa maelezo ya uongo na utakatishaji wa fedha.

Katika shitaka la kughushi linawakabili washitakiwa wote, inadaiwa katika tarehe hizo hizo kwa pamoja walighushi hati ya malipo ya kibiashara ya Mei 28, 2016 wakionyesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zenye thamani ya Dola za Marekani 40,577 sawa na zaidi ya Sh milioni 90 huku wakijua kwamba sio kweli.

Pia katika mashitaka mengine inadaiwa Aveva, Nyange na Hans Poppe kati ya Machi 10 na Septemba 30, 2016 waliwasilisha nyaraka za uongo kuonyesha Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Marekani 40,577.

KOCHA wa Simba, Sven Vandenbroeck amesema hajaridhishwa na ...

foto
Mwandishi: Francisca Emmanuel

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi