loader
Picha

Hifadhi ya Nyerere kufungua fursa Ukanda wa Kusini

RAIS John Magufuli, Julai 26, 2019 aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (Julius Nyerere Hydro Power Project -JNHPP) katika bonde la Stiegler, kwenye pori la akiba la Selous wilayani Rufi ji mkoani Pwani.

Katika tukio hilo, Rais aliiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kumega sehemu ya Pori la akiba la Selous na kuanzisha hifadhi itakayoitwa Hifadhi ya Taifa ya Julius Nyerere. Pori la akiba la Selous lina ukubwa wa kilomita za mraba 55,000 na hivyo kulifanya kuwa ndilo eneo kubwa zaidi la wanyamapori barani Afrika.

Ni mbuga ya pili baada ya Serengeti kwa wingi wa aina za wanyamapori na kubwa kuliko nchi ya Uswisi au Ireland. Selous ipo kwenye ukanda wa utalii wa kusini unaohuisha mikoa ya Lindi, Ruvuma, Morogoro na Pwani.

Hatua ya Rais Magufuli ya kuanzisha Hifadhi hii ya Taifa ya Julius Nyerere katika eneo la Selous ni ya kupongezwa sana kwani eneo hili licha ya kuwa na vivutio vingi vya asili vya utalii, ni watalii wachache waliokuwa wakilitembelea, tena watalii wawindaji.

Ni kwa mantiki hiyo, Selous halikuwa na tija sana katika kuliingizia mapato taifa ukilinganisha na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo inafanana sana na Selous kwa wingi wa wanyamapori wa aina tofauti tofauti. Bila shaka Hifadhi ya Taifa ya Julius Nyerere itachochea shughuli za utalii kwenye eneo la Selous na Ukanda wa Utalii wa Kusini kwa ujumla kwa kuwa miundombinu itaboreshwa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa hoteli, barabara za ndani ya hifadhi na za nje ya hifadhi, mawasiliano na hudumu nyingine muhimu kwa watalii.

Hifadhi hii itavutia watalii wengi na inaweza ikakaribiana kulingana au hata kuzidi hifadhi ya Serengeti na hivyo kuiingiza nchi yetu fedha nyingi za kigeni mbali na kuongeza ajira. Sababu zinazoifanya Selous kuwa hifadhi itakayokuwa bora ziko nyingi, miongoni ni kuwa pori ambalo bado halijatumika sana kwa shughuli za kitalii, hivyo kuwa na uasili mwingi kama vile misitu ya asili, maporomoko ya maji ya asili na mito ya asili.

Ni hifadhi yenye wingi wa aina za wanyamapori kwa maana ya makundi ya tembo, simba, mbwa mwitu, nyumbu, nyati, faru weusi, mamba, viboko na ndege. Sababu ya pili ni kutokana na historia yake ambapo mwindaji na askari wa Kingereza aliyeitwa Captain Frederick Courtney Selous aliuawa kwa kupigwa risasi na askari wa vikosi vya Ujerumani vilivyokuwa vikiongozwa na Jenerali Von Lettow Vorbeck tarehe 4, Januari mwaka 1917 wakati wa vita kuu ya kwanza ya dunia.

Pori hili lilipata jina la Selous mwaka 1922 lilipoanzishwa kwa heshima ya hayati Captain Selous. Halikadhalika eneo la Stiegler’s gorge ndipo mvumbuzi Mjerumani, Stiegler, aliuawa na tembo mwaka 1907.

Sababu hizi za kihitosria zitawavutia watalii kutoka Uingereza, Ujerumani na maeneo mengine kuja kutalii na kupata historia ya eneo hili. Aidha wanahistoria na watafiti wengi watavutika pia kuja kutalii kwenye hifadhi hii. Sababu ya tatu inayoifanya Selous kuvuta watalii wengi ni Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kulipa hadhi ya urithi wa dunia tangu mwaka 1982 kutokana na mfumo wake mzuri wa ikolojia.

Watalii watahamasika kuja kuona mfumo wa ikolojia wa eneo hili. Sababu ya nne ni kwamba eneo hili lina vivutio vingi vya utalii na shughuli nyingi za utalii zinaweza kufanyika kama vile utalii wa kutembea kwa miguu kwa kuambatana na askari wa wanyamapori mwenye silaha, utalii wa kutumia boti, utalii wa kuvua samaki, utalii wa kuangalia wanyamapori kwa kutumia gari na utalii wa kupiga picha.

Sababu ya tano eneo hili ni tulivu. Ni eneo zuri kwa ajili ya utalii wa kupumzika (holiday and leisure). Kwenye bonde la Stiegler mito ya Rufiji na Ruaha inakutana na kufanya kivutio kizuri kwa watalii wanaokuja kupumzika. Sababu ya sita ni hifadhi hii kuwa karibu na Jiji la Dar es Salaam, takribani umbali wa kilomita 250 tu kutoka katika jiji hilo mashuhuri nchini.

Watalii wengi wanaoshuka katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, itakuwa ni rahisi kwao kufika kwenye hifadhi hii kwa muda mfupi. Pori la akiba la Selous limegawanywa katika maeneo manne, moja wapo likiwa ni eneo la kaskazini. Katika eneo hili shughuli za utalii wa kuangalia wanyamapori, utalii wa boti, utalii wa kutembea kwa miguu na mapumziko kwenye hoteli (kambi za kitalii) hufanyika. Katika maeneo ya kusini, mashariki na magharibi shughuli za uwindaji wanyamapori katika vitalu vya uwindaji hufanyika (hunting blocks).

Eneo la bonde la Stiegler panapojengwa mradi wa kufua umeme wa Mwalimu Nyerere hufanyika utalii wa kutembea. Mradi wa umeme pia utatoa fursa mpya ya utalii wa kuangalia mitambo ya umeme wa maji. Eneo ambalo litamegwa kufanya Hifadhi ya Taifa litakuwa ni la Kaskazini ambako shughuli za utalii zinafanyika na eneo kubwa litaendelea kubakia na shughuli zake za awali.

Kutoka Jiji la Dar es Salaam hadi eneo la hifadhi ni wastani wa kilomita 250 na mtu anaweza kufika kwa kutumia njia tatu; usafiri wa barabara kupitia Kibiti - Mkongo hadi Rufiji River Camp au kutumia barabara kutoka Dar es Salaam - Morogoro – Matombo – Kisaki hadi Stiegler’s Gorge.

Njia ya pili ni ya kutumia reli ya Tazara hadi katika stesheni ya Fuga na kisha kutumia magari kutoka kwenye hoteli mbalimbali. Njia ya tatu ni kutumia usafiri wa ndege ndogo (charter) ambazo zinaweza kutua kwenye viwanja vya ndege vilivyopo kwenye kila hoteli. Shughuli za utalii wa aina mbalimbali hufanyika kutokea kwenye hoteli hizi.

BAADA ya kupiga kambi kwa siku tofauti 15 katika vituo ...

foto
Mwandishi: Ernest Makunga

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi