loader
Picha

Sekta ya utalii inavyopiga hodi Kagera

KATI ya nchi zinazokuja kwa kasi katika kuboresha sekta ya utalii ni pamoja na Tanzania kutokana na kuwa na vivutio vingi na vya aina yake vya utalii.

Tanzania ni nchi inayoongoza Afrika kwa kuwa na utalii wa aina mbalimbali ukiwamo wa mbuga na hifadhi za wanyama, misitu, maziwa, mali kale, milima, mila na tamaduni zinazotokana na historia ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), mchango wa utalii katika pato la taifa ni asilimia 14, ukiingiza wastani wa dola za Marekani bilioni 6.7 kwa mwaka. Hata hivyo, kiasi hicho cha fedha na mchango wa sekta ya utalii katika pato la taifa unatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 6.6 kila mwaka katika kipindi cha miaka 10 ijayo, kwa mujibu wa Baraza la Kusafiri na Utalii wa Dunia (WTTC).

Bodi ya TTB inabainisha kuwa takribani asilimia 12 ya ajira nchini imetokana na sekta ya utalii ambayo ni sawa na ajira milioni moja. Tanzania ni nchi ya saba kwa kutembelewa zaidi katika nchi za Jangwa la Sahara baada ya Afrika Kusini yenye watalii milioni 9.5, Zimbabwe (milioni 1.9), Msumbiji (milioni 1.7), Uganda (milioni 1.27), Kenya (milioni 1.26)na Namibia (milioni 1.2).

Takribani asilimia 81 ya watalii wanaotembelea Tanzania hutembelea nchi hiyo kwa burudani na wengi wakiwa mapumziko na asilimia 46 wanatokea nchi za Afrika wakati asilimia 32 wanatokea nchi za Ulaya.

Takribani kila mkoa wa Tanzania una aina tofautitofauti za utalii lakini nyingi zikiwa ni utalii wa mbuga na hifadhi za wanyama, misitu ya hifadhi na malikale. Mikoa maarufu kwa utalii ni pamoja na Kilimanjaro, Manyara, Arusha, Iringa, Bagamoyo, Zanzibar, Katavi, Mara na Ruvuma kutokana na vivutio vyake vingi kuwa maarufu.

Hata hivyo, ipo mikoa inayoanza kuibukia kwa sekta ya utalii kukua kwa kasi ukiwamo mkoa wa Kagera ambao upo Kaskazini Magharibi mwa Tanzania. Ingawa kiutalii bado mkoa huo hausikiki sana lakini kwa kipindi cha hivi karibuni, umeanza kuingia kwenye ramani ya utalii kupitia vivutio vingi ilivyo navyo.

Akizungumza na waandishi wa habari kutoka Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Marco Gaguti anasema mkoa huo kwa sasa una fursa kubwa ya utalii kutokana na serikali kuyapandisha hadhi mapori matano ya akiba ya Biharamulo, Buringi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika kuwa Hifadhi za Taifa.

Anasema kutokana na hatua zinazoendelea za kurekebisha miundombinu, ipo fursa ya ujenzi wa hoteli za kitalii, uanzishaji wa kampuni za utalii na shughuli za uongozaji watalii, utangazaji wa utalii wa kitamaduni na uendelezaji wa vivutio vya asili vya utalii vilivyopo katika mkoa wa Kagera.

Hivi karibuni, wakati akizindua hifadhi hizo tatu ya Burigi-Chato, Rumanyika na Ibanda, Rais John Magufuli alisema hifadhi hizo kuwa zina sifa ya kipekee kutokana na kuwa na maliasili za wanyama, mimea na mandhari nzuri ambazo ni kivutio muhimu kwa utalii. Rais Magufuli, alisema hifadhi ya Burigi-Chato ina ukubwa wa kilomita za mraba 4,702 na kuifanya ishike nafasi ya tatu kwa ukubwa nchini.

Hifadhi inayoshika nafasi ya kwanza ni Ruhaha yenye kilomita za mraba 20,300 ikifuatiwa na Serengeti yenye kilomita za mraba 14,763 iliyoanzishwa mwaka 1959. Hifadhi nyingine mpya ni Ibanda – Kyerwa na Rumanyika – Karagwe ambazo zinafanya idadi ya hifadhi zote nchini kufikia 19, mapori ya akiba 23, mapori tengefu 44, hifadhi za misitu 463, misitu asilia 17 na mashamba ya miti 23.

Anasema nchi sasa ina eneo la hifadhi lenye kilomita za mraba 361,594 ambalo ni zaidi ya theluthi moja ya nchi kulinganisha na nchi zingine. Hifadhi hizo za Rumanyika, Ibanda na Burigi- Chato kutokana na ukubwa wake zimegusa takribani kila halmashauri za wilaya za mkoa huo wa Kagera ambazo ni Manispaa ya Bukoba, Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Missenyi, Karagwe, Kyerwa, Ngara, Biharamulo na Muleba.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kyerwa, Shadrack Mhagama, pamoja na kuelezea fursa za utalii za wilaya hiyo kupitia hifadhi ya kitaifa ya Ibanda, pia anaelezea fursa nyingine za utalii zinazopatikana katika halmashauri hiyo.

Anasema Kyerwa kuna mto Kagera unaopita kwenye halmashauri hiyo wenye urefu wa kilometa sabini. “Mto huu ni kivutio kizuri cha utalii kutokana na kupindapinda kwake na ni chanzo cha uwepo maziwa madogo takribani 25. Aidha, anasema pia kuna chemchemi ya maji ya moto ya Mtagata ambayo watalii wengi wakiwemo wakazi wa Kagera huenda kuitembelea wakiamini kuwa maji hayo ya moto yanatibu magonjwa mengi ikiwemo vidonda.

Anasema chemchemi hiyo ni ya ajabu kwa kuwa mtu anapochota maji kwa mikono yake huku akiwa ametulia kamwe haungui ingawa maji ni ya moto lakini anapochota maji huku akijitikisa huungua na kubabuka kabisa.

“Tayari tumetenga maeneo ya kuchotea maji kwa kuwa watembeleaji wa eneo hili ni wengi, wapo wanaokuja kutalii lakini wapo wanaochotoka maji kwa matumizi ya nyumbani,” anasisitiza Mhagama.

Anasema wametenga pia maeneo ya wanawake na wanaume ya kuoga kwa kuwa wengi hufika wakiwa na nia hiyo. Pamoja na hayo, mkurugenzi huyo anaelezea kivutio kingine cha utalii kinachopatikana katika halmashauri hiyo kuwa ni uwepo wa kilima cha Kabukokoro.

Anasema kilima hicho hupendwa na watalii kutokana na ukweli kuwa mtu akisimama kileleni huuona mto wote wa Kagera na namna ulivyopindapinda, huona Halmashauri ya wilaya ya Karagwe pamoja na nchi ya Uganda. Eneo la Nchi Tatu pia linapatikana katika halmashauri hiyo ya wilaya Kyerwa ambalo ni sehemu inayokutanisha mipaka ya nchi tatu kwa wakati mmoja yaani Tanzania, Rwanda na Uganda.

Anasema eneo hilo ni fursa ya utalii kwa kuwa pamoja na kukutanisha nchi hizo tatu pia lipo jirani na hifadhi ya Ibanda. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, Innocent Mkandala anasema pamoja na kuwepo kwa kivutio cha maporomoko ya mto Kagera pia halmashauri hiyo ina kanisa la Kijerumani lililotumiwa na majeshi wakati wa vita ya Tanzania na Uganda miaka ya 1970.

Ukifika katika mji wa Missenyi mabaki ya kanisa hilo yanaonekana dhahiri katika kilima pekee kilichopo katika mji huo huku chini yake ukipita mto Kagera. Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe nako zipo fursa lukuki za vivutio vya utalii ambapo nako pamoja na kuwa na sehemu kubwa ya mto Kagera pia sehemu ya hifadhi za Burigi Chato, Ibanda na Rumanyika inapita katika halmashauri hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Godfrey Mheluka, anasema katika eneo la utalii wa kiutamaduni au malikale, Karagwe kuna kisiwa cha Kawela maarufu Rwakanyinyi ambako ndiko alikozikwa Chifu Rumanyika aliyekuwa mtawala wa kabila la Wanyambo wa Karagwe. Anasema kisiwa hicho ndicho pekee nchini chenye kaburi la chifu na kina kivutio pia cha popo wa ajabu kutokana na ukubwa wao.

“Ukifika katika kisiwa hicho, katika eneo la kaburi utaona popo hao wakubwa mithili ya paka wakilizunguka kaburi hilo,” anabainisha.

Aidan Bahana ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ngara anabainisha kuwa katika halmashauri hiyo takribani asilimia 30 ya hifadhi ya taifa ya Burigi- Chato iko Ngara ambapo pia ipo hifadhi ya Ibanda na Rumanyika.

Anasema halmashauri hiyo ndio mlango wa nchi za Rwanda na Burundi kuingia nchini. Anasema pia kuna eneo maarufu la utalii ambalo linakutanisha mipaka ya nchi tatu ambazo ni Rwanda, Burundi na Rwanda ambapo kwa upande wa Tanzania, mpaka ni mto Kagera unaofahamika zaidi na Rwanda kama mto Akagera.

“Ngara tuna bahati kwani hapa pia tuna eneo linalokutanisha maji ya mito mitatu kutoka nchi tatu yaani Burundi mto Ruvuvu, Tanzania mto Kagera na Rwanda mto Akagera ambao unatengeneza maporomoko ya kuvutia katika eneo la Rusumo,” anafafanua.

Manispaa ya Bukoba yenyewe katika eneo la utalii pamoja na kuwa karibu kwa umbali wa kilometa 105 kutoka ya hifadhi ya Burigi Chato, pia manispaa hiyo ina mandhari nzuri inayotokana na ziwa Victoria.

“Hapa kuna takribani fukwe za kuvutia 15, miji katika visiwa zaidi ya 10,” anasema Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Benard Limbe.

Pamoja na hayo katika eneo la Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo unaweza kutembelea maeneo mbalimbali kama Ziwa Burigi, Kisiwa cha Rubondo, German Boma, Bwina peninsula na mazingira Kahugo.

Kwa sasa mkoa wa Kagera umeanza kutumia fursa hiyo ya uwepo wa vivutio vingi vya utalii ambapo kupitia Wiki ya Uwekezaji iliyomalizika hivi karibuni, mkoa ulihamasisha uwekezaji katika hoteli za kisasa za kitalii lakini pia ujenzi wa vituo vya utalii.

BAADA ya kupiga kambi kwa siku tofauti 15 katika vituo ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Weka maoni yako

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi