loader
Picha

Kiswahili; Lugha ya ukombozi na urithi wa kipekee Afrika

HISTORIA ya harakati za ukombozi wa nchi za Afrika, hususani zilizoko kusini mwa Jangwa la Sahara haiwezi kukamilika bila kukitaja Kiswahili.

Historia inaonesha kuwa, katika vita mbili kuu za dunia; Ya kwanza (1914-1918) na ya pili (1939-1945) Kiswahili ni miongoni mwa lugha zilizotumika katika mapambano. Harakati za kupigania uhuru zilichagizwa na Kiswahili.

Wapigania uhuru wengi wa Afrika walijifunza Kiswahili nchini Tanzania katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Makundi ya wapigania uhuru wakati wa harakati za ukombozi waliopewa mafunzo katika kambi za hapa nchini ni Frelimo (Msumbiji), ANC na PAC (Afrika Kusini), ZAPU na ZANU (Zimbabwe), MPLA (Angola) na SWAPO (Namibia) na walisaidiwa na chama cha TANU na baadaye Chama Cha Mapinduzi (CCM) vya Tanzania.

Uganda katika vita ya Idd Amin, Kiswahili kilitumika katika vikosi vya polisi na majeshi katika miaka ya 1978-1979. Athari za Kiswahili nchini Uganda zipo mpaka leo na wengi wanaozungumza Kiswahili hudhaniwa na raia wengine kuwa ni wanajeshi au askari. Nchini Afrika Kusini, wapigania uhuru walioweka kambi Tanzania, baada ya nchi hiyo kupata uhuru mwaka 1994, walirejea kwao na kuendelea kutumia Kiswahili.

Kaulimbiu kama “Ubaguzi wa rangi ni unyama” bado inaishi nchini humo. Hivi karibuni, Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli akihutubia katika Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa jumuiya hiyo, jijini Dar es Salaam, alisema hakuna anayeweza kupinga ukweli kwamba Kiswahili ni lugha ya ukombozi wa Afrika.

Rais Magufuli alisema hatua ya wakuu wa nchi 16 zinazounda SADC kupitisha Kiswahili kuwa lugha rasmi ya nne ya jumuiya hiyo, kumefuta machozi ya Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye ni mpigania uhuru halisi wa Afrika. Rais Magufuli alisema wakati wa harakati za ukombozi, Nyerere alijitoa yeye na nchi yake (Tanzania) kupata kwa hali na mali na alikuwa tayari kuona watu wake wanapata shida ili nchi nyingine zikombolewe.

“Wote Nyerere aliyowatuma na walioshiriki mapambano ya ukombozi walitumia Kiswahili. Haya yote ni kutokana na uongozi bora na kujitoa kwa baba mmoja aliyependa majirani zake, Julius Kambarage Nyerere. Kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi katika SADC tumefuta machozi ya Nyerere,” alisema Magufuli.

Anasema Tanzania imeshiriki mapinduzi katika nchi nyingi za Afrika ikiwemo Shelisheli ambako mwaka 1975 Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilikwenda katika nchi hiyo kusaidia mapinduzi na Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi (sasa marehemu) aliongoza kikosi hicho na baada ya mapinduzi alikaa siku kadhaa nchini humo kama Rais wa Shelisheli.

Rais Magufuli pia anasema katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), majeshi ya Tanzania yalimwaga damu ili nchi hiyo iwe salama. Alisema pia Comoro ilisaidiwa na Tanzania kurejesha amani. Katika kisiwa cha Anjouan nchini Comoro, majeshi ya Tanzania kwa kushirikiana na majeshi kutoka mataifa kadhaa ya Umoja wa Afrika, yalishiriki katika operesheni maalumu mwaka 2008.

Operesheni hiyo ilimng’oa madarakani kiongozi wa uasi Mohamed Bakari aliyekuwa amekiteka kisiwa hicho na kukirejesha chini ya serikali ya Comoro iliyokuwa ikiongozwa na Rais Ahmed Abdallah Sambi wakati huo.

Rais Magufuli anasema azimio rasmi la wakuu wa nchi wa SADC kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi katika jumuiya hiyo yeye binafsi (Dk Magufuli) na Watanzania wote wamelipokea kwa furaha kubwa. Alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wenzake na kuwaeleza kuwa, wameingia katika vitabu vya historia na urithi wa vizazi vya Tanzania na SADC kwani vitakumbuka hatua hiyo siku zote.

Dk Magufuli alisema lugha ni chombo cha kukuza uhusiano na mawasiliano baina ya watu. “Kiswahili ni lugha ya Kiafrika na sisi ni Waafrika, uamuzi huu wa kukifanya kuwa lugha rasmi itaimarisha ushirikiano na wananchi wetu na kukuza mtangamano kati ya mataifa yetu”. Akizungumza katika mhadhara kuhusu SADC uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais mstaafu wa Tanzania na Mwenyekiti mstaafu wa SADC (mwaka 2003), Benjamin Mkapa, aliwataka Waafrika kuwa Waafrika na kuachana na utegemezi uliokithiri kutoka kwa wageni. Utegemezi mmoja wapo ni utumwa wa kukumbatia lugha zilizotumika katika ukoloni na kudhani bila hizo, hatuwezi kujitegemea.

Katika hotuba yake ya makaribisho kwa wageni wa mkutano huo wa 39, Rais Magufuli alisema mapambano ya ukombozi wa Afrika yalifanikiwa na nchi zote za Afrika katika miaka ya 1990 zilipata uhuru kwa sababu ya matumizi ya Kiswahili. Akifafanua alisema Kiswahili ni lugha ya 10 duniani kuzungumzwa na watu wengi na ya 13 Afrika na ya sita katika nchi za SADC.

“Ni lugha rasmi Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni lugha ya mawasiliano katika Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) na kutokana na hayo, ninaomba niendelee na mazungumzo yangu kwa Kiswahili, itachochea kuifanya kuwa lugha rasmi,” alisema Magufuli alipotoa hotuba ya makaribisho kabla Kiswahili kupitishwa kuwa lugha ya nne ya SADC.

Katika hotuba zake kwenye mkutano huo wa SADC, Magufuli aliwasihi nchi wanachama ambako Kiswahili hakitumiki, kuiga mfano wa Afrika Kusini itakayoanza kufundisha lugha hiyo katika shule zake mwakani. Alimhakikishia Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, aliyekuwepo katika mkutano huo kuwa, Tanzania itatoa ushirikiano wote kwa kutoa walimu na nyenzo mbalimbali za kufundishia zitakazohitajika.

“Jana nimewapa marais wote vitabu vya Kiswahili, wataenda navyo nyumbani na wote wamevipokea vizuri,” alisema mwenyekiti huyo wa SADC, Rais Magufuli.

Kudhihirisha Kiswahili ni urithi wa Afrika, katika mkutano huo wa SADC, Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa SADC, alizungumza sentensi kadhaa kwa Kiswahili, alipozungumza. Naye Rais wa Afrika Kusini, Ramaphosa aliandika kwa Kiswahili katika mtandao wake wa kijamii wa twitter maneno ya pongezi kwa Tanzania na Rais Magufuli na furaha yake kutembelea eneo la kumbukumbu la Mazimbu, Morogoro, walikozikwa mashujaa 70 wa nchi yake waliopigania uhuru ambao walitumia Kiswahili.

Alisema amejiwekea siku ya Jumatatu kila wiki kama siku yake ya kujifunza Kiswahili. Agosti 17 siku ulipofunguliwa mkutano huo, aliyekuwa Mwenyekiti wa SADC, Rais wa Namibia, Dk Hage Geingob, alitangaza Kiswahili kuwa lugha rasmi ya nne ya SADC na wakuu wa nchi baadae waliipitisha rasmi lugha hiyo katika kikao chao cha ndani. Lugha ya kwanza kutumika katika SADC ni Kiingereza, ikifuatiwa na Kifaransa na lugha ya tatu ni Kireno (zote zinatokana na ukoloni) na ya nne ni Kiswahili (lugha ya kibantu ya Afrika).

Hatua hiyo inakifanya Kiswahili kuanza kutumika katika hotuba, machapisho na vikao vyote rasmi vya jumuiya hiyo. Viongozi wa Tanzania waliozungumza baada ya Kiswahili kupitishwa rasmi SADC, akiwamo Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas, walisema ni fursa ya pekee na heshima kubwa Tanzania imepata. Dk Abbas alisema ni wakati wa kuhakikisha wafanyabiashara wa Tanzania hasa vijana wanatumia fursa ya Uenyekiti wa Tanzania na kupitishwa kwa Kiswahili kupata ajira katika nchi wanachama.

Awali, Baraza la Mawaziri wa SADC katika mkutano wake wa Agosti 13 na 14 jijini Dar es Salaam, lilipendekeza lugha hiyo kuwa lugha rasmi lilipotoa mapendekezo yake 107 waliyoyawasilisha kwenye Mkutano huo wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa jumuiya hiyo kwa uamuzi. Mwenyekiti wa baraza hilo, Profesa Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania alisema Kiswahili ni lugha ya ukombozi na inazungumzwa katika nchi nyingi duniani.

Alisema nchi ambazo Kiswaili kinazungumzwa ukiondoa Kenya na Tanzania ni Somalia, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), maeneo ya Kaskazini mwa Msumbiji na Kaskazini mwa Zambia.

Alisema pia kuwa Kiswahili kinafundishwa kwenye vyuo vikuu 53 duniani. Mapema wiki hii, akizungumza na gazeti hili kuhusu vipaumbele vya Uenyekiti wa Tanzania katika SADC, Profesa Kabudi alitaja maeneo matatu ya kipaumbele ambayo ni kuongeza biashara katika kanda; kusimamia Kiswahili kifundishwe shuleni katika nchi wanachama; na kampeni ya kuiondolea Zimbabwe vikwazo.

Vipaumbele hivyo ni sehemu ya maazimio 36 yaliofikiwa na wakuu wa nchi za SADC. Katika eneo la Kiswahili, Profesa Kabudi alisema Tanzania itasimamia lugha hiyo si tu katika kutumika kama lugha rasmi kwenye hotuba na machapisho ya SADC, lakini kuhakikisha nchi wanachama wanafundisha lugha hiyo shuleni.

Akifafanua namna Tanzania ilivyojipanga kwenye uwekezaji kuhakikisha lugha hiyo inazungumzwa katika nchi wanachama na kama kuna fedha imelipwa Kiswahili kuingia SADC au itahitajika katika uwekezaji wa wataalamu, alisema hakuna fedha yoyote Tanzania italipa kwa Kiswahili kuingia katika jumuiya hiyo.

Profesa Kabudi alifafanua kuwa, uwekezaji pekee ni kuhakikisha nchi ina wataalamu wa kutosha hasa walimu mahiri wa lugha (si Kiswahili peke yake) watakapohitajika kwenda katika nchi hizo kufundisha na kueleza kuwa nchi itapata faida kwa watu wake kupata ajira. Kuhusu vitabu, alisema nchi husika itanunua vitabu vya Kiswahili kwa ajili ya shule zake.

Alifafanua kuwa, katika Umoja wa Afrika (AU) Kiswahili kililipiwa kiasi cha fedha kuingia katika umoja huo kwa kuwa kilichukuliwa kama lugha ya kibantu lakini kwa SADC Kiswahili ni lugha ya ukombozi.

BAADA ya kupiga kambi kwa siku tofauti 15 katika vituo ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi