loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ni sahihi Kiswahili kutumika SADC

KISWAHILI ni kati ya lugha kongwe na yenye historia kubwa barani Afrika. Chimbuko na asili ya Kiswahili ni Pwani ya Afrika Mashariki hasa katika nchi ya Tanzania na baadhi ya maeneo ya Pwani ya Kenya.

Lugha ya Kiswahili ina wazungumzaji wengi Afrika, hali inayoiwezesha kushika nafasi ya tatu kwa lugha zenye wazungumzaji wengi zaidi ikiwa nyuma ya Kiarabu na Kiingereza zinazoshika nafasi ya kwanza na ya pili. Siku za karibuni Kiswahili kinazidi kupata umaarufu na kuchukua nafasi Afrika.

Hali hii inatokana na urahisi wa lugha hiyo kwa wanaojifunza na usawidi mzuri wa historia ya lugha ya Kiswahili katika mataifa mbalimbali Afrika hasa kisiasa na kibiashara.

Kisiasa, naona Kiswahili kupitia viongozi kama Mwalimu Nyerere walisaidia katika ukombozi wa nchi mbalimbali katika harakati za kudai uhuru kutoka kwa wakoloni.

Nchi mbalimbali hazikuwa nyuma kutumia Kiswahili katika shughuli za kitaifa. Kwa upande huu naona Kenya Kiswahili ni lugha ya taifa kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.

Tanzania Kiswahili ni lugha rasmi katika shughuli za kiserikali na hutumika kufundishia elimu shule ya msingi na hufundishwa kama somo sekondari na katika ngazi za vyuo.

Nchini Uganda Kiswahili zamani kilitumika katika Jeshi na Polisi lakini hivi karibuni Kiswahili pia kinatumika katika masuala ya biashara na utawala na hata katika sanaa. Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Kiswahili ni kati ya lugha nne za kitaifa.

Pia mataifa mengine yanaendelea kuweka mikakati juu ya kutumia Kiswahili kama vile Afrika Kusini na Sudan Kusini zilitoa maombi ya walimu wa lugha hiyo.

Wiki iliyopita, nchi za SADC chini ya Mwenyekiti mpya, Rais John Magufuli lugha ya Kiswahili imepitishwa kuwa moja ya lugha nne rasmi zinazotumiwa na mataifa hayo.

Kwa mantiki hiyo, naona mwelekeo mzuri wa lugha ya Kiswahili kwa viongozi mbalimbali. Nitoe wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa zinazotolewa hasa wataalamu wa Kiswahili wajitokeze pindi wanapohitajika.

Naomba Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iandae wataalamu wabobezi wa lugha hii ili wanapoenda katika nchi za watu (ughaibuni) kufundisha wasije kuiangusha nchi.

Ni vizuri pia kama serikali itaandaa mkakati kufanya tathmini ya wataalamu waliohitmu masomo yao vyuo mbalimbali nchini ili wawe na idadi kamili ya wataalamu wa Kiswahili.

Vilevile napendekeza serikali iwe na sera mahususi na mikakati kusisitiza matumizi ya Kiswahili kwa nchi za SADC ili jambo hili lipewe nafasi kubwa hasa barani Afrika.

Natoa wito pia kwa vyombo vya habari kukitangaza Kiswahili katika vituo vya redio, runinga na magazeti yatoe machapisho yatakayosaidia kukitangaza Kiswahili Afrika.

Pia wito wangu ni kwa Baraza la Kiswahili Taifa (BAKITA) washughulikie suala hili ili Kiswahili kisonge mbele kwani Bakita ndio wenye kanzidata ya wataalamu wa Kiswahili kitaifa.

foto
Mwandishi: SAMWEL HAMIS, UDSM

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi